in , ,

Natamani Mkude astaafu kwenye jezi ya Simba !

Najua swali kubwa ambalo wengi tunajiuliza ni lini Jonas Mkude atapata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Hii ndiyo ndoto kubwa ya Watanzania wengi kwa sasa.

Watanzania wengi wanatamani sana kuuza wachezaji nje ya nchi kwenye ligi ambazo zinaonekana zimepiga hatua ya kimaendeleo kisoka kuzidi sisi hapa nchini kwa imani kuwa kwenye ligi hizo mchezaji atakuwa mkubwa zaidi kiakili na mtazamo wa mpira pamoja kiwango chake uwanjani.

Moja ya wachezaji ambao mimi binafsi natamani siku moja wafike mbali kwenye ligi moja kubwa ni Jonas Mkude. Kiungo bora wa eneo la kuzuia kuwahi kutokea hapa nchini. Ana sifa nyingi sana za kiungo wa kisasa wa kuzuia.

Ana uwezo mkubwa wa kuunganisha safu ya ulinzi na safu ya kiungo cha ushambuliaji. Miguu yake hufuata mipira eneo la chini ya timu na kuipeleka eneo la juu la timu kwa ajili ya kusambaza mashambulizi.

Jonas Mkude anauwezo mkubwa pia wa kutuliza presha ya mchezo na kuifanya timu kucheza katika presha ndogo kiuchezaji hali ambayo huifanya timu kucheza bila makosa mengi binafsi.

Mchezaji huyu wa kisasa siyo rahisi kukosa timu ya kisasa kwenye ulimwengu huu wa soka la kisasa. Jonas Mkude natamani sana aende huko ulimwenguni kwa ajili ya kutumikia haswa kipaji chake .

Baada Jonas Mkude kufanikiwa kucheza soka la kulipwa katika ligi bora basi natamani sana Jonas Mkude huyu aje atundike dalunga katika klabu ya Simba . Hapa ndipo sehemu sahihi ya yeye kustaafiwa kuliko sehemu nyingine.

Sehemu ambayo yeye alianzia soka lake la kulipwa tangu akiwa na umri mdogo. Amelelewa katika klabu hii ya Simba, amekuzwa katika klabu hii ya Simba na kukomazwa zaidi katika klabu hii ya Simba.

Ameitumikia klabu ya Simba kwa moyo mkubwa na kwa muda mrefu bila ya yeye kuhama kwenda klabu nyingine yoyote duniani mpaka sasa hivi. Ameonesha kuiheshimu vya kutosha klabu ambayo inaonekana baba na mama wa kipaji chake.

Ameitolea jasho jingi klabu hii ya Simba na klabu hii imejitoa kwa ajili ya Jonas Mkude kuanzia viongozi wa klabu mpaka mashabiki wa klabu hii ya Simba , kuna undugu mkubwa ambao umeungana kati ya Jonas Mkude na Simba kwa ujumla.

Jonas Mkude ambaye aliwahi kuwa nahodha wa dhati katika klabu hii , mpaka sasa hivi Jonas Mkude ndiye mchezaji mwandamizi wa klabu hii ya Simba anaheshima yake kubwa sana ndani ya Uzi wa Simba.

Heshima ambayo natamani sana iendelee kubaki mpaka siku ya mwisho ambayo Jonas Mkude atapoamua kustaafu mpira wa miguu. Natamani sana Jonas Mkude jezi yake aitundike katika mitaa ya Msimbazi.

Mitaa ambayo imemlea , mitaa ambayo imemtambulisha kwa kiasi kikubwa Jonas Mkude , mitaa ambayo kwa kiasi kikubwa imebaki katika moyo wake na mashabiki wa Simba wamemweka katika moyo wake.

Kuna muunganiko mkubwa sana kati ya Jonas Mkude na Simba , muunganiko ambao natamani sana uishe vizuri kwenye siku zake za mwisho katika mpira wa miguu. Natamani sana mechi yake ya mwisho katika mpira wa miguu iwe akiwa amevaa jezi ya Simba

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

CORONA: Hakuna soka hadi Mei

Tanzania Sports

Tunaionea huruma miguu mizito ya Ajib