in

Yanga ‘Unbeaten’, Simba ‘Pira’ biriani

Simba vs Yanga

WENYEJI wa pambano la mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Yanga walitoshana nguvu dhidi ya  wataniwao wa jadi Simba katika mchezo uliofanyika jumamosi Nobvemba 7 mwaka huu.  Wikiendi hii imekuwa ya aina yake na mchezo huo umetuletea mambo kadhaa muhimu ambayo  tunayaangazia katika makala haya. 

1. Mashabiki roho mkononi 

Nilikuwa ukumbi mmoja wa soka mjini Morogoro nikitazama mechi kati ya watani wa jadi  Yanga na Simba. Siti ya nyuma yangu alikaa kijana mmoja aliyevalia jezi ya Simba. Zilipofika  dakika ya 83 ya mchezo kijana huyo aliinamisha kichwa kukata tamaa. mashabiki wa Yanga  waliokuwepo ukumbini walimvisha skafu na jezi ya Yanga.  

Lakini kibao kikageuka mara baada ya Simba kusawazisha bao kupitia kwa beki wake Joash  Onyango Ochieng. Shabiki huyo alianguka kutoka kwenye kiti alichokaa hadi chini pwaa!  Akapoteza fahamu. Ndipo mashabiki wa Yanga wakwa wanampa huduma ya kwanza ya kumlaza  vizuri, kumpepea na kumwagia maji waliyokuwa nayo kwenye vyupa.  

Kisha wakambeba kumwingiza kwenye chumba cha huduma ya kwanza. Sijui nini kiliendelea,  lakini naamini aliondoka salama. Mechi ya Yanga na Simba zinakuwa na presha kubwa  miongoni mwa mashabiki,wadau,viongozi wa timu, serikalini na kila kona ya nchi. Ni mechi  ambayo mashabiki wanakuwa na roho mkononi. 

2. Simba wanacheza kama mabingwa haswa 

Mabingwa watetezi simba wanacheza soka la uhakika. Ilikuwa burudani kuwatamani namna  wanavopasiana. Ni burudani sana kuwatazama, ingawa wana ‘vijitabia’ vya ulalamishi kama  ilivyokuwa Barcelona ya Pep Guardiola kila ilipokutana na Real Madrid ya Jose Mourinho ama  kwenye mashindano ya Ulaya mara nyingi walikuwa walalamishi mno kwa mwamuzi.  

Simba walipia pasi fupi fupi na walipanga viungo wawili wakabaji Mzamiru Yassin na Jonas  Mkude. Eneo hili liliwafanya watawale mchezo zaidi, licha ya makosa ya mmoja mmoja katika  kipindi chote cha mchezo. Ukiacha makosa, uzembe na kukosa maarifa ya kuipenya ngome ya  ngumu ya Yanga, kwa hakika Simba wanacheza mpira mzuri sana. 

3. Ukuta mgumu wa Yanga na spidi 

Kuna umwamba wa Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto kama mabeki wa kati, halafu  kuna spidi ya Tuisila Kisinda na Farid Mussa. Licha ya Moro kutolewa mapema lakini ilionesha  namna alivyo mchezaji muhimu kikosini. Ni kiongozi thabiti. 

Wachezaji hawa waimeifanya Yanga iwe timu inayocheza kwa kasi zaidi na kuwafanya mabeki  wa Simba kuwekwa kwenye shinikizo kila wakati. Tazama kasi ya Farid Mussa ambaye alikuwa  kwenye ‘free role’, akicheza pembeni kushoto, katikati na kurudi nyuma kuchukua mipira  kwenda mbele. 

Spidi ya Tuisila Kisinda ndiyo iliwamaliza Simba katika kipindi cha kwanza, ambapo  walishindwa kumdhibiti hivyo kumfanyia madhambi eneo la hatari na kuzaa bao la kuongoza.  Hii inanikumbusha pale kocha wa Real Maadrid Zinedine Zidane alipokuwa akimpanga Gareth  Bale, sababu ilikuwa ni hii; Speed, pace and power. Kasi, nguvu na nafasi vilihitajika kuipa uhai  timu. Hivyo Real Madrid ilitumia nafasi chache kwa kasi na nguvu. Ndiyo kazi ya Tuisila  Kisinda, nadhano Onyango kalala na viatu. 

4. Vita ya kifundi ilikuwa tamu pembeni 

Cedric Kaze kwa vile aliwasoma mabeki wa pembeni wa Simba,naye akachora mstari  kuhakikisha mabeki wake wa pembeni hawafanyi kama wanavyofanya wa Simba. Yassin  Mustafa upande wa kushoto mara nyingi alipandisha mashambulizi ya Yanga na kuishia mstari  wa katikati yaani nusu yao.  

Hali kadhalika Kibwana Shomari naye alikuwa akiishia eneo hilo na kufanya kazi ya ulinzi zaidi  badala ya kucheza kama beki mshambuliaji wa pembeni. Vita hii ilisababisha Mohammed  Hussein na Shomari Kapombe wawe wanapanda kwa tahadhari. Shomari Kapombe alikuwa  hatari zaidi kuliko Mohammed Hussein ambaye naye alifanya kama Yaasin Mustafa kuishia  kwenye nusu yake. Kisinda alinyukana na Mohammed Hussein, huku Mosquiness akichuana na Yassin au Kibwana Shomari. 

