KLABU ya Simba leo jumapili inaingia dimbani kupepetana na wageni wao Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho la Afrika. Katika mchezo huo wa mashindano ya CAF mwaka huu unafanyika kwenye uwanja wa Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar. Simba wana kila sababu ya kuibuka na ushindi huku wakiwa na mwendelezo mzuri kwenye mashindani ya CAF miaka 10 mfululizo.
Ugeni wa Stellenbosch Fc
Klabu hii kutoka Afrika Kusini ni ngeni machoni pa mashibiki na haifahamiki vya kutosha. Klabu hii imetinga hatua hiyo si kwa bahati mbaya bali uwezo wao kwenye mashindano ya CAF. Hata hivyo wanakutana na Simba isiyoshindika ambayo kucheza dimba la nyumbani alzima mgeni agaragawe. Katika mchezo huo Stellenbosch wataingia dimbani wakiwa wageni mara mbili. Ni wageni kwenye mashindano ya CAF na wageni kwenye mechi dhidi ya Simba. Hata kama benchi la ufundi limetazama mechi nyingi za Simba lakini ukweli ni kwamba kikosi hicho kinaingia kikiwa na hatua moja mble.
Fadlu Davids anawajua
Stellenbosch wanaingia kwenye nusu fainali kupambana na kijana mzaliwa wa Afrika kusini ambaye anaijua vema timu hiyo, kiufundi, maarifa na uwezo wao wa ziada. Simba hawahitaji kazi kubwa kuisoma Stellenbosch kwa sababu kocha wao Fadlu Davids anafahamu namna ya kukabiliana na timu za Afrika Kusini. Hii faida ambayo Simba wanayo kwenye mchezo huu na kwamba wanapaswa kuitumia vema kusaka ushindi wao.
Uozefu mkubwa wa Simba
Katika mashindano ya CAF, Simba wana uzoefu mkubwa mno kuliko wapinzani wao. Stellenbosch wanaingia anga za Simba wakiwa na uzoefu mdogo zaidi. Simba walianza kunguruma miaka 1970, kabla ya kupotea na kuibuka mwanzoni mwa miaka 2000. Kwa kipindi cha miaka 10 Simba wanashiriki mashindano hayo na kuwa miongoni mwa vilabu vyenye uzoefu mkubwa na vinavyovutia wachezaji na makocha wengi wa kigeni. Simba wamecheza kwenye viwanja vingi barani Afrika, kuanzia Tunisia, Algeria, Morocco, Misri, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Zimbabwe, DRC, Nigeria, Ghana na kwingineko. Ni klabu ambayo ina mengi ya kujivunia mbele ya Stellenbosch. Bila shaka yoyote Stellenbosch wanatambua kuwa mchezo wao wa kwanza wa nusu fainali unahusiana na timu kubwa ya Afrika katika mashindano.
Mabao na penati
Simba wanaweza kuifunga timu yoyote katika dakika 90 na katika hatua ya matuta. Wametinga nusu fainali baada ya kuitupa nje Al Masry ya Misri kwa matuta 4-1. Kwenye mchezo huo Simba walipachika mabao 2 ya kusawazisha ili kuwa 2-2 baada ya kuchapwa mchezo wa kwanza kwa 2-0. Katika mchezo wa marudiano walisawazisha na kuwafika hatua ya matuta. Katika upigaji wa matuta Simba hawakuonesha hofu wala kuigopa Al Masry badala yake wakaitungua vyema. Katika msingi huo Simba wanaweza kuifunga Stellenbosch katika hatua yoyote endapo wataamka vizuri kazini na kuonesha thamani yao kwenye dimba la Amaan Complex.
Uongozi imara
Kama kuna siri ambayo Simba wanayo kwa sasa ni namna viongozi wanavyoendesha mambo yao katika misingi imara. Simba ipo kwenye mikono ya viongozi ambao wameonesha thamani ya timu ni mafanikio ndani ya uwanja na hivyo timu yao imefika hatua ya nusu fainali. Uongozi huu wa chini ya Mwekezaji Mohammed Dewji umepiga hatua na kuifanya Simba kuwa timu inayoogopeka katika mashindano ya CAF.
Mashabiki wasiochoka
Kama kuna kitu kinatoa mchango kwa Simba ni mashabiki ambao wamekuwa wakijazana kwneye viwnaja mbalimbali kuisapoti timu yao. kwenye mchezo huu dhidi ya Stellenbosch visiwani Zanzibar mashabiki wanatarajiwa kujaza uwanja huo na kuinga mkono Simba kwenye kampeni ya mashindano ya CAF. Mashabiki wamekuwa bega kwa bega, na ndiyo sababu ya kupewa tuzo wakati wa mashindano ya Africa Football League kutokana na amsha amsha waliyoonesha kwenye mechi mbili, ufunguzi jijini Dar Es Salaam na Cairo. Kama CAF waliwatambua mashabiki wa Simba na kuwapa tuzo, kipi kingine kitawarudisha nyuma kushangilia timu yao. ni wakati wao wa kuimba nyimbo zote za Simba akinguruma……..
Bingwa mtarajiwa
Simba wana kila sababu ya kutwaa taji hili. Ni taji muhimu katika historia yake kwani linatengeneza rekodi ya Afrika na kutangaza jina lao na Ligi Kuu Tanzania. Katika mashindano ya CAF ni jukwaa la kuonesha vipaji, kufanya biashara na kukuza uwezo wa timu. Kwahiyo kutwaa kombe hili ni matokeo ya uwezo, uzeofu na umakini wa becnhi la ufundi na viongozi ili kuimarisha nembo ya klabu. Simba tangu mwanzoni wa mashindano haya, wana kila sababu ya kuchukua kombe hili.
Washindani wake wengi si tishio wala hawana uzoefu mkubwa kuwazidi Simba. Lakini kwenye michuano kama hii licha ya kuhitaji bahati Simba wanacho kikosi cha kuwapa ubingwa pamoja na makocha ambao wanajua kuabdilika kurekebisha makosa ya wachezaji wao pale yanapotokea. Katika mechi zote mbili dhidi ya Stellenbosch, Simba hawana sababu nyingine ya kushindwa kuvuka na kutinga fainali. Ni suala ambalo lipo mikononi mwao kutokana na aina ya timu zinazoshiriki kwenye hatua hii katika mashindano hayo.
Comments
Loading…