in

‘African Super League’ ni pasua kichwa CAF

Gianni Infantino

Rais wa FIFA Giani Infantino amepata mtu aliyekuwa anamhitaji katika nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka barani Afrika ili kutekeleza mipango yake aliyopanga kwaajili ya maendeleo ya kandanda barani humu. Mtu huyo ni Dk.Patrice Motsepe ambaye anatajwa kuwa na mtazamo sawa na Infantino. 

Tanzaniasports inafahamu ajenda 10 za rais mpya wa CAF, miongoni mwake ni kuanzisha mashindano mapya yenye jina la African Super League. Ajenda zingine ni suala la utawala bora,kubuni vyanzo vya mapato,kuboresha miundombinu ya soka Afrika na mengineyo.

Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa kwa hamu ni mkakati wa kuanzisha ‘African Super League’. Inaelezwa kuwa African Super League’ inatarajiwa kushirikisha klabu 20 za Afrika. Huo ni mkakati alionao rais mpya wa CAF, Motsepe ambapo mchongo wenyewe alipewa na rais wa FIFA, Giani  Infantino.

Mpango huo ulianza kuzungumziwa mwaka 2020 katika kikao kilichofanyika nchini DR Congo. Katika mkutano huo Giani Infantino alipendekeza kuanzishwa African Super League ili kukuza mchezo wa soka.

Giani anaamini kuwa kuanzisha African Super League kutatengeneza kiasa cha dola milioni 200 kwa bara la Afrika. Anaamini timu zinazopaswa kushiriki lazima ziwe 20 na kuifanya kuwa Ligi kubwa duniani.

Lengo lingine ni kuhakikisha African Super League inazalisha vipaji vikubwa kama George Weah, Samuel Eto’o, Mohammed Salah, Didier Drogba,Rigobert Song,Lucas Radebe na wengineo.

Msingi wa Giani kuanzisha ligi hiyo unatokana na mafaniko hafifu yaliyopo katika timu za bara la Afrika. Pia anaona Ligi za Afrika ziko nyuma kimafanikio na maendeleo mara 10 nyuma ya timu za Ulaya. Hivyo kuwa chanzo cha timu na ligi kuwa dhaifu.

Inaaminika kuwa African Super League itakuwa chachu ya ongezeko la uwekezaji na mapato. Kwamba timu zitakazoshiriki na shirikisho la soka CAF watanufaika na mashindano hayo hivyo kuwa chachu ya kuboresha kandanda la Afrika.

Mpango huo unalinganishwa na ule wa Bodi ya mchezo wa Kikapu na Chama cha mchezo wa Kikapu nchini Marekani NBA kuanzisha Ligi ya Kikapu barani Afrika maarufu kama Baskeball Africa League ikiwa ni mpango wa kushirikisha timu 12 kutoka kaskazini hadi kusini mwa Afrika. Mpango wa kuanzisha BAL (Basketball Africa League) ulitakiwa mwaka 2020 lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa corona umesababisha kusitishwa kwa muda.

Aidha, mpango wa kuanzisha Ligi ya Afrika inatarajiwa kuondoa vikwazo vya maendeleo kwa vilabu,timu za taifa,vipaji vya soka na uongozi pamoja na kuongeza tija ya mkundombinu. 

NI TIMU ZIPI ZITACHEZA?

Tanzania Sports
CAF

Hili ni swali ambalo rais wa FIFA Giani Infantino na Patrice Motsepe wa CAF wanatakiwa kuleta majibu. Kila nikitazama mpango huo naona utazinufaisha timu za upane mmoja. Ni namna gani Giani na Motsepe wataweka uwiano na vigezo vya timu zitakazotakiwa kushiriki African Super League. 

Hadi sasa zipo tofauti kubwa za ushiriki wa timu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Timu zinazotoka upandewa kaskazini mwa Afrika zinatamba kwenye mashindano mengi ya CAF kuliko upande wa Afrika magharibi,Afrika mashariki,Afrika ya kati,Afrika mashariki na hata zile za kusini mwa Afrika.

Tuchukue mfano kwenye mashindano ya CAF msimu uliopita. Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilihusisha timu kutoka Misri,Morocco na Tunisia. Mchezo wa fainali ulizikutanisha timu za jiji moja la Cairo yaani Al Ahly na Zamalek. 

Zamalek wamefanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano. Al Ahly imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tisa. Ni timu za Afrika kusini pekee ndizo zinaweza kuwachachafya timu za kiarabu.

Tunapozungumzia timu za kiarabu ina maana ya Al Ahly (Misri),Zamalek (Misri), Pyramids(Misri),Raja Casablanca (Morocco),Wydad Casablanca (Morocco),Etoile Du Sahel(Tunisia),Esperance (Tunisia), Club Africain (Tunisia).

Kwa upande wa Afrika kusini kuna timu za Orlando Pirates, Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns, pamoja na timu zingine DR Congo kama vile TP Mazembe, AS Vita na DC Motema Pembe.

Ukiondoa timu hizo kwa upande wa kusini mwa jangwa la Sahara hakuna timu zenye kufurukuta au kutwa tishio katika soka Afrika. Kwahiyo changamoto inakuja ni timu gani itaweza kuingia kwenye kapu la timu 20 na kushiriki mashindano ya African Super League?

MGAWANYO UTAKUWAJE?

Baada ya kuangalia suala la vilabu sasa tugeukie suala la mgawanyo wa nafasi za timu kushiirki kutokana na nchi wanachama wa CAF. Bara la Afrika lina jumla ya nchi 56, ambazo ndizo wanachama wa shirikisho la soka CAF. 

Hii ina maana ukitazama timu zinazofanya vizuri utaona zinatoka katika mataifa ya Morocco,Tunisia,Misri,Afrika kusini na DR Congo, pamoja na baadhi ya mataifa ya Nigeria,Ghana na Ivory Coast. 

Katika muktadha huu naona ugumu utakavyokuwa kwenye suala la kuchagua vilabu vya nchi wanachama wa CAF.

GHARAMA ZITAPUNGUA?

Gharama za Ligi ya Mabingwa Afrika zimesababisha kuonekana mashindano hayo kutokuwa na faida kwa timu. Gharama za usafiri wa ndege ni eneo ambalo linasumbua timu nyingi za Afrika. Hivi karibuni imeshuhudiwa timu ya taifa ya Gabon ikilala uwanja wa ndege kwa sababu ya gharama.

Wakati Giani na Motsepe wakiwa wanapanga kuongeza mapato kwa timu bado hali ya mashabiki na timu gharama ni kubwa. Suala la usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine limekuwa tatizo kubwa linaloambatana na gharama.

Hata kama wataendesha mashindano hayo kwenye nchimoja maana yake kutakuwa na gharama za uendeshaji pia.

NAFASI YA LIGI YA MABINGWA

Mvuto unaotengenezwa kwenye Ligi ya Mabingwa ukiletewa mashindano ya African Super League bila shaka kutakuwa na hasara kwa upande mmoja. Ligi ya Mabingwa inaweza kuathirika kutokana na kupoteza mvuto kwa watazamaji na wawekezaji. Pamoja na nia nzuri ya kuboresha soka barani Afrika ni wazi nafasi ya Ligi ya Mabingwa inatishiwa na mashindano mapya ikiwa yataanza. Na hilo litakwenda sambamba na ushindani kutoka ligi zingine za nje  hasa lina;ofika suala la muda wa mchezo. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Patrice Motsepe

Fahamu mambo muhimu kuhusu Rais wa CAF

Yanga v SIMBA

Lini TFF wataleta utamu wa takwimu VPL?