in , , , ,

Skudu wa burudani, Yanga ni watoa dozi Afrika

Hii ni Yanga ya kugawa  dozi…

Ni Yanga ya Miguel Gamondi. Ndivyo unavyoweza kusema kwa sasa. Uwezo wao wa kuzuia, kushambuliaji, kujihami kwa pamoja ni miongoni mwa sababu za kuifanya timu hii iwe moto wa kuotea mbalimbali. sifa ya Yanga ya Miguel Gamondi ni hamasa, ari na njaa ya kusaka ushindi. Wakicheza mfumo wa 3-5-1-1, Yanga walikuwa wakifurahia mchezo wao. TANZANIASPORTS katika tathmini yake imebaini kuwa Yanga kuna matukio kadhaa ambayo yanasisimua kuwashuhudia mabingwa hawa wa soka wa Tanzania, walioanza mchezo bila nahodha wao Bakari Mwamnyeto.

NUSU KWA NUSU

Mchezaji yeyote anayepangwa kikosi cha kwanza Yanga anafahamu kuwa pale benchi kuna mwingine mwenye uwezo kama yeye. Wakati El Marreikh wakifikiri wangeona washambuliaji wawili kwenye safu ya Yanga, hali ilikuwa tofauti kwa kocha Gamondi. Yeye alimwanzisha Kennedy Musonda kwenye safu ya ushambuliaji huku Aziz Ki akiwa nyuma yake. Hii ina maana benchi la Yanga lilikuwa na mshambuliaji mwingine aliyewekwa kama silaha ya kuimaliza El Marreikh. Ni mshambuliaji Clement Mzize ambaye aliingia kipindi cha pili na kutekeleza matakwa ya kocha wake. 

Tanzania Sports

HAWASOMEKI KIMBINU

Wakati El Marreikh wakiwa wamejiamini kupindukia na wakifanya jitihada za kusaka mabao bila mafanikio, walijikuta wakipambana na mfumo mpya kipindi cha pili. Katika mfumo mpya wa 3-4-3 Yanga waliongeza chachu ya kusaka mabao, huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Clement Mzize na pamoja na Pacome Zouzoua. 

Mfumo mfumo unawawezesha Yanga kushambuliaji kwa pamoja na kujilinda kwa pamoja. Wakati Dickson Job na Ibrahim Bacca wakibaki kwenye mstari wa katikati ya dimba ili kujihami dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza, viungo wao wote walikuwa wanaliandama lango la El Marreikh. 

Kwahiyo El Marreikh walikuwa na kazi ya kudhibiti kasi ya Yanga katika mfumo tofauti. Katika kipindi hiki wachezaji wa nakshi nakshi ndiye walikuwa wameongezwa. Mpira ukinda kwa Pacome Zouzoua unachezwa kwa ubunifu mkubwa, hali kadhalika kwa beki wao w akushoto Lomalisa Mutambala. Ubunifu wa wawili hawa ulikuwa wa aina yake na ulichangia viungo wa El Marreikh na beki wao wa kulia kushindwa kuvuka mstari wa katikati mara kwa mara kwa lengo la kuhofia mashambulizi yao.

SOKA LA NGUVU-KAZI

Yanga ya Gamondi inacheza soka la shoka. Ni mpira wa kikubwa ambao unaweza kuwafikisha mbali. Wachezaji wanaonesha uzoefu katika mashindano ya kimataifa. Hawana presha katika kuipigania Yanga wala kutishwa na wapinzani wao. Waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 jijini Kigali nchini Rwanda katika uwanja wa Kigali Pele. 

Katika mchezo huu wao wa marudiano Yanga walicheza kana kwamba hawana uhakika wa kufuzu. Walitafuta bao kwa mwanzo hadi mwisho. Mashambulizi yao yalionesha bayana kuwa Yanga wanaweza kuifunga timu bila kujali ukubwa wao. Aina ya soka la Gamondi na wachezaji alionao walicheza kana kwamba mechi hiyo ni ya kufa na kupona.

SILAHA NZITO DAKIKA 90

Dakika zote 90 za mchezo Yanga walitumia silaha zao muhimu. Silaha yao ya kwanza ni beki w akulia Yao Atuolla, kisha kuna ufundi wa hali ya juu wa Lomalisa Mutambala. Mashambulizi ya mabeki hawa wa pembeni yalikuwa mwiba kwa El Marreikh. Uthibitisho wa umahiri wao ni namna Lomalisa alivyopiga bao la ushindi ambalo litiwa kimyani na Clement Mzize. 

Krosi maridadi iliyopigwa kutoka winga ya kushoto na guu la kushoto la Lomalisa Mutambala ilitua kichwani mwa Mzize na kuiandikia timu yao la ushindi. Silaha nyingine ni eneo la kiungo ambalo liliongozwa na Khalid Aucho na Mudathir Yahya. 

