in

Atletico Madrid timu ya ‘wazee’

Luis Suarez

Wakati Luis Suarez anasajiliwa Atletico Madrid mtu mmoja alikuwa amechukia mno na kudai kuwa uamuzi huo ulichukuliwa kwa kukurupuka huku ukiacha klabu ya Barcelona bila mwelekeo wala mpango mbadala wa kunyakua wachezaji mahiri.

Mtu huyo alikuwa Lionel Messi ambaye aliandika maelezo marefu katika mitandao ya Kijamii kumshukuru na kumtakia kila la heri Luis Suarez katika maisha mapya jijini Madrid.

Wiki hii Kocha Diego Simeone ametamka mpango mwingine wa kuwasajili wachezaji wazee. Mpango wake unahusu kuwasajili Mesut Ozil wa Fenerbahce  na Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan.

Kwa mtazamo wa Lionel Messi aliamini kuwa Suarez bado anao uwezo wa kutoa mchango mkubwa kwa mafanikio ya Barcelona. Aliamini Barca ilimhitaji Suarez kuliko kukumbatia makinda ambao hawana uzoefu. Aliamini kuwa Suarez angefaa kuwafundisha chipukizi hao ili waweze kunufaika na ujuzi wake.

Hata hivyo bodi ya Barcelona ikaamua  kumpiga bei kwa Atletico Madrid. Bila kupepesa macho Atletico Madrid walimnyakua staa huyo wa Uruguay na kumpa namba katika kikosi cha kwanza.

Wakati akimnyakua staa huyo kwenye kikosi chao alikuwepo Alvaro Morata, Joao Felix na Diego Costa. Usajili wa Luis Suarez ukaendeleza dhana ya kuwa Atletico Madrid kwa sasa imegeuka kuwa timu ya wazee kuliko ilivyokuwa moto wa kuotea mbali miaka ya nyuma. Kwamba ule utambulisho wao wa kuibua vipaji vya washambuliaji wanaokuja kutesa Ulaya umetupwa kando.

Zipo sifa kubwa za Atletico Madrid katika soka, mojawapo ni kuwaibua washambuliaji hatari zaidi. Namba 9 yeyote anayepitia Atletico Madrid huwa anakuwa tishio mbele ya lango la adui.

Katika maisha yao ya soka wamekuwa na kawaida ya kuibua washambuliaji ambao wanakuja kutamba Ulaya na dunia. Ushahidi wa kwanza ni Sergio Kun Aguero ambaye kwa sasa ndiye mshambuliaji namba moja wa Manchester City.

Nyota huyo wa Argentina alicheza kwa mafanikio Atletico Madrid kabla ya kuuzwa kwenda Man City. Ni kama wengi walivyoamini wakati Atletico Madrid kuwa ingeporomoka baada ya kumuuza mshambuliaji wao nyota Fernando Torres kwenda Liverpool.

Kuondoka kwa Torres kwenda Liverpool nako kulichukuliwa kama moja ya sababu ya timu hiyo ni kutafuta fedha ili kuboresha bajeti zao. Hata hivyo kuondoka kwa nyota hao kulitafsiriwa kuwa Atletico inafanya kazi ya kutengeneza washambuliaji wakali na kuwauza kwa bei kubwa.

Radamel Falcao ni miongoni mwa nyota waliowahi kutamba katika kikosi cha Atletico Madrid. Falcao naye alikuwa mshambuliaji hatari La Liga na alijizolea sifa nyingi kabla ya kuwahama miamba hao wa jiji la Madrid.

Wengi wanamkumbuka Diego Costa ambaye aling’ara Atletico Madrid kabla ya kuhamia Chelsea. Umahiri wa kupachika mabao wa Costa ulibeba sifa zilezile za washambuliaji hatari wa Atletico Madrid. Ubora na uwezo wake vilisababisha malumbano kati ya Brazil na Hispania ambao kila mmoja alitaka Costa achezee nchi zao. Diego Costa ni mzaliwa wa Brazil ambaye ana uraia wa nchi mbili yaani Brazil na Hispania.

