MABADILIKO makubwa ya sekta ya michezo yanaelekea kushika hatamu barani Afrika kutokana na wawekezaji na wamiliki wa vilabu vya soka kukimbilia katika nchi mbalimbali barani Afrika kuwekeza katika sekta hiyo ama kutumia njia nyingine katika kukuza biashara zao pamoja na kutafuta faida. Miongoni mwa mataifa ambayo yanawindwa pakubwa na matajiri wa vilabu vya soka duniani ni Tanzania, Afrika kusini, Nigeria kwa kuzitaja chache.
TANZANIASPORTS katika uchunguzi wake imebaini kuwa wamiliki wa vilabu vya soka barani Ulaya wanachukua mkondo mpya wa kufungua milango ya kupata faida, kuuza nembo za timu zao, kufanya biashara na serikali na wadau wa soka, huku umoja wa Vilabu ukitajwa kuwa sehemu muhimu ya kukuza ushirikiano kati ya vilabu vikubwa na vidogo, vilabu vya nchi zilizoendelea na zile zinainukia kiuchumi na kimichezo.
Ligi Kuu Tanzania imetajwa kuwa kwenye nafasi 10 bora za ubora wa soka barani Afrika, huku shirikisho la soka CAF likiitaja klabu ya Simba kushika nambari 4 kwa ubora wa miaka 10 mfululizo. Sababu hizo zinachagiza wamiliki wa vilabu, wawekezaji na wadau wa michezo kutumia sababu hizo kama nyenzo ya kupanua uwekezaji wao kupitia michezo, huku mabilionea wa Afrika nao wakiwa hawajalala usingizi kwani timu zao zimekuwa kwenye mafanikio makubwa.
Wazawa katika michezo

Ujio wa Mohammed Dewji katika klabu ya Simba, kisha GSM katika klabu Yanga kwa upande wa Ligi Kuu, huku nchini Afrika kusini klabu ya Stellenbosch F.C inanufaika na utajiri wa mmiliki wake ambaye ni miongoni mwa mabilionea wa Kiafrika. Wapo wazawa wa kiafrika waliobaini fursa za kutangaza biashara zao kupitia sekta ya michezo. Ni sababu hii Yanga hivi wanavaa nembo ya “Visit Zanzibar”, ama Simba walivyovaa nembo ya “Visit Tanzania”.
TP Mazembe chini ya Moise Katumbi imekuwa ikifanya vema lakini sasa ushindani kutoka kwa mabilionea wengine umechangia kuyumba kwao. Hali hiyo imezeshwa kupitia ushirikiano walionao mabilionea hao kutafuta fursa kwa ajili ya kuwauzia mawazo ya uwekezaji matajiri wakubwa wa Ulaya, pamoja na vilabu vingine kuvutiwa na kasi ya ukuaji wa kandanda katika bara la Afrika.
Arsenal, PSG kwa ‘Visit Rwanda’
Miongoni mwa vilabu vinavyonufaishwa na soko la kiafrika ni pamoja na Arsenal ya England na PSG ya Ufaransa. Vilabu hivyo vimepata udhamini kutoka serikali ya Rwanda ambapo vinavaa jezi zenye nembo ya “Visit Rwanda” ikiwa ni sehemu ya kutangaza utalii na fursa za uwezekaji nchini Rwanda. Nembo ya “Visit Rwanda” imeonekana katika viwanja vingi baarani Ulaya, hasa timu hizo zinaposhiriki mashindano ya Ulaya ambapo yanatanua fursa ya kutangazika zaidi. Ajax ya Uholanzi pia ni miongoni mwa vilabu vilivyochunguilia fursa ya soko la michezo barani Afrika baada ya kuanzisha tawi lake kupitia klabu ya Ajax Cape Town ya Afrika kusini. Fursa hii inawasaidia Warwanda kutangaza vivutio vyao vya utalii kupitia viwanja vya Ligi Kuu ya Ufaransa na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pia Arsenal wanatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii kupitia Ligi Kuu England na Mashindano ya Ligi ya Mabingwa.
Manchester United na Tanzania
Mmiliki mwenza wa klabu ya Manchester United ya England, Sir Jim Ratcliffe hivi karibuni alitembelea Tanzania kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan. Ratcliffe ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya INEOS ambaye amekubali kutumia fursa za kutangaza utalii wa Tanzania. Bado hatujui msimu ujao Manchester United itakuwa nembo gani lakini ujio wa kiongozi huyo umebainishwa bayana kuwa ushirikiano wa kampuni ya INEOS, klabu ya Manchester United utakuwa kwenye sekta ya utalii.
Sekta ya Utalii ni miongoni mwa maeneo nyeti yanayokuza uchumi wa Tanzania. Kwa kutambua thamani ya soko na fursa hii isingekuwa rahisi kwa mmiliki wa INEOS kukwepa mwaliko. Kwa msingi huo Man United licha ya kuwatumia wanasoka wake waliocheza katika klabu mbalimbali kama mabalozi wao kwenye nchi zao, sasa inavuka hatua kuelekea kwenye uwekezaji wa fursa ya utalii ambapo itanufaishwa na wingi wa watu ambao ni mashabiki, pamoja na usajili wa wanachama wapya.
