in , , ,

SIMBA WAMENGURUMA BILA DOZI NENE 

MECHI iliyojaa hofu, wachezaji kukosa umakini ndani ya dakika 45 za kwanza wakati miamba ya soka Tanzania ilipojikuta ikiruhusu bao mapema na kuwaweka matumbo joto maelfu ya mashabiki wao na wadau wa soka Tanzania, lakini Simba wamethibitisha kuwa wao wanalijua vema soka la Afrika na wana uzoefu mkubwa linapofika suala la mashindano ya Kimataifa. 

TANZANIASPORTS katika tathmini yake ya mchezo huo inaonesha dhahiri ni uzoefu ndio umewabeba Simba pamoja na faida ya kulazimisha sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Ndola nchini Zambia. 

Simba waliuanza mchezo vibaya, kabla kupindua meza katika kipindi cha Pili. Faida ya mabao mawili kibindoni iliwafanya Simba wasiamini presha toka kwa wapinzani wao, ambao walikuwa wakiwinda ushindi kwa udi na ufumba. 

Power Dynamos haikuwa timu tishio, lakini makosa ya Simba wenyewe yaliruhusu wageni wajione wana uwezo wa juu. 

MARA SITA AFRIKA

Kwa mara ya 6 Simba wametinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla ya 4-3. Kutinga hatua hiyo imedhihirisha kuwa licha ya kuhenyeshwa na wapinzani wao, bado Simba ni timu yenye kutuma ujumbe wakati wote kwa vigogo wa soka Afrika.

Msimu wa 2018/2019 Simba walitinga robo fainali, lakini wakafurumshwa hatua ya awali msimu uliofuata na UD Songo ya Msumbiji katika msimu uliofuata. Msimu wa  2020/21 walitinga Robo fainali, lakini msimu uliofuata 2021/2022 walitupwa nje ya mashindano na Jwaneng Galaxy ya Botswana. Katika msimu wa 2022/23 Simba walitinga tena robo fainali, na kudhihirisha wao wapo tayari kwa mapambano licha ya makosa kutokea.

KUSHINDWA KUMALIZA MECHI NDOLA

Licha ya kufuzu, Simba wanatakiwa kurudisha kumbukizi katika mchezo wa kwanza wa kule Ndola ambako walikosa mabao mengi, huku mshambuliaji wao Jean Baleke akikosa mabao mawili akiwa ndani ya eneo la hatari. Ilikuwa mechi ambao Simba walicheza mpira mkubwa kama walivyozoeleka lakini wakafeli kuamua matokeo hadi kuja kumalizia Dar Es Salaam. 

KIGUGUMIZI CHA VIUNGO NA WALINZI

Kulikuwa na viungo watatu, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin na kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza, ambao walikuwa na dakika 45 mbaya kazini. Safu ya ulinzi ikiongozwa na Che Marlone na Kennedy Juma pamoja na safu ya kiungo walifanya makosa na kusababisa wageni kupata bao la kwanza. Uchezaji wa viungo watatu ulikosa umakini na ubinifu katika awamu ya kwanza ha mchezo na kuwapa mwanya wageni watawale zaidi.  Mabadiliko ya kocha Robertinho ndiyo yaliwezesha kuipa uhai timu hiyo.

SIRI YA POWER DYNAMO

kucheza mara mbili na Simba kuliwapa nafasi ya kuijua vizuri timu hiyo. Simba waliwakaribisha  Power Dynamo katika Simba Day. Lakini siku chache baadaye wakatakiwa kucheza nayo kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tayari Power Dynamo walikuwa na faida hiyo, hivyo mchezo wa marudiano uliochezwa Dar Es Salaam ulikuwa wa tatu kwao. Siri hii ilikuwa inawabeba Power Dynamo huku wakiamini wangeitupa nje ya mashindano. 

ROBERTINHO AMEPITA NJIA YA VIPERS

Wakati Vipers ilipoitupa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika TP Mazembe, kikosi hicho kiliweka rehani nafasi yao kutokana na upangaji wa kocha huyu. Ingawa Vipers walishinda, lakini timu ilibadilika baadaye sana kutokana na Mwalimu kufanya mabadiliko. TANZANIASPORTS katika tathmini yake ya ufundi wa Robertinho inaonesha kuwa ni kocha anayepangua pangua kikosi cha ushindi na kuifanya timu ishindwe kucheza kwa ufanisi  na mtiririko hali ambayo inawia vigumu kutengeneza kombinesheni. Kikosi cha Simba ya Robertinho hakionekani kuwa na kombinesheni ya kueleweka kuanzia safu ya ulinzi, viungo na washambuliaji wake. Kupanga na kupangua kunawafanya wachezaji wacheze bila uelewano na kuathiri ufanisi wao. 

BENCHI LA SIMBA 

Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa benchi la Simba si imara kwa kuzingatia vigezo vya uwiano wa viwango kwa wachezaji mmoja mmoja. Wachezaji wanaowekwa benchi hawana uwiano sawa na wanaoanza kikosi cha kwanza. Hii Ina maana Simba wanatakiwa kuimarisha viwango vya wachezaji wao wabadala. Haiwezekani kuwa na mchezaji mbadala wa Mohammed Hussein au Shomari Kapombe halafu hawapati hata mechi za kuwajengea utimamu wa kimchezo. Hii ni changamoto kwa wachezaji wanaokaa benchi pamoja na benchi la ufundi kuangalia namna ya kuinua viwango vya wachezaji wao.

IMANI YA MASHABIKI 

Pengine mashabiki wa Simba wamezoea mashindano haya. Wamezoea kuwaona nyota wao wakichuana na wengine wa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata hivyo licha ya kuzoea ni wazi suala la Imani ya mashabiki kwa wachezaji wao huenda ikaanza kushuka kutokana na viwango,uamuzi wa bencjia ufundi, kupungua makali ya nyota wao, ni miongoni mwa mambo yanayoibua mjadala ikiwa wana Imani au la.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Skudu wa burudani, Yanga ni watoa dozi Afrika

Tanzania Sports

Wasichoelewa usajili wa golikipa mpya Arsenal