Wiki inaelekea kuisha, wiki ambayo ilikuwa na habari kubwa sana katika klabu ya Yanga. Habari ambayo kwangu mimi naiona kama funzo kubwa sana kwa kocha msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa.
Charles Boniface Mkwasa ameingia katika hali ya kutoelewana kati yake na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Congo, David Molinga baada ya Charles Boniface Mkwasa kumtoa kwenye timu mshambuliaji huyo.
Inawezekana Charles Boniface Mkwasa akawa sahihi sana na inawezekana pia asiwe sahihi, na hii inategemeana sana na namna ambavyo mtu anavyolitazama na kulitafakari hili suala la Charles Boniface Mkwasa na David Molinga.
Upi usahihi wa Charles Boniface Mkwasa? Kama kocha ambaye alikuwa na jukumu la kusimamia mazoezi kipindi hiki ambacho Luc Eymael hakuwepo ndani ya nchi , basi alikuwa na jukumu la kuhakikisha hali ya mazoezi inaenda vyema.
Mazoezi yalienda vyema? Bila shaka yalienda vyema? Mazoezi yaliandaliwa kwa kushirikiana na kocha mkuu Luc Eymael? Tuwe natumaini kuwa wote wawili walishirikiana kwa ukaribu kuandaa mazoezi kipindi ambacho timu inarudi mazoezini baada ya likizo ya Corona.
Tukiwa ndani ya tumaini lile lile la kwamba makocha wote wawili (Luc Eymael na Charles Boniface Mkwasa ) walishiriki kuandaa mazoezi ya timu, tujiulize swali moja kama makocha wote wawili walishirikiana kuandaa mazoezi lazima kuna vigezo ambavyo waliviweka kwa kila mchezaji awe navyo.
Timu ilikuwa kwenye likizo ya Corona. sehemu nyingi duniani zilikuwa ndani , wachezaji wengi hawakuwa na nafasi ya wao kufanya mazoezi kwa sababu ya kuwa ndani ya nyumba tu, lazima kuna vitu kadhaa vibadilike kwenye miili ya wachezaji.
Uwezekano mkubwa wa wachezaji kutokuwa na “fitness” ulikuwepo kwa sababu wachezaji walikuwa hawana nafasi ya kufanya mazoezi, kurudisha “fitness” ya mchezaji kunahitajika moyo wa mchezaji mwenyewe.
Kuna uwezekano mkubwa sana kwa wachezaji kuongezeka uzito kwa sababu ya wao kukaa ndani muda mrefu kipindi cha Corona. Lazima kungekuwepo na mazoezi maalumu ambayo yangeandaliwa na benchi la ufundi ili kuwarudisha wachezaji katika hali yao ya kawaida.
Bado nina matumaini makubwa sana kwa Luc Eymael na Charles Boniface Mkwasa kuwa walikaa wote wakajadiliana hili ndiyo maana Charles Boniface Mkwasa alimtoa David Molinga kuwekeza muda wake kwenye mambo mawili, moja kutafuta “fitness”, mbili kupunguza uzito wake , kitu ambacho kilikuwa sahihi kabisa kwa Charles Boniface Mkwasa kama kocha.
Yanga walianza mazoezi wiki iliyopita, walikuwa na muda mfupi wa mazoezi kabla ya mechi yao dhidi ya Mwadui inayochezwa mwishoni kwa juma hili , kwa muda huu mfupi Charles Boniface Mkwasa alihitaji wachezaji ambao wana “fitness” nzuri kwa ajili ya kupata matokeo chanya.
Kumwacha Dar es Salaam, David Molinga kwa sababu ya kutokuwa na “fitness” nzuri na kwenda na wachezaji wengine Shinyanga ambao yeye aliona angalau wana “fitness” nzuri lilikuwa jambo sahihi kabisa kwa Charles Boniface Mkwasa, na hii ndiyo mwisho wa usahihi wa Charles Boniface Mkwasa kwenye jambo hili.
Kutokuwa sahihi kwa Charles Boniface Mkwasa kwenye hili jambo unaanzia pale ambapo kama Charles Boniface Mkwasa alimwacha David Molinga kwenye kikosi cha Yanga bila kumpa taarifa kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael. Na hili jambo limeonekana wazi.
Hutokuwa umekosea kama ukiwaza kuwa Charles Boniface Mkwasa hamkushirikisha Luc Eymael kwenye suala la kumuacha David Molinga kwa sababu baada ya kumtangaza kumtoa kwenye kikosi cha Yanga, Luc Eymael alimrudisha na leo kasafiri naye mpaka Shinyanga.
Hii ndiyo sehemu ya Charles Boniface Mkwasa kutokuwa sahihi kwa kiasi kikubwa kwenye hili suala. Hili suala lazima kiutu uzima liwe na funzo kwenye pande mbalimbali, kuanzia kwa Charles Boniface Mkwasa na klabu ya Yanga.
Charles Boniface Mkwasa aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Hans Van de Pluijm mwaka 2015 kwenye timu ya Yanga. Miaka mitano imepita , nilitegemea muda huu Charles Boniface Mkwasa angekuwa anawaza kuwa kocha mkuu wa Yanga au timu yoyote ya ligi kuu.
Charles Boniface Mkwasa kuwa chini ya mtu ambaye wanalingana elimu ya kimpira ni kutokutendea haki vyeti vya ukocha vya Charles Boniface Mkwasa. Ninatamani kwa kiasi kikubwa yeye afikirie kuwepo sehemu ambayo atakuwa kocha mkuu.
Yanga wana chakujifunza hapa pia. Wanatakiwa kufikiria kuwa na Luc Eymael au Charles Boniface Mkwasa kwa sababu ni ngumu kwa mafahari wawili kukaa kwenye zizi moja na wakaelewana kwa kiasi kikubwa.
Comments
Loading…