in , , ,

Chelsea ni kupigwa tu

 

*Man U safi, Swansea walala

 

Sasa ni kupigwa tu; ndivyo unavyoweza kuelezea hali ya mabingwa watetezi wa England, Chelsea, kwani wamepoteza mchezo was aba kati ya 12 waliyocheza katika Ligi Kuu ya England (EPL).

Huku kocha wao, Jose Mourinho akiwa kwenye majukwaa baada ya kulimwa kadi nyekundu na kuadhibiwa kuukosa mchezo huo kutokana na kutoa lugha chafu na kumkasirikia mwamuzi Jonathan Moss, Chelsea walilala kwa Stoke.

Mourinho alipewa adhabu wakati timu yake ikilala 2-1 kwa West Ham mwishoni mwa mwezi uliopita, na vijana wake ambao kipa Asmir Begovic alidai wanamuunga mkono kocha wao, walishindwa kumwondolea shinikizo, kwa kukubali kichapo cha 1-0.

Wasaidizi wa Mourinho waliwasimamia wachezaji lakini wakajikuta wakipata matokeo yale yale, baada ya Marko Arnautovic kupiga tikitaka nzuri dakika ya 53 na kuutia mpira kimiani, hivyo kuwashusha Chelsea hadi nafasi ya 16 kati ya timu 20 zinazoshiriki EPL.

Chelsea walipata nafasi za kufunga, ambapo mshambuliaji kutoka Barcelona, Pedro, alipopata yake mpira uligonga mwamba wakati Loic Remy alipotakiwa kuutia wake kimiani, alijikwaa alipotaka kumzunguka kipa aliyeonesha umahiri Jumamosi hii,.

Chelsea waliomba penati kwa madai kwamba kipa huyo wa kimataifa wa England alimwangusha Remy, lakini mwamuzi Anthony Taylor alikataa. Butland pia aliokoa mipira dhahiri kwenda wavuni ya Ramires na Diego Costa.

Chelsea walitawala mchezo, lakini Stoke waliwatuliza kutokana na mpangilio wao kamambe wa ulinzi, huku wakishangiliwa vilivyo na washabiki wa nyumbani, maarufu kama wafinyanga vyungu.

Mourinho atarejea kwenye benchi la ufundi Chelsea watakapowakaribisha Norwich Novemba 21, ambapo katika kile ambacho hakikutarajiwa, sasa mabingwa hao watetezi wanajaribu kujiokoa kutumbukia kwenye eneo la kushuka daraja.

Costa aliendelea na aina ya uchezaji wa kuwatisha na kuwagongesha wachezaji wapinzani, ambao unachukiwa nao pamoja na makocha wao, na Jumamosi hii aliyeonja joto ya jiwe alikuwa Ryan Showcross, ambaye hata hivyo alijizuia hasira hadi mwisho wa mchezo.

 

MANCHESTER UNITED WAPO VIZURI

Jesse Lingard akifunga bao la kwanza kwa man u
Jesse Lingard akifunga bao la kwanza kwa man u

Manchester United wamefanikiwa kuvuka kikwazo kwa kuwafunga West Bromwich Albion 2-0, huku mchezaji wao, Jesse Lingard  akifunga bao lake la kwanza kwa Man U.

Wakicheza nyumbani Old Trafford, Man U walimaliza kipindi cha kwanza bila bao, hadi mapema kipindi cha pili, Lingard (22) alipofuma mpira akiwa kwenye kona ya boksi la penati, akajikunja na kucheka na nyavu.

Saido Berahino aliyeingia akitoka benchi alikosa nafasi ya wazi ya kusawazisha bao, ambapo akiwa karibu kabisa na goli, kipa akiwa keshapotea, alipiga vibaya mpira wa kichwa uliopaa juu.

Man U walijihakikishia ushindi  kwa penati iliyofungwa na Juan Mata baada ya mshambuliaji Anthony Martial kuangushwa na Gareth McAuley, aliyepewa kadi nyekundu. Ushindi huo unawaacha United katika nafasi ya nne wakati West Brom ni wa 12.

Huu ulikuwa ushindi wa kwanza katika mechi tatu kwa wenyeji, ambao pia wamefanya vyema kwenye ulinzi, kwani hawajaruhusu bao katika dakika 550.

Bado kocha Louis van Gaal anashambuliwa na washabiki ambao wanapinga aina yake ya soka ya kujihami, wakiimba; ‘shambulia, shambulia, shambulia!’ Van Gaal alisema ni vyema washabiki wakamzomea yeye badala ya wachezaji na jana akasema haelewi uamuzi wa washabiki hao.

 

MATOKEO MENGINE, MECHI ZA JANA

Matokeo mengine ya EPL jana
Matokeo mengine ya EPL jana

Katika mechi ya mapema Jumamosi ambapo Newcastle walisafiri umbali mrefu kucheza na Bournemouth wakati wa chakula cha mchana, wenyeji walipata ushindi wa 1-0. Leicester walitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuwazima Watford 2-1.

Sunderland bado hawajapata dawa ya ugonjwa wao hata wakiwa nyumbani, kwani wamebaki nafasi ya pili kutoka mkiani baada ya kukubali kipigo cha 1-0 kutoka kwa Southampton. Kabla ya mechi hiyo, kocha wao, Sam Allerdyice alidai wachezaji wake bado wanashindwa kucheza vyema mbele ya washabiki wao wengi nyumbani.

Norwich wamepata mwelekeo wa kutoka pabaya kwenye msimamo wa ligi, kwani walipowakaribisha Swansea hawakuwacha salama, bali waliwapiga bao 1-0 na kuwafanya vijana hao wa Garry Monk wajiulize kulikoni wameanza kupoteza mechi.

West Ham walitoshana nguvu 1-1 na Everton hivyo kwamba wote wamepanda nafasi, West Ham wakishika ya tano na Everton ya nane, lakini msimamo unaweza kubadilika Jumapili hii baada ya mechi kadhaa.

Vinara wa ligi hiyo, Manchester City wanashuka dimbani ugenini kucheza na Aston Villa ambao msimu huu si wazuri sana na wameshafukuza kocha Tim Sherwood. Kocha mpya, Remi Garde atatazama mechi hiyo akiwa jukwaani, aanze kujua ukubwa wa kazi iliyopo, baada ya Sherwood kusema ni nzito kubadili mwelekeo hasi unaowaathiri Villa kwa miaka kadhaa sasa.

Arsenal wanaoshika nafasi ya pili wanawakaribisha mahasimu wao wa London Kaskazini – Tottenham Hotspur, baada ya kuoga kichapo cha 5-1 kwenye ligi ya mabingwa Ulaya kutoka kwa Bayern Munich.

Liverpool ni wenyeji wa Crystal Palace, ambapo baada ya kuonja ushindi Anfield, kocha Jurgen Klopp anataka kuuendeleza. Katika mechi ya kumuaga nahodha Steven Gerrard msimu uliopita uwanjani hapo hapo, Palace waliwatandika Liverpool 3-1. