in

Harmonize kupeleka Bongofleva bungeni?

Harmonize

WENGI wamezoea kumwona Rajab Abdul Kahali kama raia wa kawaida. Lakini linapokuja jina la Harmonize hali inakuwa tofauti. Ni ina kubwa kwenye miondoko ya Bongofleva. Anajua kuimba. Anajua kusakata muziki. Anajua kutunga mashairi. Anaujua muziki wake vema. Amepata mwanamke mrembo.

Muziki umempa mafanikio makubwa ya kiuchumi na heshima. Anaheshimika na viongozi wa serikali. Anaheshimika na wadau wa muziki. Anaheshimika na wafanyabiashara wa muziki. Anapendwa na vijana wengi wanaopenda Bongofleva. Ameimba mbele ya ugeni mzito. Amekuwa kipenzi cha Rais wa Tanzania, John Magufuli. Amekuwa nyota analiyepikwa na nyota mwingine Diamond Plutanumz. Ni kijana kutoka mkoani Mtwara. Ni shabiki wa michezo hususani mchezo wa soka. Timu yake anayoipenda ni  Ndanda F.C ya mkoani Mtwara.

Penginesio suala  kuimba pekee, bali hata kusaidia jamii kunamfanya mwanamuziki Harmonize aendelee kuwa gumzo miongoni mwa watanzania. Jina lake rasmi ni Rajab Abdul Kahali lakini amekuwa maarufu kwa jina la jina maarufu Harmonize.

‘KONGE GANG, KONDE BOY’

Wengi wanamkumbuka mwanamuziki huyo ambaye alichukua uamuzi mgumu wa kujiondoa katika Lebo ya muziki ya Wasafi na kuanzisha yak wake, Konde Gang. Pia kujiita ‘Konde Boy’ ina maanisha ni “Kijana wa Kimakonde”. Neno ‘Konde’ linatokana na jina la kabila la Wamakonde wanaoishi katika mkoa ya kusini ya Lindi,Mtwara na Ruvuma.

Harmonize amewahi kuingilia kati na kuokoa jahazi wakati klabu ya nyumbani kwao ya Ndanda F.C  ya mkoani Mtwara kwa kutoa fedha za kusafiri kwenda  kucheza mechi ya Ligi Kuu katika mkoa mwingine.

Alikuwa Harmonize ambaye alitoa fedha zake ambazo zilisaidia kuisafirisha timu hiyo. Mwanamuziki huyo alifanya hivyo kama njia ya kurudisha faida kwa jamii ikiwemo kusaidia nyumbani kwao.

Vilevile Harmonize amekuwa akijihusisha na matukio ya mchezo wa soka kila mechi wanayocheza klabu ya Ndanda F.C amekuwa akihuhuduria viwanjani sambamba na mashabiki wa timu hiyo. Anashiriki kuishangilia Ndanda F.C, akipiga ngoma na kuhamasisha wenzake.

HARMONIZE ATAINGIA KWENYE SIASA?

Rais John Magufuli alifungua mjadala baada ya kueleza kuwa anatamani msanii wa Harmonize kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara.

Vyombo vya habari vimewahi kuripoti kuwa Rais Magufuli alisema kuwa anatamani kumwona Harmonize akiwa bungeni. Magufuli aliyesema hayo mwaka jana 2019 katika mkutano wa hadhara mkoani Lindi, mara baada ya msanii huyo kutumbuiza katika mkutano huo.

Harmonize amekuwa akitumbuiza katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanya rais Magufuli mara baada ya kutoa wimbo wake wa “Magufuli”.

Wimbo huo wa Magufuli ulioimbwa kwa mdundo wa wimbo wake wa zamani ya “Kwangaru”, umemsifu Magufuli kwa kazi aliyoifanya katika taifa hilo.

“I wish ningemuona Magufuli nimpigie magoti na kumpongeza hadharani…mchapakazi hachoki…Fly over sasa tunazo, Airport imeshajengwa…acha nikupongeze kwa Air Tanzania…” anaimba Harmonize kwenye wimbo wa Magufuli.

