Haijalishi jinsi wazo la kuendelea kulazimisha michezo hiyo ifanyike majira ya joto Ulaya linavyoonekana la kipuuzi
Huenda mitazamo isiwe ya kibaguzi kama ilivyokuwa zamani, lakini bado ni kweli kwamba, angalau England, Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) hujadiliwa kidogo kama mashindano yenye hadhi yake kuliko jinsi yanavyoathiri Ligi Kuu ya England.
Kawaida kutakuwepo na malalamiko kuhusu kwa nini mashindano hayo hufanyika katikati ya msimu wa Ulaya, lakini Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limekuwa likijaribu kutii matakwa ya vilabu vya Ulaya—hata hivyo likajikuta linafungwa mikono na Fifa pamoja na ratiba yake inayozidi kuwa ngumu.
Ni lazima kukiri, upangaji ratiba si nguvu ya CAF. Hakujawahi kuwa na AFCON iliyofanyika mahali na wakati ulioamuliwa awali tangu 2012:
- 2013 ilihamishwa kutoka Libya kwenda Afrika Kusini kwa sababu ya vita;
- 2015 ikaenda Equatorial Guinea baada ya Morocco kujiondoa kwa hofu ya Ebola;
- 2017 ikaenda Gabon kutokana na vurugu nchini Libya;
- 2019 ikaondolewa Cameroon kwenda Misri kwa sababu ya kuchelewa kwa ujenzi;
- 2021 ilifanyika Cameroon lakini hadi 2022 kwa sababu ya Covid;
- 2023 awali ilipangwa Côte d’Ivoire mwezi Juni/Julai, lakini ikarudishwa Januari/Februari baada ya CAF kutambua kuchelewa kwamba kucheza mashindano wakati wa msimu wa mvua Afrika Magharibi ni jambo lisiloingia akilini.
Haijalishi jinsi wazo la kuendelea kulazimisha michezo hiyo ifanyike majira ya joto Ulaya linavyoonekana la kipuuzi—je, mpango ni kutokufanya tena mashindano Afrika Magharibi?—hilo bado ndilo sera rasmi.
AFCON 2025 ilipangwa kufanyika Morocco Juni/Julai. Lakini Gianni Infantino alipoanzisha Kombe la Dunia la Vilabu lililopanuliwa, Afrika ikalazimika kuyasukuma mashindano yake hadi kuanza 21 Desemba.
Kwa mtu aliyesema kabla ya Kombe la Dunia kwamba “anajihisi Mwafrika”, Infantino ana njia ya ajabu ya kuonyesha hilo. Rais wa Fifa bado anapiga nyimbo zile zile za kupinga ukoloni kwa ajili ya kupata uungwaji mkono barani Afrika, lakini anaonekana kutokujali nafasi finyu ya mashindano hayo kama alivyopuuza vifo vya maelfu ya wafanyakazi wahamiaji nchini Qatar.
Pendekezo lake la ligi kubwa ya Afrika ya timu 20 yenye thamani ya dola milioni 100—wazo tatanishi ambalo lingekanyaga ushindani wa jadi na mashindano yaliyopo—mwishowe likawa tu mashindano ya timu nane mwaka 2023 (hayajawahi kutangazwa rasmi kama yamefutwa, lakini hayatajwi tena kwenye tovuti ya CAF).
Kwa kawaida, Fifa inahitaji wachezaji kuachiliwa na klabu siku 14 kabla ya mashindano, lakini kwa AFCON hii imeshushwa hadi siku sita, huku klabu zikihimizwa kutafuta “makubaliano binafsi” kama hazitaridhika. Dhihaka dhidi ya Afrika iko wazi.
Patrice Motsepe, rais wa CAF na mshirika muhimu wa Infantino, alihudhuria droo ya Kombe la Dunia Ijumaa licha ya majaribio ya Donald Trump kumzuia rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kuhudhuria mkutano wa G20 mwakani. Trump, aliyeshiriki kikamilifu kwenye droo hiyo, alisusia mkutano wa viongozi wa G20 Johannesburg mwezi Novemba akidai kuwa wazungu wachache Afrika Kusini “wanateswa”.
