in , , , ,

Samatta: Haikuwa sahihi kusaini Villa Januari

Inawezekana ardhi ya Tanzania iliwahi kushuhudia mvua nyingi zenye maji ya furaha, maji ambayo yaliweka tabasamu kwenye nyuso za Watanzania wengi.

Maji ambayo yalikuja kama baraka kwetu sisi. Wazee wetu waliwahi kubahatika kupata maji ya baraka baada ya Tanganyika kupata uhuru kutoka kwenye mikono ya wakoloni.

Ni wakoloni ambao waliziba uhuru wa wazee wetu, hawakuwa huru hata kufanya kazi zao binafsi za kuwaingizia kipato cha biashara, miguu yao ilifungwa, midomo yao ilizibwa, macho yao yalitiwa upofu na kilichokuwa kimebaki ni akili tu.

Hii ndiyo silaha ya kwanza ambayo walikuwa nayo; ndiyo silaha ambayo ilianza kufanya kazi kwa kasi baada ya neno ‘natamani’ kupitia kwenye akili zao.

Ndio hapo wakaanza kutamani kitu kimoja baada ya kingine. Walitamani mikono yao ifanye kazi ambazo zingewaingizia kipato, wakatamani miguu yao iwe huru kutembea na macho yao yawe na uwezo wa kuona.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maji ya baraka yaliyotokana na mvua ya uhuru kumwagika katika ardhi yetu ya Tanganyika, hatimaye tukawa huru.

Naam, ni uhuru ambao ulituwezesha kusimama sisi kama sisi. uhuru ambao ulitupa matamanio mengi makubwa ya kufanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali kwenye ardhi hii bora duniani.

Matamanio ambayo yalitusogeza mpaka kwenye mpira wa miguu, mchezo wa hisia. Ni hisia zilizopo kwenye mioyo yetu, sehemu ambako ndicho kuna chumba tulivu kilichopambwa na maua waridi, yaani chumba cha mahaba.

Chumba ambacho tuliamua kukitunza kwa ajili ya mpenzi wetu anayeitwa mpira wa miguu. Huyu ndiye mpenzi ambaye anapendwa sana; ndiye mpenzi pekee ambaye tupo tayari kumhonga shilingi bilioni moja ndani ya miezi ya miezi miwili.

Mwezi Januari mechi ya Simba na Yanga iliingiza shilingi milioni mia tano na mwezi wa tatu mwaka huu mechi hii hii ilifanikiwa kuingiza kiasi cha shilingi milioni mia tano. Ndani ya miezi miwili shilingi bilioni moja imepatikana kwenye mpira .

Huu ni ‘Upendo wa Agape’, upendo ambao unaweza ukasababisha kufanyika kitu ambacho kwa macho ya nyama unaweza ukahisi hakiwezekani , ndiyo upendo ambao unaweza ukasababisha kutengeneza kisiwa jangwani.

Ndiyo upendo ambao unatupa furaha kumtazama kijana wetu Mbwana Ally Samatta, kijana ambaye alituletea mvua ya furaha yenye maji ya baraka baada ya kutupa uhuru katika mpira wa miguu.

Uhuru ambao tulikuwa tunautamani sana kuupata siku moja; tulitamani kuona Mtanzania mmoja akicheza kwenye Ligi Kuu ya England (EPL)nafasi ambayo Mrisho Ngassa aliinusa lakini hakufanikiwa kuipata kama ambavyo Samatta.

Inawezekana kabisa Watanzania wengi walikuwa wanatamani sana Samatta apate timu kwenye moja ya ligi tano barani Ulaya hasa hasa baada ya yeye kufanya vizuri na KR Genk ya Ubelgiji.

Wengi waliona ni muda sahihi kwake yeye kuondoka, hata yeye alionekana kabisa anataka kuondoka kwa wakati huo ndiyo maana aliamua kubadilisha wakala na kumpata wakala ambaye ni moja ya wakala wa Saido Mane wa Liverpool.

