Ukifuatilia mijadala kuhusu wadhamini wa vilabu mbalimbali nchini Tanzania unaweza kudhani kuna maelfu ya mabilionea wameteka udhamini wa vilabu vya soka. Mjadala huo umejikita kuilaumu kampuni moja inayodhamini vilabu vingi vya Ligi Kuu.
Wanaolalamikia kampuni hiyo kudhamini kwa wingi vilabu vya Ligi Kuu hawana mbadala wowote na hawaweki sababu wala mbinu za kutafuta wadhamini wengine kwa ajili ya kuimarisha Ligi Kuu.
Bahati nzuri Rais wa shirikisho la Soka nchini TFF, Wallace Karia amewahi kubainisha kuwa Ligi Kuu bado ilikuwa na uhaba wa fedha na kuna kila sababu ya kuimarisha vitengo vya masoko ili kutafuta mapato zaidi. Kauli ya Rais Karia ilidhihirisha kilio cha muda mrefu cha uhaba wa wadhamini katika Ligi Kuu Tanzania.
Miaka kadhaa iliyopita vilabu vilikuwa na changamoto ya kulipa mishahara wachezaji na maofisa wake, kukosa bajeti ya safari, kukosa honoraria, kukosa fursa ya kupata wadhamini wakubwa, kukosa mapato ya uhakika na mengineyo mengi yalisababisha ufanisi hafifu wa vilabu husika. kwahiyo napotokea mdhamini mmoja kuwekeza fedha zake kwenye vilabu kadhaa huku kanuni ikiwa haimnyimi fursa hiyo linakuwa jambo la heri kwani inawezesha klabu husika kupata fedha za uendeshaji wkenye klabu zao.

Ligi Kuu Tanzania imekuwa na changamoto ya mapato kabla ya kuingia kwenye mabadiliko ya uongozi. Viongozi wengi waliokuwa wakijiingiza kwenye uongozi wa soka walikuwa na mawazo ya kuchota chochote kutoka kwenye klabu kuliko wao kuingia chochote kusaidia klabu hasa suala la uchumi. Mategemeo makubwa yalikuwa kutoka kwa watu binafsi ambao wanachangia timu hizo na kuziwezesha kucheza mechi mbalimbali.
Hata hivyo mabadiliko ya sekta ya michezo yamesaidia kupunguza “watu wa mpira” ambao hawakuwa wakiongeza tija zaidi ya kuwa sehemu ya migogoro. Ujio wa kampuni na mabenki kudhamini vilabu vya Ligi Kuu ingelifaa kuheshimiwa na kutambuliwa mchango wanaotoa kuliko kukandia na kuendeleza majungu ili kuwaondoa wadhamini hao ambao wanasaidia kukuza vipaji, kuongeza mapato ya nchi na kadhalika.
Katika msingi huo suala la mdhamini mmoja kudhamini timu nyingi linafaa kukumbushwa kwamba tunakotolea mifano wametuzidi mbali sana kwenye suala la uwekezaji kwenye michezo. Mfano soka, unapojaribu kulinganisha kati ya Tanzania na England fahamu kuwa wenzetu wamewekeza kuanzia ngazi ya watoto wadogo hadi wakubwa.
Chukua mfano wa Brazil, wao wanaamini mchezaji wa timu ya Taifa lazima apitie ngazi zote za taifa. Kwa mfano lazima acheze kwenye timu za Taifa za umri wake kuanzia chini ya miaka 15, 17, 19, 20, 23 hadi timu za wakubwa. Wao wanaamini huo ni uwekezaji ambao unakuza vipaji vya wachezaji na tayari katika klabu zao wapo kwenye usimamizi imara unaotokana na mapato mazuri wanayopata wamiliki wa vilabu kutoka kwa wadhamini na wadau wao.
Vilevile suala la vilabu kuwa na wadhamini zaidi ya mmoja ni kitu ambacho kiimewezesha kukuza mapato ya timu mbalimbali. Kwahiyo timu zinapokuwa na wadhamini wengi inasaidia kukuza Ligi Kuu pamoja na kuboresha mapato. Hata hivyo klabu hizo haziwezi kupata wadhamini wengi mahali ambapo hapaeleweki soko lake huko waendako.
Mdhamini anawekeza fedha zake akifahamu kuwa atapata nini kwenye uwekezaji huo na kwa kipindi gani. Si rahisi mdhamini kuweka fedha zake kwenye klabu ambayo inapigania kubaki Ligi Kuu kati ya timu 16. Kwani sababu inakuwa rahisi tu kwamba fursa ya kuwekeza kwenye timu hiyo inahusu mechi 32 tu ambazo hazichezwi kila siku. Kwa maana hiyo uchache wa mechi na mashindano ni sababu nyingine ya uchache wa wadhamini.
Tunapopata wadhamini wengi maana yake tunao uwingi wa mechi ambazo zitawafanya watazamaji kuendelea kuziona kampuni za wadhamini zikiongezeka.
Hivyo basi, mijadala hii kuhusu kampuni moja kudhamini timu nyingi ni vema ikazingatia hali halisi ya mazingira yetu ya kibiashara. Kwamba wadhamini mbadala watakuwa wa aina gani na wanawekeza kiasi gani kwenye timu za Ligi Kuu.
Ukiangalia sasa utaona kubwa timu tano ambazo unaweza kudhamini na mechi zake zinakuwa na ushindani, yaani zinavutia watazamaji ni Simba, Yanga, Azam, Singida Black Stars na Tabora United hizi ni za uhakika. Mategemeo mengi ni pale Simba na Yanga zinapokutana na timu nyingine ndipo mvuto wa ligi unaongezeka. Kinachosaidia Ligi yetu ni kuongezeka kwa wachezaji wa kigeni na ushiriki mzuri kwenye mashindano ya Kimataifa.
Ongezeko la wachezaji wa kigeni limeibua ushindani kwani wadhamini waliopo angalau wanaweza kutoa fedha zao kwa timu na kuimarisha vilabu mbalimbali. Hata hivyo, tunatakiwa kuwa na zaidi ya vilabu viwili au vitatu vya ushindani katika Ligi Kuu.
Ligi Kuu Afrika kusini kuna mechi zinavutia mno, Mamelodi Sundowns wakikutana na Orlando Pirates ni shughuli pevu, masha amsha ni kubwa. Hali kadhalika Kaizer Chiefs ikikutana na Supersports United, Stellenbosch au Cape Town City unatambua shughuli inakuwa ngumu kwa kila upande.
Kifupi wana mechi nyingi wanaoweza kuziita dabi, tofauti ya Ligi Kuu Tanzania tunayo Dabi tatu tu; Simba, Yanga na Azam. Nje ya hapo mechi nyingine zinakuwa za kawaida. Katika mazingira hayo ili kuimarisha na kupandisha uwezo wa timu ni pamoja na kuwa na wadhamini wenye nguvu na uhakika kuongeza ushindani kwenye ligi yetu. Pia wadhamini hao kutumia Ligi yetu kukuza nembo zao kupitia mchezo.
Comments
Loading…