in

Fahamu mambo muhimu kuhusu Rais wa CAF

Patrice Motsepe

Wapinzani wa Motsepe walikuwa Jacques Anouma raia wa Ivory Coast, Ahmed Yahya (Mauritania) na Augustine Senghor (Senegal).

SHIRIKISHO  la Soka barani Afrika (CAF) limepata kiongozi mpya kufuatia uchaguzi wake uliofanyika mjini Rabat nchini Morocco. Rais mpya wa CAF ni Dk. Patrice Motsepe raia wa Afrika kusini, ambaye anachukua madaraka kutoka kwa Ahmad Ahmad raia wa Madagascar. Katika makala haya utafahamu mambo muhimu kuhusu kiongozi huyo mpya wa soka Afrika.

NI BILIONEA WA TISA

Motsepe anafahamika kuwa mfanyabiashara mkubwa barani Afrika akiwa mmoja wa matajiri wanaotajwa mara kwa mara. Motsepe anashika nambari 9 kati ya mabilionea walioko Afrika. Kwa mujibu wa jarida la kiuchumi la Forbes limesema Motsepe anamiliki kampuni inayojishughulisha na biashara ya madini ya African Rainbow Minerals aliyoanzisha mwaka 1994. Motsepe alizaliwa Januari 28, mwaka 1962. 

Mafanikio yake kibiashara yanayotoka na sera ya kuwezesha watu weusi nchini Afrika kusini ambayo ilianzishwa na utawala wa rais Nelson Mandela maarufu kama ‘Black Empowerment’. Utajiri wake unatajwa kuwa ni dola bilioni 3.

KUTWAA LIGI YA MABINGWA

Motsepe ni mmiliki klabu ya Mamelodi Sundowns. Mwaka 2016 klabu hiyo ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Afrika na ikawa klabu ya pili ya Afrika kusini kunyakua kombe hilo lenye hadhi kubwa barani Afrika.

‘RAFIKI WA FIFA’

Tanzaniasports inafahamu kuwa Motsepe ni rafiki mkubwa wa rais wa Shirikisho la soka Duniani FIFA, Giani Infantino. Taarifa zinasema rais wa CAF aliyepita, Ahmad Ahmad hakupikika chungu kimoja na rais wa FIFA. 

Kwa sasa Infantino inaonekana kama amepata mtu wake aliyemhitaji kwa sababu amewahi kuwashauri wagombea wengine kwenye nafais kuangalia uwezekano wa kumwachia Motsepe kuwania urais wa CAF.

Taarifa zinaeleza zaidi kuwa FIFA wamekuwa na mkono wao kuhakikisha Motespe anachaguliwa kuwa rais wa CAF.

‘AFRICAN SUPER LEAGUE’

Miongoni mwa mambo yanasubiriwa kwa hamu ni mkakati wa kuanzisha ‘African Super League’. Inaelezwa kuwa African Super League’ inatarajiwa kushirikisha klabu 20 za Afrika. Huo ni mkakati alionao rais mpya wa CAF, Motsepe ambapo mchongo wenyewe alipewa na rais wa FIFA, Gian Infantino.

USHINDI BILA MPINZANI

Katika hatua nyingine Patrice Motsepe amefanikiwa kukwaa madaraka ya CAF akiwa hana mpinzani. Motsepe amechukua madaraka hayo baada ya wapinzani wake kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho. 

Motsepe amechukua madaraka hayo baada rais wa zamani wa CAF, Ahmad Ahmad kuwa wa kwanza kupigwa marufu kujihusisha na soka, pamoja na kufungiwa kwa miaka mitano kuanzia Novemba mwaka 2020. 

Hata hivyo Ahmad alikata rufaa katika Mahakama ya michezo, lakini adhabu yake ilipunguzwa kutoka miaka mitano hadi miwili. Licha ya kupunguzwa adhabu hiyo bado haikumwezesha kutetea kiti chake. 

Wapinzani wa Motsepe walikuwa Jacques Anouma raia wa Ivory Coast, Ahmed Yahya (Mauritania) na Augustine Senghor (Senegal). Senghor na Yahya wamepewa nafasi ya kuwa makamu wa rais wa CAF. Anouma ameteuliwa kuwa mshauri maalumu wa rais wa CAF.

WAKILI MAARUFU

Mbali ya biashara, Motsepe ni mwanasheria kitaaluma. Yeye ni mtu wa kwanza kuongoza kampuni maarufu ya Bowman Gilfillan. Licha ya kuedesha kampuni ya uchimbaji wa madini ya chuma na dhahabu, anajishughulisha na masuala ya kisheria kupitia kampuni ya uwakili.

ASISITIZA UMOJA NI NGUVU

Baada ya kuchaguliwa kwake Motsepe anasisitiza umoja miongoni mwa viongozi wa kandanda barani Afrika. Akizungumza baada ya kuchaguliwa Motsepe alisema, “Afrika inahitaji busara ya pamoja, lakini inahitaji watu wenye busara zaidi na vipaji vya kuinua soka la bara la Afrika. Sote tukifanya kazi pamoja, soka la Afrika litatoa uzoefu wake duniani na kupaa mafanikio na kuendelea zaidi pamoja na kuburudisha wadau na wapenzi wa kandanda,”.

NGUVU YA KUSINI

Kimsingi sasa baada ya uchaguzi wengi wanangojea matunda ya uongozi mpya wa Motsepe. Kiongozi huyo anatoka Afrika kusini ambalo ni taifa jirani la Madagascar alikotoka rais Ahmad Ahmad. Kuchaguliwa kwa jirani wa Ahmad maana yake ukanda wa Kusini mwa Afrika kumeonesha nguvu na kuwa na watu wenye nguvu katika kandanda. Ni wakati wa kuona matunda ya nguvu hizo zikitumika kuleta mafanikio kwa bara la Afrika. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
AMRI BAWJI

NDOTO YA AMRI BAWJI IPO SIKU ITATIMIA

Gianni Infantino

‘African Super League’ ni pasua kichwa CAF