in

Natamani Ajib amweke benchi Chama!

Ibrahim Ajib

Natamani sana hiki kitokee lakini swali kubwa ambalo linabaki kichwani kwangu kitawezekana hiki kitu? Itawezekana miguu ya Ibrahim Ajib kuwa na macho kama ambavyo miguu ya Claoutus Chota Chama?

Miguu ambayo hutoa pasi nyingi za mwisho, pasi ambazo husababisha magoli. Miguu ambayo macho yake huona nyavu na kupeleka mpira kwenye nyavu. Hii miguu Ibrahim Ajib atakuwa nayo?

Kuna mtu ananiambia wakati Ibrahim Ajib yupo kwenye klabu ya Yanga alifanikiwa kufikisha pasi ishirini (20) za mwisho zilizozaa magoli. Pasi ambazo zilimfanya ndani ya msimu huo kuwa mchezaji ambaye ametengeneza magoli mengi kuzidi wachezaji wote.

Ndani ya msimu huo pia alifanikiwa kufunga magoli saba (7). Kiwango hiki kilikuwa kiwango bora kwa Ibrahim Ajib tangu aanze maisha yake ya mpira wa miguu. Hajawahi kuwa na kiwango kikubwa kama hiki alichokuwa nacho Yanga.

Lakini mshangao mkubwa kwa Ibrahim Ajib ni yeye kushindwa kukiendeleza kiwango hicho alichotoka nacho Yanga mara baada ya yeye kusajiliwa ndani ya kikosi cha Simba SC, kwa kifupi alikosa mwendelezo.

Mwendelezo ambao umeshindwa kumpa nafasi ndani ya kikosi cha Simba Sc mbele ya mwamba wa Lusaka, Claoutus Chota Chama. Kitu ambacho kinakosekana kwa Ibrahim Ajib ndicho kitu ambacho kinapatikana kwa Claoutus Chota Chama.

Ibrahim Ajib atakosa mwendelezo wa kiwango chake lakini Claoutus Chota Chama atakuhakikishia mwendelezo wa kiwango chake ndiyo maana Ibrahim Ajib anakosa nafasi mbele ya mwamba wa Lusaka.

Natamani sana Ibrahim Ajib aamke. Natamani sana apate namba kwenye kikosi cha Simba. Kipaji chake ni kikubwa sana lakini kinakosa jitihada ambazo zinaweza zikamfanya yeye afike sehemu ambayo ni kubwa.

Kipaji chake kinahitajika sana kwenye timu yetu ya taifa ya Tanzania. Timu yetu ya taifa inatatizo moja la kutokuwa na mchezaji anayeweza kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.

Mchezaji ambaye ataunganisha eneo la kiungo cha kati na eneo la ushambuliaji. Mchezaji ambaye ana uwezo wa kufunga magoli kipindi ambacho safu ya ushambuliaji imebanwa kufunga magoli.

Mchezaji ambaye ana uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za magoli kwa washambuliaji. Mchezaji huyu hatuna kwenye timu yetu ya taifa. Lakini Ibrahim Ajib anasifa zote kwenye haya mahitaji yetu.

Kinachokosekana ni jitihada za kuhakikisha kipaji chake kinang’ara kama ambavyo alifanya akiwa Yanga. Kwa bahati mbaya kwa sasa yuko sehemu ambayo kuna viungo wengi ambao ni wabunifu.

Viungo ambao wana jitihada kubwa kuzidi yeye. Jitihada hizi za viungo hao wa Simba zinatakiwa kumwamsha Ibrahim Ajib , hatakiwi kuwa mnyonge na kudumaa kwa sababu ya upinzani mkubwa ndani ya kikosi cha Simba SC.

Anachotakiwa ni yeye kuhakikisha anapambana kwa ajili ya kipaji chake. Natamani sana Ibrahim Ajib siku moja awe na namba ya kudumu ndani ya timu ya Simba SC wakati matamanio yangu nikiwa nayaandika naombeni mnifikishie kwake ujumbe wa yeye kuhakikisha anawekeza juhudi na maarifa ndani ya kipaji chake.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Marcos Alonso

Tuchel bila mastaa wa dunia atamudu Chelsea?

soufiane rahimi

Sofiane Rahimi ni ‘hirizi’ ya Morocco