in

Yuko wapi Meddie Kagere?

Magoli ya Meddie

Jina pekee lilitosha kuigopesha timu yoyote ile . Jina ambalo lilijengwa kwa udongo wa magoli. Alijenga imani ya uoga kwa wengi kwa sababu ya undugu wake na goli. Undugu ambao ulikuwa unamfanya yeye awe na uwezo wa kwenda kulisalimia goli kila wakati.

Goli lilijenga mazoea na yeye , likajenga urafiki na yeye , goli likawa limezoea kukutana na rafiki yake anayeitwa Meddie Kagere kila mwisho wa juma kiasi kwamba kila aliyekuwa anawaona Meddie Kagere na goli aliwaona kama marafiki walioshibana sana.

Ilikuwa ngumu kuamini kama kuna siku itatokea Meddie Kagere na rafiki yake goli wataacha kutembeleana hata siku moja. Ilikuwa ngumu mno kwa sababu tu walikuwa damu damu lakini cha kushangaza leo hii kila mmoja anajiuliza yuko wapi Meddie Kagere?

Tulizoea kumuona kwa rafiki yake goli wakiongozana mara kwa mara , kwa sasa hatuwaoni tena. Hata goli mwenyewe anajiuliza mengi sana kuhusiana na upotevu wa rafiki yake mpendwa Meddie Kagere , swali kubwa ambalo linazunguka kichwani kwa goli ni hili , yuko wapi rafiki yangu Meddie Kagere?

Meddie Kagere ambaye mabeki wa timu pinzani walikuwa wanahofia kukutana naye , walikuwa wanajiandaa mara dufu kila wakikutana naye wakiamini wanaenda kukutana na ushindani mkubwa lakini mabeki hao wamebaki na swali moja tu, yuko wapi Meddie Kagere?

Meddie ambaye ilikuwa ngumu kumpokonya mpira mguuni kwake , Meddie ambaye alikuwa na kasi ya kukimbia huku akikokota mpira, Meddie ambaye ilikuwa ngumu kumsukuma kwa sababu ya uimara wake, Meddie huyu ametubakizia na swali moja tu, yuko wapi huyu mtu?

Hata kipindi ambacho mashabiki wa timu pinzani walipoliona jina lake kwenye orodha ya wachezaji watakaoanza kucheza mioyo ya mashabiki ilikuwa inaenda kwa kasi sana, lakini mashabiki hawa wa timu pinzani na wenyewe wanajiuliza yuko wapi Meddie Kagere ?

Meddie Kagere ambaye kila alipokuwa anawafunga alikuwa anajiziba jicho moja , hii ndiyo ilikuwa ishara yake kubwa sana kila alipokuwa akafunga goli, ishara ambayo kwa sasa ni nadra kuiona ndiyo maana tunabaki kujiuliza yuko wapi Meddie Kagere?

Yuko wapi? Ameenda wapi? Hajui kila mmoja amemkumbuka sana? Hasikii kelele za mashabiki wa timu yake ya Simba? Kelele ambazo zinaonesha namna ambavyo wamemkumbuka comando wao waliombatiza kwa jina la Terminator.

Terminator ambaye alikuwa anawapa kiburi mashabiki wa Simba kila jina lake lilipokuwa linatokea kwenye karatasi yenye orodha ya wachezaji ambao walikuwa wanatakiwa kuanza kwenye mechi husika.

Walijiamini mno mbele ya Meddie Kagere, mbele ya Meddie Kagere waliamini kuwa wanaweza wakafanya chochote kile kwa kuamini kuwa muda wowote Meddie Kagere anaweza kuwapa ushindi kwenye mechi yeyote ile.

Lakini leo hii wamekaa kimya mashabiki hawa, ukimya ambao unakuja na swali moja tu, yuko Meddie Kagere? Meddie ambaye alikuwa anawapa raha na furaha kila mguu wake ulipokuwa unakanyaga uwanjani.

Kuna wakati mashabiki hawa walimpigia simu Mohammed Hussein “Mmachinga” kumpa taarifa kuwa Meddie Kagere anakuja kuvunja rekodi yake ya kufunga magoli mengi ndani ya msimu mmoja.

Meddie Kagere alitakiwa msimu huu afunge magoli 27 ili kuvunja rekodi ya Mohammed Hussein “Mmachinga” ambaye aliwahi kufunga magoli 26 ndani ya msimu mmoja.

Baada ya kupigiwa simu Mohamedd Hussein “Mmachinga” alimsubiri Meddie Kagere aje kuvunja rekodi yake lakini mpaka sasa hivi haoni dalili ya Meddie Kagere kufika, Mohamed Hussein naye kabaki na swali moja , yuko wapi Meddie Kagere?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Mabingwa

Simba kushusha vifaa vinne

David Molinga

David Molinga tishio jipya kwa Simba