in , , ,

Tunaionea huruma miguu mizito ya Ajib

Tushaibatiza majina mengi sana miguu yake, hii ndiyo miguu ambayo iliitwa miguu ya dhahabu. Miguu ambayo ilikuwa inang’arisha mpira wa miguu na kuweka katika umbo la msichana mrembo ambaye kila kijana anatamani kuwa naye.

Nani asiyependa kumuona Ibrahim Ajib akicheza? nani asiyetamani kuona sanaa kubwa iliyopo katika miguu ya Ibrahim Ajib? Hapana shaka hakuna mtu asiyetamani kukiona kipaji hiki ambacho inasemekana kilishushwa moja kwa moja kutoka mbinguni.

Kipaji ambacho Watanzania wengi wanajivunia kuwa nacho. Kipaji ambacho Watanzania wengi wanaamini ipo siku kipaji hiki kitaimba nyimbo za kimataifa na kila sikio na jicho duniani litakuwa kwa Ibrahim Ajib.

Swali kubwa ambalo mpaka sasa linasubiria jibu kupatikana ni lini Ibrahim Ajib atafikia kwenye sehemu ambazo sisi tunatamani azifikie? Ni lini dunia nzima itapiga goti na kushujudia miguu ya Ibrahim Ajib?

Ni lini Ibrahim Ajib ataamua kuweka alama ambazo zinaishi? alama ambazo vizazi vingi duniani vitamuenzi na kumheshimu? Kwa mbali naona historia ya Haruna Moshi Bobani katika maisha ya Ibrahim Ajib.

Naona kabisa dalili za kumsimulia Ibrahim Ajib kuwa alikuwa ni mmoja ya wachezaji ambao waliwahi kuwa na vipaji vikubwa hapa nchini Lakini kwa bahati mbaya tutamsimulia wakati ambao akiwa hajafanya chochote kikubwa.

Tutamsimulia wakati ambao Ibrahim Ajib akiwa hana cha kujivunia katika maisha yake ya soka la ushindani. Hatokuwa na kitabu cha kuvutia kama kilivyo kitabu cha Mbwana Ally Samatta.

Ukitazama kipaji cha Ibrahim Ajib kina nafasi kubwa kabisa kutoka sehemu ambayo Haruna Moshi “Boban” aliwahi kukwama na kumpeleka sehemu ambayo Mbwana Samatta yupo.

Sijui kama hili Ibrahim Ajib analiona? kuna wakati huwa nafikiria inawezekana sisi Watanzania tunamuona Ibrahim Ajib kama mchezaji mkubwa lakini yeye akajiona kama mchezaji mdogo ndiyo maana hata juhudi zake ni ndogo.

Kinachomtofautisha Ibrahim Ajib na Mbwana Samatta ni juhudi. Mwingine anajuhudi kubwa na mwingine ana juhudi ndogo ndiyo maana kila uchwao anapiga hatua za kurudi nyuma.

Leo hii Ibrahim Ajib hana nafasi kwenye kikosi chake cha Simba. Halioni hilo yeye anaona ni sawa tu, kinachomfurahisha ni uwezo wake wa kuingiza mshahara tu na siyo uwezo wake wa kuingiza mafanikio makubwa ndani ya uwanjani.

Miguu yake ni ya dhahabu ila tatizo ina majipu ambayo hayampi nafasi ya yeye kukimbia kwenda mbele palipo na mlima mafanikio, hawezi kupanda kwa sababu ya majibu yake na hana jitihada za yeye kuendelea kupigana ipasavyo ili kuyaondoa hayo majipu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Natamani Mkude astaafu kwenye jezi ya Simba !

Tanzania Sports

Corona: Ni wakati wa viongozi kuchukua hatua madhubuti