in , ,

Hasira za Man United sokoni

LIGI KUU England inaelekea ukingoni. Kila kocha sasa anafikiria kutengeneza timu mpya kwa kuimarisha vikosi vyao. Ni dhahiri kati ya timu hizo basi itakuwa Manchester United ya Ruben Amorim. Tangu alipochukua kibarua cha kuinoa Man United amepitia nyakati ngumu ikiwemo kuwategemea wachezaji chipukizi katika kikosi cha pili. Ruben Amorim ndiye kocha atakayeingia sokoni kwa hasira zaidi kutokana na mwenendo wa timu hiyo. 

Hadi sasa Manchhester United inashikilia nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi huku ikiwa ina uhakika wa kubaki Ligi Kuu msimu ujao baada ya wapinzani wa karibu Ipswich Town kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa wikiendi iliyopita. Kwa kuzingatia  hilo, kumekuwa taarifa nyingi za wachezaji wanaowindwa na mashetani wekundu wa Old Traford ili kuimarisha kikosi chao huku baadhi ya waliopo wanatarajiwa kutemwa mwinoni mwa msimu huu. 

Miongoni mwa wachezaji ambao wanawindwa na Man United kwa sasa ni mshambuliaji wa Wolves Matheu Cunha mwenye asili ya Brazil. Taarifa zinaeleza kuwa Manchester United imemweka mshambuliaji huyo kama chaguo la kwanza kwenye kikosi chake. Mshambuliaji huyo ammewaridhisha mabosi wa Man United na kwamba wanamwone ndiye suluhisho katika kikosi chao kwenye upachikaji wa mabao kuanzia msimu ujao. 

Cunha amekuwa akipachika mabao ya kusisimua katika Ligi Kuu England na kuwavutia mabosi wa timu kubwa. Msimu huu amepachika mabao 16 katika mechi 31 akiwa kwenye kikosi cha Wolves. Mabao ya mshambuliaji huyo angalau yaliimarisha kikosi cha Wolves msimu huu kutokana na mwenendo wao wa kusuasua. 

Mbrazil huyo amekuhusishwa na kuhamia vilabu vikubwa barani Ulaya tangu msimu uliopita lakini hakuondoka. Ulipofika usajili wa mwezi Januari ilitarajiwa nyota huyo angeondoka, lakini aliamua kubaki klabu kwake na kusini mkataba mpya.  

Uamuzi wa kusaini mkataba mpya ndiyo umekuwa chachu na nguvu kwa klabu ya Wolves na kujenga ushawishi miongoni mwa wachezaji wao wanaowindwa. Kitendo cha kumshawishi nyota huyo asaini mkataba mpya kilichukuliwa kama uwezo mkubwa wa Wolves kwenye meza ya majadiliano. 

Wakati Cunha akihusishwa na kusajiliwa Man United, mwishoni mwa wiki walidhihirisha kuwa wao ni wakali wa soka kuliko vijana Old Traford baada ya kuwazaba 1-0.

Imeelezwa kuwa nyota huyo amewekewa kitita cha kumng’oa Wolves kiasi cha pauni milioni 62.5. 

Aidha, ili kuipata saini ya Cunha, Man United watalazimika kushindana na vigogo wengine ambao wanawinda huduma ya nyota huyo. Miongoni mwa timu hizo ni Newcastle United ambao wamepanga kuweka ofa yao nono mezani kwa Cunha mwenye umri wa miaka 25 iliatue St. James Park’s. 

Man United wamepanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao na nyota huyo ndiye anayewavutia na wanahusudu kuona ufundi wake ukifanyika akiwa amevalia jezi za Man United. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Amorim aliwahi kuonekana akizungumza na nyota huyo tangu alipowasili Man United, na mara baada ya kumalizika mchezo uliopita walikuwa kwenye mazungumzo wakielekea katika vyumba vya kubadilisha nguo.

“Nadhani anafanya vizuri katika klabu yake. Kazi yake imekuwa nzuri sana. ni mchezaji mwenye kipaji na vitu vya ziada, ni aina ya wachezaji ambao kila kocha angependa kuwa nao kwenye kikosi chake. “ alisema Amorim.

Mwanzoni mwa mwezi Aprili, Amorim alieleza umuhimu wa kupanga mikakati ya usajili kwa msimu ujao. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 alisema, “Kuna tabia ambazo zimekosekana kwenye kikosi chetu na tunajaribu kuangalia njia za kufanya ikiwemo kuziba mapengo. Ninaposema nahitaji wachezaji wakubwa haina maana kwamba nataka kusajili nyota toka Real Madrid. Ninacholenga ni wachezaji ambao wanapokuwa kikosini wanausoma mchezo na kuleta ubunifu wao kulingana na mfumo wetu. Naelewa wakati mwingine fedha zinasaidia. Tunatakiwa kuwa makini sana kwenye idara yetu ya usajili. Tunatakiwa kufahamu mfumo wetu na namna ya kucheza, pia wachezaji tunaosajili wawe sahihi kwa wale tunaowataka kufanya kile tunachopanga, hivyo ndivyo inavyotakiwa kwa msimu ujao.”

Mshambuliaji nyota wa klabu ya Ipswich Town, Liam Delap ni miongoni mwa nyota wanaotakiwa katika kikosi cha Manchester United. Delap ni mchezaji wa zamani wa Manchester City mwenye thamani ya pauni milioni 30. Lakini wanakabiliwa na changamoto toka kwa Chelsea ambao wanataka kumsajili kwenye kikosi chao. Man United wanatarajiwa kumtumia Marcus Rashford kama sehemu ya mpango wa kumsajili mshambuliaji Ollie Watkins. 

Chelsea na Man United zinapambana katika kufuzu Ligi ya Mabingwa kupitia mashindano ya Europa League.

Usajili wa nyota hao si mwisho, bali imeelezwa vigogo wa Man United watahakikisha wanaongeza nguvu ili kupigania ubingwa msimu ujao. Mojawapo ya kibarua cha msimu ujao ni kuhakikisha klabu hiyo inapigania ubingwa tofauti ilivyokuwa msimu huu ambapo ilikuwa inapambana kubaki Ligi Kuu kutokana na matokeo mabaya waliyopata hadi kumfukuza kocha wako Eric Ten Hag.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Bingwa mpya Ulaya, historia mpya

Tanzania Sports

Ubingwa Serie A bado mbichi