in

Hatua Muhimu za kuinua Netiboli Tanzania

Mpira wa pete au netiboli ulikuwa miongoni mwa michezo maarufu sana nchini Tanzania.

Mchezo huu ulianzishwa wakati wa ukoloni. Mchezo huu ulikusudiwa kuwa burudani na ulianza kuchezwa shuleni. Ili kuukuza na kuuendeleza, vilijengwa viwanja kwenye takribani shule zote za msingi nchini.

Waanzilishi wa mchezo huo walikuwa Waingereza mnamo mwaka 1890. Kawaida ya mchezo huo ni kwamba huchezwa na timu mbili na kila timu inakuwa na wachezaji saba.

Mchezo huu siku za nyuma ulikuwa ukichezwa hasa shuleni, vyuoni na katika majeshi. Baadaye ulienea kwenye mashirika  na hata katika wizara na idara mbalimbali za serikali. Maendeleo ya mchezo huu yalifanya  kuwe na vyama vya kusimamia taratibu na sheria zake  katika kila mkoa.

Mwaka 1966, chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kiliundwa kukuza mchezo wa wanawake nchini Tanzania, ligi na mashindano yalianzishwa katika juhudi za kuongeza umaarufu wa mchezo huo.

Majukumu makubwa ya Chaneta ni kuandaa mashindano yote ya netiboli  nchini, kuendeleza vipaji vya wanamichezo wa netiboli, kuandaa semina na mafunzo kwa waamuzi na makocha kutoka mikoa yote vilevile kutafuta watalaamu wa kufundisha kutoka maeneo mengine nje ya Tanzania.

Pia Chaneta ilipewa jukumu la kuinua mchezo huo na kufikia viwango vya kimataifa kama ambavyo barani Ulaya na Australia walivyofanya kuipaisha netiboli kwenye viwango hivyo. Ili kutimiza azma hiyo Chaneta ilianza kueneza mchezo huo kutoka ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuzingatia mbinu na sheria za kisasa.

Miaka ya nyuma kulishuhudiwa baadhi ya vijiji vikishiriki mashindano ya ligi za wilaya, hali ambayo ilitoa mwelekeo wa mchezo huo kukua na kufikia ngazi ya kimataifa. Hatua hiyo iliongeza watu kutoka kila pembe ya nchi kuupenda mchezo huo kama ilivyokuwa kwenye soka.

Mashindano ya netiboli miaka 1970, 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 yaliongeza hamasa ya kuupenda mchezo huo.

Tangu kuundwa kwa Chaneta kumefanyika mashindano mbalimbali kama vile Kombe la Challenge la Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Taifa, Kombe la Klabu bingwa taifa na Kombe la Nje.

Maendeleo ya netiboli nchini tangu kuundwa kwa Chaneta yalijionesha kutokana na kuwepo kwa utaratibu wa mashindano, kufanikiwa kupata waamuzi na makocha wenye sifa za kimataifa. Licha ya jitihada hizo mara nyingi Tanzania haijafanikiwa kupenya kwenda katika medani ya kimataifa.

KLABU BINGWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI MWAKA 1985

Kushindwa kufanya vizuri katika mashindano makubwa kulirudisha ari na hamasa kwa wapenzi na mashabiki wa mchezo huo kwani walijiona wanyonge.

Hata hivyo unyonge huo ulipunguzwa mnamo mwaka 1985 kwenye Uwanja wa Gerezani jijini Dar es Salaam yalikofanyika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati. Aliyekuwepo uwanjani hapo alishuhudia mambo yaliyokuwa yakifanyika.

Wapenzi wa Netiboli walifaidi uhondo wa aina ya pekee  wakati vijana  wa timu ya Bora walipoudhihirishia uwanja uliofurika watazamaji kuwa wao ni wachezaji wenye uhakika na ufundi.

Ilikuwa siku ya pekee nchini kwa wapenzi na mashabiki wa netiboli, siku ambayo haitasahaulika kamwe na wachezaji wa timu ya Malawi. Huenda mwaka 1985 ulikuwa wa neema kwa timu ya Bora iliyowachezesha Asha Juma, Suma Oliva, Judith Chifupa, Oliver Shimwela,  Edna John, Penina Maduhu na Amina Bakari.

Vijana hao ambao walikuwa ‘kichefuchefu’ kwa timu pinzani kutokana na machachari yao wakiwa uwanjani, walicheza mchezo wa kasi  wenye mashambulizi yaliyoandamana na sauti za vifijo na nderemo za mashabiki zilizidisha hasira na hofu kwa wachezaji wa timu ya Malawi.

Hali hiyo ilitoa mwanya kwa Asha Juma (GK), kutoa mpira kwa Suma Oliva (GD), akisaidiwa na Judith Chifupa (WD) hali iliyomfanya mchazaji wa kiungo Oliver Shimwela kutopumua alipoweza kudaka mipira ya hapa na pale  na kuwapasia Edna  John (GA) akishirikiana vema na Penina Maduhu (WA) bila makosa walikuwa wakimpasia pasi maridadi mfungaji hodari  Amina Bakari.

Wachezaji wa Bora walionekana kuwazidi maarifa wapinzani wao waliopigwa na butwaa na kutota kwa magoli. Washambuliaji hodari Edna John na Amina Bakari walilisakama goli la Malawi mithili ya siafu dhidi ya mende. Wachezaji wa Malawi walijikuta kama watazamaji wakati Bora kwa mbwembwe nyingi wakitupia pasi fupi fupi  zilizokuwa na lengo la kufika kwa kila mmoja bila kipingamizi hadi kupata goli. Hakika ilikuwa siku mbaya kwa timu ya Malawi.

Chenga za mwili za hapa na pale katika mchezo huo ziliwafanya wapinzani kukimbia ovyo uwanjani  nap engine kugongana wenyew. Hadi mwisho wa mchezo huo, Bora ilionekana imara na yenye stamina ya kuendelea wakati timu kutoka ilikuwa hoi kabisa, hatimaye Bora ilishinda kwa magoli 36-23.

Ushindi huo uliifanya Tanzania kuvishwa taji la Umalkia wa Netiboli Afrika Mashariki na Kati. Hayo yote yalikuwa ni mafanikio ya nidhamu na juhudi nyingi za wachezaji, maandalizi ya kutosha yaliyofanywa na viongozi wa klabu pamoja na ushauri wa Chaneta.

Wapo wapi sasa wachezaji watakaoinua netiboli mkoani Singida, kina nani watabadili nafasi za wachezaji kama Queen Msemwa, Grace Mwaikambo, Rehema Mhina, Aurelia Joseph, Lucy Daniel na kucheza netiboli kwa kiwango cha juu.

Wapi sasa vinara wa netiboli kutoka Mbeya, Morogoro, Kagera, Tanga, Tabora, Arusha na Dodoma. Ziko wapi timu kali za netiboli ambazo zitazungumzwa kama Simba na Yanga? Wakati ule ulikuwa ukizitaja Bandari ya Tanga, Jeshi Stars, Bima, Bora, Biashara ya Singida, Kilitex, General Tyre, Printpak, Bhesco, KIA, Kurugenzi, Nyuki na kadhalika.

Wapi mafunzo kwa makocha kama ambavyo tumekuwa tukisikia katika soka mara Kilimanjaro, Rukwa  na kwingineko kuhusu mafunzo ya makocha wa mchezo huo. Netiboli itafanya nini kurudisha mafunzo hayo kwa mikoa mbalimbali kama Tabora na kwingineko ili kupata wakufunzi wazuri wa mchezo huo? Wapi viongozi wapenda netiboli kama enzi za Bi. Sophia Kawawa, G. Tibakweitira, Hindu Lilla, C.B Simfukwe, na Alfred Tandau?

Jambo la msingi linaloweza kuufanya mchezo wa netiboli kurudi na kuwa maarufu nchini Tanzania ni daima kuwa vitani kuyashinda mazingira yanayofanya mchezo huu usiwe maarufu; hapo ndipo tofauti kati ya binadamu na viumbe wengine hujitokeza.

Uongozi wa Chaneta unapaswa urudi mezani na kukubaliana na hali ya usasa iliyopo sasa ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa Watanzania. Siku zote viongozi wa vyama husika wakiamua kushupalia jambo na kupanga mikakati ya namna ya kulifanikisha ni rahisi kwa maelfu ya watu kuungana kufuatilia mambao yao.

Report

Written by Amini Nyaungo

For the past 9 years, I have been working as the Sports news Journalist in online and print media this experience help me to be utilized by the different sports events where I have got chances to the media as the football pundit in different media in Tanzania.

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
cedric kaze

Tathimini za Kaze kazini Yanga

Simba vs Yanga

Yanga ‘Unbeaten’, Simba ‘Pira’ biriani