BMT ifanye haya kukuza michezo

Yafuatayo ni mapendekezo 10 ambayo nadhani Baraza la Michezo la Taifa (BMT) linatakiwa kufanyia kazi ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini Tanzania.
Ni wazi kwamba watu hutofautiana na si wote watakubaliana na uchaguzi na masuala yenyewe, lakini kwa ujumla ningependelea zaidi kuona wadau wenye taaluma ya michezo wakihusishwa zaidi kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, lazima tufanye kazi kuhakikisha kwamba tunakuwa nao bega kwa bega ili Tanzania hatimaye ivuke na kufikia hatua ya juu zaidi kimataifa katika michezo.
BMT inatakiwa kurejesha mashindano ya michezo katika shule za msingi na za sekondari, ndiyo yale mashindano yaliyokuwa maarufu sana ya UMITASHUMTA na UMISETA. Mchango wa mashindano hayo ulikuwa mkubwa sana katika maendeleo ya michezo, kwani ndiko vipaji vipya vilikogunduliwa.
BMT inatakiwa kuhakikisha kwamba vyama vya michezo vinavyoundwa tangu ngazi za wilaya hadi mikoa vinaungwa mkono, kwani ndivyo vitaibua viongozi kutoka pande zote za nchi, watakaoshirikishwa kuanzia ngazi za chini hadi taifa. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na uongozi imara sana katika ngazi ya taifa.
Vyama vya mochezo lazima visaidiwe ili kurejesha baadhi ya mashindano yaliyofutwa; kama Kombe la Bonite Moshi kwa upande wa mpira wa wavu. Ushauri wangu kwa BMT ni kuwasiliana na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi kutafiti njia murua ya kurejesha tena mashindano hayo.

Mhe Rais Jk Kikwete, akizungumza na wanamichezo kabla ya michezo ya Olimpiki 2012, London
Mhe Rais Jk Kikwete, akizungumza na wanamichezo kabla ya michezo ya Olimpiki 2012, London

Kwa maoni yangu, kudidimia kwa mpira wa wavu Tanzania kulianza Kombe la Bonite lilipofikia kikomo. Itungwe sheria na kanuni iwepo, kuvielekeza vyama vya michezo vya taifa kuwa chini ya ofisi moja yenye mawasiliano muhimu kama simu, mtandao wa intaneti na vifaa vingine muhimu kwa ofisi, vitakavyowarahisishia mawasiliano.
Kwa sasa ofisi zimekuwa kama za kwenye mikoba ya watu binafsi, ambapo wanashikilia nyaraka mbalimbali, hata zile muhimu majumbani mwao, jambo linalofanya kukosekana ufanisi kimawasiliano na pia katika utunzaji kumbukumbu na kutunza historia ya vyama husika inavyopaswa.
Lazima maboresho yafanywe ili vyama vya michezo viweze kufanya kazi pamoja na kwa karibu zaidi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuibua na kukuza vipaji na kuwafanya wachezaji kuwa na ushindani mkubwa kimikoa, kitaifa na kimataifa.
BMT itoe muhtasari utakaokuwa na dira na mwongozo wa utawala bora itakayotakiwa kufuatwa na vyama vya michezo, ili kuepuka migogoro na mizozo isiyo na msingi inayopelekea BMT kujitwisha wajibu wa kuwa mithili ya mahakama na kutumia muda mwingi katika kupokea, kupitia na kuamua rufaa.
Upo umuhimu mkubwa kwa maandalizi ya timu zinazoshiriki michezo katika ngazi ya taifa kufanywa kitaaluma zaidi, iwepo mipango mizuri na ya kueleweka katika masuala kama mafunzo, aina ya vyakula vinavyotakiwa na upatikanaji wake, matibabu michezoni na kuwafunda wanamichezo kisaikolojia.
Ukweli ni kwamnkba haya yanaweza kufanywa kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe, kutoka Kitivo cha Michezo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi nyingine za elimu nchini Tanzania.
BMT iishauri serikali na kuweka kiungo kwa wawekezaji wanaokuja Tanzania kwa ajili ya kuchangia sekta ya michezo ili watoe sehemu ya mapato yao kujenga viwanja muhimu vya michezo vinavyohitajika na viwe katika viwango vya kimataifa.
Miaka 50 baada ya uhuru, kwa mfano, hatuna bwawa la kuogelea linalokidhi viwango vya kimataifa (50 x 25 m). Jambo hili linadhoofisha hata vyama vya kuogelea, kwa sababu hakuna mahali waogeleaji watarajiwa au hata waliofuzu kwingine wanakoweza kwenda kufanya mazoezi, achilia mbali kushindana.
BMT ifanye tathmini mara kwa mara kwenye uongozi wa vyama vya michezo ili kuhakikisha vina tija na ufanisi, hasa pale inapotokea viongozi wale wale wamekuwa madarakani kwa muda mrefu au chama kinadumaa.
Mwisho, lazima tovuti itengenezwe na iwe inafanya kazi kwa ajili ya kuwezesha wanamichezo na wadau wake kuwasiliana kwa urahisi. Hiyo itafanya kazi kama jukwaa muhimu la kukusanya mawazo na ushauri juu ya jinsi ya kuendeleza vyama na michezo nchini.
Jukwaa hilo, pamoja na mambo mengine, litawezesha upokeaji mawazo na ushauri kutoka nje ya nchi na kuasiliwa Tanzania. Kwa mfano, nchini Uingereza kuna mashine maalumu za kufanya mazoezi ya kuweka sawa mishipa ya moyo, nayo ipo kwa ajili ya umma (hazihamishiki).
Vifaa hivyo huwezesha watu wa kawaida wanaokimbia mbio za pole au wapendao kutembea kwenye viwanja vya michezo kujiweka sawa kiafya pasipo kuingia gharama yoyote. Hili lingeweza kufanywa nchini Tanzania kwa msaada wa kampuni kama Vodafone, Tigo, TBL, SBL nk.
Haya ni mawazo na michango yangu kwa ajili ya maendeleo ya michezo kwa nchi yetu. Ni wazi kwamba chipukizi wanategemea BMT iwasaidie katika kutambua vipaji vyao, kuviendeleza na kuwapa upeo mkubwa kwa kuviendeleza. Labda siku moja tutakuwa na shujaa wetu katika michezo atakayetoa mfano kwa vijana.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kocha mwingine EPL atema mzigo

30 TWIGA STARS WAITWA KAMBINI