JULAI 25 mwaka huu vigogo wa soka nchini Simba na Yanga zitakutana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka, Azam Federation Cup (ASFC).
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Lake Tanganyika uliopo mkoani Kigoma. Huo ni mchezo muhimu wa kufunga msimu ambapo unazikutanisha timu hizo kwa mara tatu msimu huu 2020/2021 huku Simba ikiwa imezabwa mara mbili na kutoka sare mara moja.
Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu huu Simba na Yanga zilitoka sare 1-1. Mchezo wa marudiano Simba ilizabwa bao 1-0 na Yanga. Katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Simba ilifungwa kwa matuta na Yanga.
Kana kwamba haitoshi, Simba imetwaa ubingwa msimu huu kinyongea baada ya kushindwa kumfunga mtani wake wa jadi. Ubingwa mtamu ni pale unapochukuliwa baada ya kumshughulikia mtani wako wa jadi. Lakini mashabiki na viongozi wa Simba wanafahamu kuwa utamu wa ubingwa wa amsimu 2020/2021 umeingia doa baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na Zawadi Mauya.
Vijana wa Didier Gomes wataingia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho huku wakiwa na uchu wa kulipiza kisasi cha kufungwa katika Ligi kuu. Kwa maana hiyo mchezo wa fainali unatarajiwa kuwa na presha kubwa kwa timu zote, Yanga watakataka kuendeleza ubabe na kuonesha kuwa walistahili kuinyuka timu hiyo. Simba watakuwa na uchu wa kulipa kisasi cha kufungwa na kuonesha kuwa wao ndio wababe wa soka nchini kwa sasa, na hakuna mwingine.
HOFU YA MAKOCHA
Makocha wa timu zote mbili wanahofiana, kimbinu,uchezaji na uwajibikaji wa timu. Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi akizungumzia kuelekea mchezo huo ameonesha kumhofia mshambuliaji wa Simba na nahodha wao John Bocco.
Akizungumza na gazeti la michezo la Mwanaspoti jumatatu wiki hii amebainisha kuwa, “Simba ina wachezaji wengi wazuri lakini Bocco ni hatari zaidi, napenda aina yake ya uchezaji kwani anajua nini akifanye katika wakati sahihi, anajitahidi kutumia nafasi. Hata akiwa peke yake anapambana kupata nafasi za kufunga. Ni mchezaji wa kuchungwa zaidi uwanjani,”
Kwa upande wake kocha wa Simba, Didier Gomes amenukuliwa kumhofia kiungomshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kama mmoja wa wachezaji nguzo ya ushindi wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu.
“Feisal ni mchezaji mzuri pale Yanga. Anajua mpira,anajua namna ya kuwasoma wapinzani na kupeleka mashambulizi mbele, nampenda sana,” amesema Gomes.
Kauli hizo mbili zinaonesha bayana mikakati ya makocha hao itakuwa kwenye eneo la kiungo na safu za ulinzi. Ni kama vile akilini wanapanga kuzuia kufungwa, lakini wakati huo huo wakionesha hawaangalii namna ya kufunga. Kauli hizo zinabainisha namna gani mechi ya fainali haitakuwa jambo jepesi. Badala yake timu zote mbili zinataka kuibuka na ushindi kwa namna yoyote ile.
UKUTA MAJARIBUNI
Safu za ulinzi za Simba na Yanga zinakabiliwa na wakati mgumu zaidi kuhakikisha nyavu zao hatikiswi. Pascal Wawa akiwa na Joash Onyango Achieng watakuwa na kazi moja tu; kuhakikisha washambuliaji wa Yanga hawapati nafasi ya kufumania nyavu zao.
Hali kadhalika Dickson Job na Bakari Nondo Mwamnyeto watakuwa na kazi ya kuwachunga washambuliaji wa Simba wasilete madhara. Kama kuna eneo litakuwa majaribuni basi hili la kiungo ndio shughuli pevu. Ni vita vya Bocco na Job, kule Onyango na Yacouba Sogne. Kwenye nafasi za pembeni itakuwa vita kati ya Luis Miwuissone na Adeyum Saleh, huku Mohammed Hussein atakumbana na Tuisila Kisinda. Katikati ya dimba kutakuwa na shughuli ya Taddeo Lwanga na Tonombe Mukoko. Nguzo hizi ndizo zitajenga ukuta mgumu au laini na kusababisha madhara kwa timu zao.
NUSU FAINALI YA LAWRENCE GAMA
Fahamu kuwa katika michezo miwili ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ilichezwa kwenye viwanja vyenye historiana ;Lawrence Gama. Nusu fainali za ASFC 2021 zote zilichezwa katika viwanja alivyojenga aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora na Ruvuma, Dkt.Lawrence Mtazama Gama. Maono na usimamizi wa Gama ndio matunda ya viwanja vya CCM Majimaji mjini Songea na Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
MZEE MPILI vs MANARA
Katikati siku za hivi karibunu Mzee Mpili ameibuka na kuwa kiburudisho katika mchezo wa soka kwa sababu amefanikiwa kuziba mdomo wa msemaji wa Simba, Haji Manara. Kati ya wasemaji wa vilabu vya soka ambao wamekua gumzo bila kujali wanaongea pointi au porojo basi ni Hai Manara wa Simba.
Jukwaa la kusema sema ameachiwa huku baadhi wakiendeleza utaratibu wa kusema taarifa za timu zao bila kurusha vijembe au kuhangaika kuzingumzia timu zingine ambazo hawapaswi kuzimemea. Mzee Mpili baada ya kupiga mikwara viongozi wa Yanga, akageuka lulu katikati ya gumzo la mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Simba.
Mzee huyo aliwahakikisha ushindi wana Yanga kitu ambacho kilitokea kweli. Kipigo cha 1-0 kutoka kwa Yanga ndicho kiini cha kunyamazishwa kwa Haji Manara na washabiki wengi wa Simba. Moyoni wanajua utamu wa ubingwa ni kumtandika magoli mengi mtani wa jadi, lakini hawajafanikiwa. Sasa shughuli imehamia Kigoma. Ni Mzee Mpili au Manara, mojawapo atacheka au kununa. Shughuli ije Kigoma.
Comments
Loading…