Viungo wawili hao walitumika kuficha mipira mingi na kupoozesha kasi ya El Marreikh kila walipotaka kuleta hatari. Aucho aliweza kuwalamba chenga, lakini Mudathir Yahya alikuwa moto wa kuotea mbali. Viungo hawa wanatumika kusukuma timu pinzani kwenye lango lao.

KUNA MAXI BILA MAYELE

Ingawa Yanga hawana Fiston Mayele, lakini kikosi chao kina Max Nzengeli. Mshambuliaji huyu amekuwa mahiri tangu atue yanga. Ni silaha ambayo inatumika kuleta ubunifu na kuzifumua safu za ulinzi za upinzani. El Marreikh walishindwa namna ya kumdhibiti kiasi kwamba wakawa wanamchezea rafu mara kwa mara. Maxi aliwafanya mashabiki wa Yanga wajiamini zaidi. Ni mchezaji ambaye anazifungua safu za ulinzi na kutengeneza mabao.

TANZANIASPORTS inafahamu kuwa Maxi kazi yake ya kwanza ni kuhakikisha Yanga wanapata mabao, hata kama yeye hafungi. Ni mchezaji wa kitimu, anayeifanya safu ya ushambuliaji kuwa na uhai wakati wa mchezo. Anaweza kusaidia ulinzi na kushambulia kwa kushtukiza pia. Ni mchezaji wa dakika 90, licha ya Gamondi kuweza kuamua vinginevyo.

BAO LA MASTAA WAWILI

Clement Mzize baada ya kufunga bao la ushindi alishangilia kwa mtindo wa nyota mwenzake wa zamani Fiston Mayele, lakini wakati akimalizia ushangiliaji wake akaja na staili ya staa mwingine aliyewahi kutikisa Afrika. Mwaka 1990 katika fainali za Kombe la Dunia, mshambuliaji wa Cameroun Roger Milla alikuwa maarufu kwa staili ya ushangiliaji wa kukata mauno kana kwamba anacheza muziki kila alipopachika bao alikimbilia kwenye kibendera na kucheza. Clement Mzize alianza staili ya Mayele kisha akamaliza kukata mauno kama Roger Milla. Inasemwa mpira ni burudani, hakika Mzize alilenga hilo.

UAMUZI WA HARAKA

Sifa kubwa ya Migeul Gamandi ni kufanya maamuzi upesi bila kusubiri. Anapokuwa kwenye eneo lake anausoma mchezo, anapanga karata zake. Upesi anaweza kuchukua maamuzi ya kumtoa mchezaji asiyetegemewa. Katika pambano la kwanza alimtoa Mudathir Yahya na nafasi yake ikachukuliwa na Kennedy Musonda. 

Wengi walitarajia kuona Clement Mzize angetolewa katika mechi ile, lakini hali ikawa tofauti. Gamondi aliwaeka pambano Musonda na Mzize, na ndio waliofunga mabao katika mchezo ule. Pambano la pili amemweka benchi Mzize na kumwanzisha Musonda. Lakini kipindi cha pili akafanya mabaidliko mengi ya kumtoa Khalid Aucho katika hali ya kushangaza. Lakini mabaidliko yake yaliifanya Yanga iwe ileile na ikapata bao la ushindi.

SKUDU ANAPENDWA

Winga raia wa Afrika kusini Skudu Makudubela anapendwa na mashabiki. Anaonekana kama mchezaji wa burudani. Washabiki wanapenda vituko vyake, uchezaji wake, kasi yake na uwezo wa kupangua safu ya ulinzi wa timu pinzani. Katika mchezo dhidi ya El Marreikh Skudu aliingizwa kiwanjani dakika za mwisho. 

Ziliibuka shangwe katika majukwaa ya mashabiki wa Yanga. Ni ishara kuwa huyo amekuwa mchezaji kipenzi ingawa bado hajaweka alama uwanjani. Kabla ya kuingia nahodha wake Bakari Mwamnyeto alikuwa anamhamasisha na kucheka naye wakati akiajindaa kuingia. Ni dhahira hata wachezaji wa Yanga walifurahi kumwona staa huyo wa Afrika kusini. Ni mchezaji wa burudani Yanga. 

USHINDI POPOTE

Yanga walishinda Kigali Pele nchini Rwanda. Wameshinda tena mchezo wa marudiano jijini Dar es salaam. Ushindi wao ni kama ilivyokuwa msimu uliopita. Walishinda ugenini mechi nyingi, Afrika kusini, Tunisia na Algeria. Walipata matokeo mazuri katika viwanja vigumu na kudhahirisha kwao popote pale wanagawa dozi. Hii ni Yanga ya kugawa  dozi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Baraka Majogoro anawinda AFCON kimya kimya

Tanzania Sports

SIMBA WAMENGURUMA BILA DOZI NENE