Uwingi wa Watu kivutio
Wataalamu wa biashara na uchumi wanatuambia kuwa bara la Afrika ndiko liliko soko kubwa la bidhaa bora kutokana na kasi ya ongezeko la watu pamoja na mahitaji ya huduma mbalimbali. Wawekezaji na wataalamu wa biashara wanaliangalia bara la Afrika kama fursa ya kupata faida za kibiashara pamoja na kutoa mchango wa maendeleo huku kigezo kikubwa kikiwa idadi kubwa ya watu.
Kwa mujibu wa Jarida la masuala ya uchumi, biashara na siasa la The Economist katika utafiti wake wa “The Economist; Megachange the World in 2050” wa mwaka 2012 wanaeleza, “Dunia inaelemewa na kasi ya ongezeko la watu katika historia ya Ulimwengu. Ilichukua miaka 250,000 kufika idadi ya watu bilioni 1, takribani karne moja iliyopita (mwaka 1927), Dunia ilifikisha idadi ya watu biliono 2 na imechukua miaka 33 kufikisha idadi ya watu bilioni 3. Ifikapo mwaka 2050 Dunia itakuwa na watu bilioni 9 na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kasi. Baadhi ya nchi zitakuwa na kasi kubwa ya ongezeko la watu. Miaka 1970 nchi ya Nigeria ilikuwa na watu milioni 57. Ifikapo mwaka 2050 kama hakutakuwa na uzazi wa mpango basi watakuwa na watu milioni 389, ambapo itakuwa ni idadi kubwa kubwa kuliko Taifa kubwa kiuchumi la Marekani. Nchi ya Tanzania inaongezeko la kasi ya watu, ambapo miaka 1970 kulikuwa na watu milioni 14, na idadi hiyo itaongezeka zaidi hadi Milioni 139 ifikapo mwaka 2050. Ifikapo mwaka 2100 inatarajiwa kushika nambari tatu au tano kati nchi zenye ongezeko kubwa la watu duniani.”
Soka kama madini
Fursa za uchumi imekuwa tija kwa nchi mbalimbali, lakini mchezo wa soka haukuwa umepata nafasi kubwa ya kujiimarisha kiuchumi. Wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali wanatazama fursa za uchumi kwenye nchi za Afrika kupitia njia mbalimbali na kukuza shughuli zao. Mfano, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF kulikuwa na nchi 38 ambazo hazikuwa na viwanja venye hadhi ya kutumika kwenye mashindnao yao. lakini kwa kipindi cha miaka mitano wamepunguza idadi hiyo hadi kufikisha nchi 12 ambazo zinaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha vinakuwa na viwanja vya kutosha ambavyo vinaweza kutumika kwenye mashindano mbalimbali.
Katika njia hii umiliki wa ubia, haki ya majina ya viwanja (naming rights) ambapo wamiliki wanatumia majina yao kwa nia ya kukuza biashara zao, mfano FNB Stadium (First National Bank) WA Afrika Kusini ni mfano mzuri ambao unavutia uwekezaji. Hivyo basi, kama yalivyo madini muhimu barani Afrika, nao mchezo wa soka unazidi kupasua anga.
Haki ya Akademi
Wachezaji wa zamani Afrika wamekuwa wamiliki wa vituo vya soka kama vile Samuel Eto’o Fils (Cameroon), Mohammed Kallon (Siera Leone), Abeid Ayew (Ghana) na wengineo wamekuwa kama fano bora wa kukuza vipaji ambavyo vinatamba kwenye Mataifa ya kigeni. Wimbi kubwa la wachezaji wenye asili ya Afrika kusajiliwa katika Mataifa ya Ulaya na Amerika ni ushahidi mwingine kuwa kuna soko na fursa kubwa.
Ni jambo la akawaida sasa wachezaji weusi kuchukua uraia wa nchi za Ulaya, na kwa namna kama hiyo wengi wa wawekezaji wanalitazama bara la Afrika kama sehemu muhimu ya kuvuna faida. Ujenzi wa vituo vya ushirikiano ama umiliki binafsi ni miongoni mwa mambo yanayowavutia wamiliki hao kuwekeza Afrika na kukuza soka zaidi.
Matokeo duni, maarifa makubwa
Katika vitu vinavyoshangaza sasa ni uwezo wa wawekezaji kuweka fedha zao kwenye vilabu ambavyo havina matokeo mazuri viwanjani. Mfano Kampuni ya INEOS ilikubali kununua hisa za umiliki wa Manchester United huku ikiwa na matokeo mabovu uwanjani. INEOS imepanua uwezo wake kupitia klabu hiyo huku ushawishi wake ukifika bara Afrika ambapo bila shaka yoyote baada ya ujio wao Tanzania watapanua fursa za kujitangaza na kutangaza vivutio vya utalii bila kujali matokeo ya uwanjani. Everton fc ilikuwa inadhaminiwa Sportpesa huku ikiwa haina ukubwa wa matokeo uwanjani. Kwahiyo taasisi za kimichezo zimeongeza wigo kutoka kutegemea matokeo ya uwanja hadi kukuza brandi yao kwenye fursa za sekta nyingine kama vile Afya, madini na utalii.
Comments
Loading…