Kumpata wakala huyu kulikuwa na maana moja kubwa kuwa Samatta alikuwa anataka kuja England kwenye EPL – kitu ambacho alifanikiwa na akasajiliwa na Aston Villa.

Turudi hapa’ matamanio makubwa kwake yeye yalikuwa kucheza EPL kitu ambacho ni kizuri na kikubwa sana kwenye ndoto ya maisha yake, lakini swali kubwa ni iwapo ulikuwa ni muda sahihi na sehemu sahihi kwake kujiunga?

Twende taratibu; tujiulize wote kwa pamoja ili tupate jibu moja kwa pamoja. Ilikuwa ni muda sahihi? kwangu Mimi ukiniuliza nitakwambia haukuwa muda sahihi. Kwa nini nasema hivi?

Sikiliza nikuambie kitu kimoja ambacho kitatufikirisha kwa pamoja. Mbwana Ally Samatta kaenda Aston Villa mwezi wa kwanza, mwezi ambao hufanyika dirisha dogo la usajili, huu muda ulikuwa si muda sahihi kwake yeye kuondoka Ubelgiji.

Angemaliza msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji akaendelea kufunga mabao kama ambavyo alivyokuwa anafunga ili kuzidi kujiweka sokoni na dirisha la usajili la majira ya joto la mwezi wa sita ndiyo lingeamua kuwa huo ndiyo ulikuwa muda sahihi kwake yeye kuondoka kwa sababu angepata timu ambayo angeanza nayo ligi.

Kupata timu katikati ya ligi tena ambayo ina hatihati ya kushuka daraja hakumweki yeye kwenye akili nzuri kucheza. Akili yake inamweka kwenye presha kubwa na hofu ya yeye kuogopa kushuka daraja.

Pili, kupata timu mwezi wa sita kungempa nafasi kubwa kwake yeye kufanya pre-season na timu husika ili kuelewana na wachezaji wenzake na Kujenga muunganiko mzuri ndani ya timu kwa sasa hakuna muunganiko ndani ya timu yake ya Aston Villa.

Aston Villa ilikuwa sehemu sahihi kwake yeye kwenda ? Hili ni swali ambalo linafuata baada ya kujiuliza kama kwa wakati ule ulikuwa muda sahihi kwake yeye kwenda Aston Villa. Swali hili naomba tulijibu kwa pamoja kwa kutafakari hiki:

Mbwana Samatta alienda Aston Villa mwezi wa kwanza, ligi ikiwa inatoa taswira ya nani ambaye anaweza kuwa bingwa na nani ambaye anaweza kushuka daraja; moja ya timu ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kushuka daraja ni Aston Villa.

Najaribu kujiuliza kama walilitazama hili kwa undani kuwa Aston Villa ilikuwa sehemu yenye presha kubwa kwake kwa sababu ya timu kupigana kutoshuka daraja na ikizingatia ni mara yake ya kwanza kucheza EPL; azoee mazingira ya ligi , afu azoeee joto la kupambana kutoshuka daraja .

Walitazama kama Aston Villa walikuwa na hatari kubwa ya kushuka daraja? Au lengo ni Mbwana Samatta kucheza lEPL? Hapana shaka kama lengo lilikuwa kucheza ligi kuu ya England basi Aston Villa haikuwa sehenu sahihi kwa Mbwana Samatta

Kipigo cha juzi kutoka kwa Leicester City kimewafanya wawe katika mazingira magumu sana ya kubaki ligi kuu; wanashika nafasi ya 19 wakiwa na alama 25 wakiwa wamebakiza mechi 10, kati ya hizo mechi tano ni dhidi ya timu ambazo zinagombania nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) ambazo ni Liverpool, Wolves, Arsenal, Chelsea, Everton na Manchester United.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Man U wawashangaza City

Tanzania Sports

Corona na hatari ligi kubwa Ulaya