Kwenye mipango ya Juni/Julai kufungwa kwa Afrika, ilipendekezwa mashindano yarudi Januari/Februari. Lakini hapo pia kuna changamoto zake.
Kuanzia 1996 hadi 2012, AFCON ilichezwa Januari/Februari katika miaka ya shufwa((mfano: 2, 4, 6, 8.) Kwanini kila baada ya miaka miwili? Kwa sababu mwaka 1957 mashindano yalipoanza, Afrika ilikuwa miaka 13 kutoka kupata nafasi ya kudumu Kombe la Dunia, hivyo ilikuwa njia pekee ya kupata mashindano ya ushindani.
Kwa kuwa ni timu tano tu ndizo zilikuwa zinakwenda Kombe la Dunia hadi hivi karibuni, AFCON ilikuwa kwenye mchakato yakinifu kusaka mapato kwa nchi nyingine zaidi ya 50 wanachama wa CAF. Kama Ulaya inapingana na hilo, wakati wachezaji wengi wa Kiafrika wanacheza huko, basi inapaswa kutafuta njia mbadala za kufadhili soka la Afrika.
Kulikuwa na hisia kwamba katika miaka ya Kombe la Dunia, AFCON inafunikwa. Kwa kuongezea, kanuni za Fifa zinavitaka vilabu kuwaachia wachezaji kwa shindano moja tu kwa mwaka. Katika mwaka wa Kombe la Dunia, vilabu vya Ulaya vingekuwa na hoja ya kukataa kuwaachia wachezaji waende AFCON, hasa ubadilishaji wa Ligi ya Mabingwa ulivyozagaa hadi Januari.
Suluhu iliyopatikana ni haya mashindano ya Desemba/Januari, ambayo yanaweza kutajwa kama mashindano ya mwaka 2025 ili vilabu visitumie udhuru wa kukataa kuwaachia wachezaji, huku ikioana na mapumziko ya msimu wa baridi kwa ligi nyingi za Ulaya. Ndiyo maana, ukiwa na mechi moja tu ya Premier League, unaweza kujaza Boxing Day yako kwa kutazama:
Zambia v Comoros, Misri v Afrika Kusini, Morocco v Mali na Angola v Zimbabwe.
Athari kwa vilabu vya Premier League
Vilabu vitaathirika, ingawa Arsenal na Chelsea hawatakuwa na mchezaji yeyote AFCON.
- Sunderland inaweza kukosa hadi wachezaji saba, muhimu zaidi wakiwa Noah Sadiki (DRC) na Reinildo (Msumbiji), huku beki wa kushoto anayemsaidia, Arthur Masuaku, pia yuko DRC. Kurudi kwa Dennis Cirkin kumejiri kwa wakati mwafaka.
- Liverpool kumkosa Mohamed Salah si pigo kama zamani, na Omar Marmoush wa Misri ameanza mechi mbili tu kwa Man City msimu huu.
- Manchester United watapungukiwa mashambulizi kwani Amad Diallo na Bryan Mbeumo watajiunga na Côte d’Ivoire na Cameroon.
- West Ham watamkosa Aaron Wan-Bissaka (DRC) na El Hadji Malick Diouf (Senegal).
- Everton na Crystal Palace watakosa ubunifu wa Iliman Ndiaye na Ismaïla Sarr (Senegal), huku Fulham wakimkosa Alex Iwobi (Nigeria).
- Kutokufuzu kwa Ghana na Gambia kunamaanisha Mohammed Kudus, Antoine Semenyo na Yankuba Minteh wataendelea kupatikana kwa Tottenham, Bournemouth na Brighton mtawalia.
Lakini hii siyo hadithi ya Premier League.
Hii ni hadithi ya soka la Afrika, na jinsi—licha ya maneno mazito ya Infantino—limebanishwa kapuni; jinsi, kadiri ulafi unavyopanua ratiba ya soka duniani, Afrika imejikuta ikitafuta kona finyu ya kujibana kwa aibu ili kuendesha mashindano yake makuu zaidi.


Comments
Loading…