Misimu kadhaa baadaye Diego Costa, Fernando Torres walirejea klabuni hapo kwa nyakati tofauti. Umahiri wao wa kupachika mabao ulikuwa umeshuka lakini walibakiwa na ufundi na hamasa iliyowasaidia chipukizi kukuza viwango vyao. Kwa hatua ya kuwarejesha Torres na Costa ni wazi Atletico Madrid imekuwa timu ya wazee siku hizi badala ya kuibua washambuliaji hatari.

Kwanini nasema ni timu ya wazee? Wiki hii Kocha Diego Simeone ametamka mpango mwingine wa kuwasajili wachezaji wazee. Mpango wake unahusu kuwasajili Mesut Ozil wa Fenerbahce  na Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan.

Diego Simeone amekaririwa na vyombo vya habari akisema, “Msimu ujao ikiwezekana tutawasajili Mesut Ozil na Zlatan Ibrahimovic ili kuungana na Luis Suarez katika safu ya ushambuliaji. Tunawahitaji hawa wachezaji wanaoonekana wazee na wameishiwa makali. Wakati tunamsajili Suarez wengi walilaumu umri wake na kwamba tumesajili mzee. Sisi sio klabu tajiri yenye fedha wala bajeti ya kufa mtu, lakini tuna uhakika na uwezo wetu wa kuwashawishi wachezaji wa namna hiyo kujiunga timu yetu. Suarez alipata ofa kutoka timu mbalimbali lakini alichagua kujiunga Atletico Madrid. Kwahiyo tukiwa na Ozil na Zlatan tuna imani tutashindana na wababe wengine Ulaya na kuwapa somo wachezaji wetu vijana.”

Kocha Simeone anayo hoja kwa sababu kuu mbili; kwanza klabu yake haina uwezo mkubwa kifedha hivyo kushindw akushindana na zingine sokoni, pili wachezaji wazee wamekuwa wakiendelea kung’ara kwenye vilabu mbalimbali.

Zlatan yupo AC Milan ambako ameipa uhai timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu Italia. Edinson Cavani naye ni mzee ambaye anawapa changamoto vijana wa Manchester United ingawa hakuchezea Atletico Madrid lakini anaingia katika hoja hii.

Hii ina maana wachezaji vijana wa Atletico Madrid kama vile Joao Felix wanatakiwa kujifunza mengi kutoka kwa wazee hao. Alvaro Morata ambaye alisajiliwa Atletico Madrid akitokea Chelsea naye hakufua dafu Wanda Metropolitano hivyo akauzwa kwenda Juventus Turin mahali ambako alicheza ka mafanikio kabla ya kurejeshwa Real Madrid.

Kushindwa kung’ara Real Madrid na Chelsea kulimpa nafasi Diego Simeone kumsajili Morata na kudhani angekuwa moto wa kuotea mbali katika kikosi chake. Akiwa anawakilisha wachezaji vijana Alvaro Morata hakung’ara hivyo akauzwa kwenda Juventus.

Ujio wa Luis Suarez ndiyo umeinua kiwango cha kufumania nyavu cha Atletico Madrid ingawaje alichukuliwa kuwa mzee. Misimu kadhaa iliyopita Atletico Madrid ilikuwa na wazee Diego Godin na Gabi ambao waliruhusiwa kuondoka. Kwa sasa kuwafikiria Ozil na Zlatan inaonesha Atletico Madrid wana imani zaidi na wachezaji wazee siku hizi kuliko vijana. Na isemwe Atletico Madrid imekuwa timu ya wazee.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Newcastle United

Ushindi umebadili kila kitu kwa Newcastle

Marcos Alonso

Tuchel bila mastaa wa dunia atamudu Chelsea?