5. Onyango ni mwamba mwenye bahati  

Refa amekupatia kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Tuisila Kisinda. Kisha mwamuzi alikuwa  amemuonya mara mbili ikiwa tayari alikuwa hatarini huenda angepewa kadi ya pili ya njano  hivyo kuambulia nyekundu.  

Nilitegemea kocha wa Simba, Sven Vandebroeck asingemrudisha uwanjani kuendelea na kipindi  cha pili, badala yake alimtoa Larry Bwalya. Vyanzo vya taarifa vilieleza mapema wiki hii kuwa  Bwalya alipangwa kucheza mchezo huo huku akiwa anachomwa sindano la kuondoa maumivu  aliyonayo. 

Hata hivyo kasi ya Kisinda ilikuwa mwiba kwa Onyango, licha ya bahati ya kusahihisha makosa  yake kwa kusawazisha bao. Onyango ni beki mtulivu, anayo maarifa na amefanikiwa kuwa beki  anayokokota mpira kwa ufasaha na kwa umbali mrefu. Anao utulivu kichwani, licha ya kufanya  makosa hakutoka mchezoni yaani akili zake zilikuwa zimetulia mno. 

6. Tonombe anawakilisha maarifa ya wachezaji wa kigeni 

Wachezaji wa kigeni wanawakilishwa vema na Tonombe Mukoko, Mosquines,Tusila Kisinda,  Joash Onyango, Pascal Wawa Lamine Moro ni baadhi ya wachezaji ambao wanawakilisha  maarifa ya wageni waliopo VPL. Wachezaji hawa wameongeza ufundi,ushindani,msisimko wa Ligi na kuwavutia washabiki wengi.  

Unapomtazama Tuisila, kisha ukamgeukia Wawa na halafu Moussine unaona wazi kabisa ni  wachezaji ambao wamekucha chafu ya ushindi katika timu zao. Wanawakilisha maarifa  makubwa ya kandanda na kuwaachia wachezaji wazawa. Yanga wanao mawinga watatu mahiri  kwa sasa, Deus Kaseke, Farid Mussa na Tuisila Kisinda. 

Bila shaka Kisinda atakuwa anawaachia maarifa zaidi kutokana na kasi yake. Toinombo Mukono  ametuonesha nini kazi ya kiungo mkabaji. Amezuia pasi vipenyo nyingi za Simba kwenye 18 za  Yanga.  

Amepanda mbele kusaidia mashambulizi, apiga mashuti lango la Simba, amatumia nguvu zake  na ikibidi amecheza mechi kama kiungo mkabaji halisi. Ni furaha kumwona akiwakilisha Yanga.  Mmakonde Mosquines naye ni fundi mzuri anayeleta ladha soka la Bongo, akiwa na mpira  haeleweki atauficha upande upande upi na kusababisha madhara lango la adui. 

7. Yacouba si Sarpong, wana vitu tofauti. 

Ukimpanga Yacouba kwenye 4-3-3 maana yake anakuongezea spidi na uwezo wa kukaa na  mpra. Yacouba ana mikimbio ya aina yake, na muda aliokuwa uwanjani alikuwa hatari zaidi  kuliko Sarpong.  

Katika mfumo huo huo ukimpanga Michael Sarpong maana yake anatakiwa kuzungukwa na  wachezaji wawili ambao watakuwa na kazi ya kutengeneza pasi ili afunge. Yacouba anaweza  kukusadia kwenye ulinzi, na akacheza kama mshambuliaji mmoja peke yake mbele katika  mfumo wa 4-5-1, lakini Sarpong atahitaji zaidi mfumo 4-4-2 ambao ni ‘diamond’ zaidi. 

Sarpong anaweza kuwa machachari dhidi ya mabeki, ni kama alivyokuwa Joseph Kaniki ambaye  alitegemea ‘pace and power’ nafasi na nguvu ili kuwashinda mabeki. Kwa Yacouba anakuja na  kitu tofauti kwani anaweza kumiliki mpira kwa muda mrefu mbele ya beki kuliko Sarpong. Je  wanaweza kuchea pamoja? Jibu ni ndio na hapana. Ni hapana kwa sababu watakonsa balansi  kati ya kiungo na ushambuliaji. 

8. ‘Plan B’ ya Kaze? 

Simba wanapiga mpira mwingi sana. Wamejaza wabunifu kwenye kikosi chao. Wanaweza  kutawala mchezo na kukufunga wakati wowote. lakini Yanga ya Cedric Kaze ‘plan B’ yake  ilikuwa ipi?  

Kwa haraka mimi ninaweza kusema kulihitajika nguvu na akili ya Calinhos kipindi cha pili  kutokana na uwezo, mipira yake yenye malengo na mirefu ingewafanya Simba warudi nyuma  zaidi na kusababisha shinikizo kwao. Calinhos ni mmoja tu ambaye anajua kutumia nafasi za  mipira ya adhabu,pasi ndefu na maarifa ya ziada kulainisha kazi za timu. Kipindi cha pili Yanga  ilikuwa inalinda zaidi bao lao, na akamuingiza Mauya kwa kulinda, hali ambayo ilisababisha  Shomari Kapombe aongeze kasi ya kupanda zaidi na kuwasumbua Yanga. 

Uzuri ni kwamba Yanga hawajafungwa mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.  Kutoka sare na Simba wamedhihirisha kuwa wamedhamiria kulitwaa taji la Ligi Kuu Tanzania  Bara. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Hatua Muhimu za kuinua Netiboli Tanzania

Yanga v SIMBA

Hakuna Yanga Na Simba Safi Kwa Mkupuo !!!