in

Tuchel bila mastaa wa dunia atamudu Chelsea?

Marcos Alonso

WIKIENDI iliyopita nimewaangalia kwa mara ya kwanza Chelsea wakimenyana na klabu ya Burnley kwenye mfululizo wa Ligi Kuu England chini ya kocha mpya Thomas Tuchel. Kocha huyo ameongoza katika mechi mbili na kuvuna pointi 6 hivyo kuipandisha nafasi Chelsea.

Jina la Tuchel ni kubwa katika kandanda. Ukiangalisha sifa za Lampard na Tuchel ni mbingu na ardhi, kwa vile Mjerumani huyo anao uzoefu mkubwa katika kazi yake pamoja na kukabiliana na presha kubwa ya kuzinoa timu za mabilionea. Lampard alipewa Chelsea ikiwa ni mwaka mmoja tangu aingie kwenye ukocha. Kwahiyo hadi anaondolewa alikuwa amedumu kwa msimu mmoja na nusu, sawa na miaka miwili na nusu kwenye ukocha.

Waama, unapowatazama Chelsea wanavyocheza bado utaona hawajazoea kile anachokitaka Tuchel. Mojawapo ya mambo niliyokuwa namshangaa Frank Lampard ni uamuzi wa kumweka benchi mara kwa mara Calum Odoi. Si tu kijana huyo anacho kipaji cha kipekee bali namna anavyoweza kupangua ngome ya adui na kuwachosha mabeki pamoja na kutengeneza nafasi za kufunga.

Odoi ni winga ambaye anacheza kwa kasi za mawinga wa zamani Damian Duff, Steve McManaman, Luis Figo na wengine wenye kasi. Ingawaje Odoi hajafikia viwango vya mastaa niliowataja lakini naye anaonekana kuweza kutesa katika kizazi cha sasa.

Katika kikosi hicho Tuchel anaonekana kuwachezesha kwa kasi wachezaji wake pamoja na kuwabadilisha nafasi mara kwa mara akiwemo James aliyechezeshwa winga wa kulia. Kasi ya wachezaji wa Chelsea inaongezeka zaidi.

Mchezo wao dhidi ya Burnley ulionekana wazi kasi yao ilikuwa ya juu zaidi hivyo kuwafanya wakimbie kilometa nyingi kusaka ushindi. Kwa staili hiyo ya kucheza kwa kasi na kubadilishana nafasi ndani ya uwanja na kubeba majukumu mapya ni mtindo anaotumia Thomas Tuchel kwa muda mrefu kwenye kandanda.

Bahati mbaya Tuchel wa Chelsea siyo yule wa PSG wala Borussia Drortmund. Kwa mfano, akiwa PSG alikuwa mastaa wa dunia kama Neymar Junior, Julian Draxler, Angel Di Maria,Kylian Mbappe, Edinson Cavani na wengineo.

Kwenye kikosi chake kipya cha Chelsea, hakuna mchezaji mwenye hadhi ya Neymar Junior wala Kylian Mbappe. Hakuna mshambuliaji mwenye hadhi kama ya Edinson Cavani. Bahati nzuri amekukatana na beki wake wa zamani Thiago Silva ambaye anajulikana kwa umahiri na uongozi ndani ya uwanja.

Sasa kama Tuchel alishindwa kuwika akiwa na mastaa wa dunia Neymar, Marco Verrati, Mbappe na Cavani ataweza kuleta mafanikio akiwa na wacheaji wenye hadhi ndogo kama Mount, Odoi,Kurt Zouma,Pulisic, Kovavic, Timo Warner, Mendy, Kai na wengineo? Hilo ndilo swali la msingi ambalo linasubiriwa kupatiwa majibu. Mtoa majibu ni muda na namna Chelsea watakavyovumilia mwenendo wa Tuchel katika klabu hiyo.

Kimsingi tofauti za timu za PSG na Chelsea ni kwamba kule Ufaransa alikuwa na wachezaji wenye majina makubwa na wenye hadhi na ujuzi wa kumpa matokeo wakati wowote. Kwa Chelsea ndiyo kwanza wameingiza wachezaji wanaotajwa mastaa Timo Warner, Mendy, Thiago Silva na Kai lakini hawa hawawezi kuwa na ubora kama wa akina Mbappe na Neymar.

Jambo lingine ni ushindani wa Ligi Kuu England. Kule Ufaransa alikuwa anajishindia mara kwa mara na kutwaa ubingwa mfululizo. Lakini kwenye mashindano ya Ulaya hakufanikiwa kutamba. Mafanikio yake ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa simu uliopita hayakumletea taji baada ya kuambulia kichapo katika mchezo wa nusu fainali.

Kwa muktadha huo kila nikiwatazama  Chelsea naona wazi nyenzo za mafanikio kwa kocha huyo sio sawa na zile alizokuwa nazo PSG, wala ule uvumilivu uliokuwepo Borussia Dortmund haupo pale Chelsea. Makocha wengi wamefungashiwa virago kwa sababu mbalimbali ikiwemo “inategemea bosi Roman Abramovich ameamkaje”.

Na zaidi bado Chelsea wanacheza mpira uliokosa utulivu. Kuna wakati wanacheza vizuri kwa pasi za haraka, uhakika na mbinu, lakini dakika chache baadaye unaweza kuona wamepoteana na hakuna mawasiliano kati yao kuanzia safu ya ulinzi,kiungo hadi washambuliaji.

Hali hiyo kwa kiasi fulani inachangia wachezaji kukimbia kwa muda mrefu kutafuta mpira na kushindwa kukaa nao. Je, Tuchel atamudu vipi kuituliza Chelsea ambayo inaonekana kujitafuta?

Upande wa washambuliaji nako hali imekuwa butu. Katika mchezo wa wikiendi iliyopita mabao yote mawili yalifungwa mabeki wao wa pembeni. Marcos Alonso ambaye ni beki wa kushoto alipachika bao maridadi la pili baada ya nahodha wake Cesar Azpilicueta kutangulia kufunga la kuongoza.

Kwahiyo beki wa kulia na kushoto ndiyo waliompatia ushindi Tuchel katika mchezo wa wikiendi, lakini safu ya ushambuliaji bado haijaleta mabao ya kutosha hali ambayo inasababisha timu iwe na pointi chache pamoja na mabao machache ya kufunga. Je ni namna gani Tuchel atafufua makali ya safu ya ushambuliaji ya Chelsea? Hilo nalo ni swali la msingi linalongojea majibu kutoka klabu hiyo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Luis Suarez

Atletico Madrid timu ya ‘wazee’

Ibrahim Ajib

Natamani Ajib amweke benchi Chama!