in

Kwanini Azam FC wasimsajili Kakolanya ?

Beno Kakolanya

Tanzania Prisons ndiyo ilikuwa sehemu ya kwanza kwa watu wengi kumtambua. Alikuwa ni mmoja ya magolikipa wachache sana ambao walikuwa na kiwango kikubwa lakini wakiwa wanacheza katika vilabu ambavyo vinaonekana ni vidogo.

Mikono yake ilikuwa dhabiti kulinda milingoti mitatu ya Tanzania Prisons. Nyakati ambazo timu yake ilikosa jibu kwa maswali magumu ndani ya uwanja yeye aliibuka kama jibu sahihi katika maswali magumu.

Ni mara chache sana kwa golikipa kuipa alama muhimu tena na nyingi timu husika lakini mikono yake ilichomoa michomo mingi ambayo iliipa alama nyingi Tanzania Prisons. Wakati ambao safu ya ushambuliaji ilipokuwa inashindwa kufunga magoli yeye alilinda timu isifungwe magoli.

Wakati ambao safu ya ushambuliaji ilipokuwa inafunga magoli yeye alisamama kulinda hayo magoli. Mikono yake iliwavutia wengi sana kwenye mpira wetu. Yanga ndiyo timu iliyobahatika kumnasa kipa huyu mahiri.

Aliisaidia kwa kiasi kikubwa Yanga. Kitu kizuri au kibaya wakati anafika Yanga aliikuta Yanga ambayo ilikuwa inaunga unga ndani na nje ya uwanja. Ilikuwa Yanga ambayo ilikuwa haina uwezo mkubwa wa kulipa mishahara kwa wachezaji.

Hata dau lake la usajili halikumaliziwa kwa sababu ya ukata mkubwa ambao ulikuwa ndani ya klabu ya Yanga. Kutokulipwa kwake pesa ya usajili kilimfanya asimame kwanza nje ya uwanja. Alishinikiza kulipwa Nadal yake ya msingi.

Alitaka kuwakumbusha viongozi wa Yanga umuhimu wa kutimiza ahadi muhimu ambazo zilikuwa ndani ya mkataba. Ahadi ambazo zilisimama kama makubaliano ya msingi ndani ya mkataba wake.

Tanzania Sports
Beno Kakolanya

Kwa jicho la haraka haraka hapa viongozi wa Yanga walikuwa ndani ya makosa kwa wao kushindwa kutimiza makubaliano ya msingi yaliyokuwepo ndani ya mkataba wa Yanga na Beno Kakolanya. Kwa kifupi Beno Kakolanya alikuwa sahihi kugomea kwa sababu ya kudai haki zake za msingi.

Tuachane na hayo kwanza. Turudi kwenye ile Yanga ambayo Beno Kakolanya aliikuta. Yanga ambayo haikuwa na wachezaji nyota wengi ndani ya uwanja. Hii ilikuwa tofauti na Yanga ambazo zilikuwepo nyakati za nyuma.

Ilikuwa Yanga ya tia maji tia maji. Beno Kakolanya alisimama kama moja ya nguzo muhimu ndani ya kikosi cha Yanga kwa kipindi hicho. Aliikoa sana Yanga, unaikumbuka mechi ya Simba na Yanga ambayo iliisha kwa suluhu katika uwanja wa Mkapa?

Mechi ambayo michomo aliyoiokoa Beno Kakolanya ilimfanya kuonekana ni shujaa mkubwa ndani ya kikosi hicho na kwenye mechi hiyo kwa ujumla. Vyote hivi najaribu kuvionesha ili uone umuhimu wa Beno Kakolanya.

Beno Kakolanya ni moja ya magolikipa wachache ambao wanaweza kukuhakikishia kukupa alama muhimu ndani ya mchezo. Ni moja ya magolikipa wachache ambao wanaweza kulinda magoli ya timu na timu ikapata alama muhimu.

Beno Kakolanya ni moja ya magolikipa wachache ambao ni wadaraja la juu kwenye ligi yetu. Beno Kakolanya ni moja ya magolikipa ambao wanafaa kuwepo kwenye timu ambayo inagombania ubingwa tena yeye akiwa ni golikipa namba moja.

Kwa bahati mbaya yuko sehemu ambayo yeye anatumika kama golikipa namba mbili. Sehemu ambayo haimpi uwezo mkubwa wa kuonesha kiwango chake kikubwa ambacho amejaliwa. Ni sehemu ambayo inamnyima nafasi ndani ya uwanja.

Azam Fc imeachana na golikipa Mghana, Razack Abalora. Haina golikipa wa kiwango cha juu kwa muda huu. Azam FC ni moja ya timu ambayo kwa sasa inagombania ubingwa wa ligi kuu pamoja na ule ubingwa wa Azam Federation Cup.

Kuwepo kwenye nafasi ya kugombania ubingwa wa kombe lolote kunakulazimu uwe na wachezaji ambao watakubeba kwenye hiyo hali. Moja ya wachezaji ambao ni muhimu ni wachezaji katika eneo la golikipa. Ni eneo ambalo  lina nafasi kubwa katika kukuhakikishia ubingwa.

Beno Kakolanya yupo kwenye daraja hilo la kuibeba timu ambayo inawania ubingwa. Hivo kuliko kwa Azam FC kuwekeza nguvu nyingi kusajili golikipa wa kimataifa kwanini wasiwaze namna ya kumchukua Beno Kakolanya ambaye anaweza akawapa kitu bora kuzidi golikipa wa nje?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Usajili wa Yanga

Tetesi za usajili Bongo ‘Deal done’

Wazir Junior

Wazir Junior ni Adam Salamba mpya?