Lakini swali ni je, mwanamuziki huyo ataonesha nia kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2020 ambao maandalizi ya uchaguzi tayari yameanza?

Iwapo Harmonize atagombea wadhifa huo wa ubunge basi anaweza kuwa msanii wa kwanza maarufu kuchukua kiti cha ubunge kupitia chama tawala (CCM).

KUFUATA NYAYO ZA WAKONGWE?

Katika ukanda wa Afrika mashariki , mwanamuziki kuwa mwanasiasa sio jambo geni. Tayari tunao wanasiasa gozi ambao ni wabunge ingawa wote wanatokea chama cha upinzani.

Msanii wa bongofleva Joseph Haule (Profesa Jay) alipata ubunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro tangu mwaka 2015 mpaka sasa. Wimbo wa ‘Ndiyo Mzee ulimpatia umaarufu mkubwa mwanamuziki huyo ambao ulikuwa unaeleza namna viongozi wanaweza kutoa ahadi bila kutekeleza.

Msanii mwingine maarufu ni Joseph Mbilinyi (Mr.Two au Sugu) ni mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha upinzani cha CHADEMA tangu mwaka 2010 hadi sasa. Mwaka 2018, Joseph Mbilinyi alishtakiwa kwa kumtumia lugha ya fedheha dhidi ya rais Magufuli na kutumikia kifungo cha miezi mitano.

Huko nchini Uganda, mbunge wa jimbo la Kyadondo mashariki ni Robert Ssentamu ambaye ni maarufu kwa jina la Bobi Wine. Mwanamuziki huyo kwa sasa amekuwa mwiba mchungu kwa utawala wa rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akiwa anakubalika na kuwavutia maelfu ya vijana ambao wanamuunga mkono.

Bob Wine alishinda kiti cha ubunge mwaka 2017 akiwa mgombea binafsi baada ya kutojiunga na chama chochote.

Msanii nyota mwingine kutoka nchini Uganda, Jose Chameleone (Joseph Mayanja) aliongoza wanamuziki nyota nchini humo kuimba wimbo wa kumsifu rais Museveni katika kampeni wa “Tubonga nawe” mwaka 2015, lakini alipotangaza nia mwaka huu kuingia kwenye siasa rais Museveni alifuta urafiki na Chameleone.

Chameleone ambaye ni mmoja wa wanamuziki maarufu katika eneo la Afrika Mashariki. Moja ya nyimbo zake zinazofahamika ni ule wa “Shida za Dunia”, unaozungumzia matatizo yanayowakabili watu.

Mwanamuziki huyo anayewania umeya wa Jiji la Kampala alisema, “Wakati huduma zinapokuwa katika hali mbaya, watu wanaanza kuamka …Watu wana kiu ya uongozi unaofaa na hawajaupata. Wale wanaodhani kuwa ni mkumbo wa Bobi Wine wana ukweli kiasi kidogo sana,” Chameleone alinukuliwa akisema hayo mwanzoni mwa mwezi Juni.

Huko nchini Kenya mwanamuziki Charles Njagua Kanyi (Jaguar) alishinda kiti cha ubunge wa jimbo la Starehe jijini Nairobi kupitia tiketi ya chama tawala cha Jubilee mwaka 2017.

Jaguar ni mwanasiasa mwenye mvuto kwa vijana na wanawake nchini humo. Hivi karibuni mwanamuziki huyo alishtakiwa kwa kutoa kauli ya chuki dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni nchini humo.

HARMONIZE KWENDA BUNGENI?

Swali hili linajibiwa kwa matamanio yake aliyoyasema mkoani Lindi, ikiwa na maana kuwa Harmonize anaweza kuwania ubunge katika jimbo la Tandahimba endapo atafuata ushauri wa rais Magufuli. Je, hilo litawezekana na atapeperusha Bongofleva hadi Bungeni?

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Liverpool FC

Mechi kumi zilizompa ubingwa Liverpool

SIMBA

SIMBA BINGWA 2019/2020