in

Wazir Junior ni Adam Salamba mpya?

Wazir Junior

Wakati Luc Eymael anaonekana kutoelewana na benchi la ufundi la klabu Yanga, benchi ambalo yeye mwenyewe ndiye alikuwa kocha mkuu , macho yangu yalikuwa yanamtazama Charles Boniface Mkwasa.

Huyu ni mmoja ya watu wachache duniani wanaoijua vyema sana Yanga kwa sababu amecheza Yanga kwa mafanikio makubwa sana tena nahodha wa timu hii.

Charles Boniface Mkwasa hakuishia kuiongoza Yanga uwanjani kama nahodha tu,  baada ya kumaliza muda wake wa kucheza mpira alihamia kwenye eneo jingine la ukocha. Eneo ambalo lilimpa nafasi tena ya kuitumikia Yanga.

Kwa vipindi tofauti tofauti amekuwa kocha wa Yanga. Kila kwenye nyakati ngumu yeye aliibuka kusimama kama msaada ili aiokoe timu yake ya moyoni. Ana mapenzi makubwa sana na klabu hii.

Mapenzi ambayo yalimfanya asimame kama kiongozi tena katibu mkuu wa klabu kipindi ambacho Yanga inakimbiwa na viongozi wake. Alikimbia mwenyekiti Yusuph Manji, mwenyekiti msaidizi akakimbia na baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji wakakimbia pia.

Tanzania Sports
Wazir Junior akisaini mkataba

Yeye alisimama kama Musa kuwaongoza wana Yanga kuelekea kwenye kanani yao. Kwenye kipindi cha uongozi wake kulikuwepo na timu moja inayoitwa Lipuli FC. Timu ambayo ilikuwa na mshambuliaji nyota kwa wakati huo anayeitwa Adam Salamba.

Moja ya wachezaji ambao kwa kipindi hicho timu nyingi zilikuwa zinatamani kuwa naye. Charles Boniface Mkwasa ni mmoja ya viongozi ambao walifanya jaribio la kumsajili Adam Salamba lakini kwa bahati mbaya Yanga ilikuwa na ukata.

Mwisho wa siku Adam Salamba alienda kwa watani wao Simba. Sehemu ambayo ilitufanya tumsahau. Hakuonesha kiwango chake kama kile ambacho alikionesha wakati akiwa Lipuli FC pamoja na Stand United ya Shinyanga.

Adam Salamba ni moja ya vielelezo vya washambuliaji wa Tanzania. Washambuliaji ambao wamekuwa hawana mwendelezo wa viwango vyao. Kumekuwa na utamaduni wa baadhi ya washambuliaji kuwika msimu mmoja tu.

Msimu juzi tulibahatika kuwa na Salim Aiye kutoka Mwadui FC ambaye alimaliza ligi akiwa na magoli 20. Magoli ambayo ni mengi sana kwa mshambuliaji wa ndani. Swali kubwa kwake ambalo alitakiwa kutujibu ni namna gani ambavyo anaweza kuendeleza kiwango chake.

KMC FC walimchukua kwa ajili ya msimu uliomalizika. Kwenye karatasi ilionekana ni usajili mzuri sana kwa KMC FC . Kwa Salim Aiye kutoka Mwadui FC sehemu ambayo hakukuwepo na uhakika mkubwa wa mshahara kwenda sehemu ambayo kuna uhakika wa mshahara kilikuwa kitu kizuri kwake.

Lakini pamoja na mazingira mazuri ndani ya klabu ya KMC FC, Salim Aiye hakufanikiwa kucheza kwenye kiwango kile kile ambacho alikuwa nacho Mwadui FC.

KMC FC pia walimsajili Charles Ilanfya kutoka Mwadui FC , kabla ya kuja KMC , Charles Ilanfya alikuwa na kiwango kizuri sana akiwa Mwadui FC lakini kwa bahati mbaya alishindwa kukiendeleza alipofika KMC FC.

Unamkumbuka Eliud Ambokile wa Mbeya City? Ambaye alimaliza ligi akiwa na magoli zaidi ya kumi? Wengi tulitegemea mwendelezo mzuri kutoka kwake lakini kwa bahati mbaya ameshindwa kuendeleza kiwango chake alichokuwa nacho Mbeya City.

Azam FC wanajivunia Shaaban Idd Chilunda kama mtoto ambaye amekulia kwenye Academy yao,  kuna msimu aliwika lakini mpaka sasa hivi ameshindwa kuwa na mwendelezo kama ilivyo kwa Paul Nonga wa Mwadui FC achana na huyu wa Lipuli FC.

Kuna orodha ndefu sana ya washambuliaji wengi wa ndani ambao wamekuwa hawana mwendelezo.  Vitalis Mayanga wa Ndanda FC , Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons, Dany Lyanga, Omary Mponda wa Ndanda FC, Mohamed Rashind wa Tanzania Prisons,  Marcel Kaheza wa Maji Maji FC. Wote hawa waliwika msimu mmoja tu.

Jana Yanga walimsajili Wazir Junior kutoka Mbao FC. Mchezaji ambaye amemaliza msimu wa ligi kuu akiwa na magoli 13 nyuma ya Meddie Kagere ambaye ameibuka kama mfungaji bora msimu huu.

Hapana shaka Wazir Junior kafanya vyema sana akiwa na Mbao FC msimu ulioisha . Swali kubwa linabaki kwake , ataendeleza kiwango hiki cha msimu ulioisha ? Atatatua tatizo la kutokuwa na mwendelezo ? Tatizo ambalo lipo kwa washambuliaji wengi wa Tanzania ? Ndiyo maana nikauliza Wazir Junior ni Adam Salamba mpya?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Beno Kakolanya

Kwanini Azam FC wasimsajili Kakolanya ?

Dar young africans

Yanga wakata nyota 14, Morrison ndani?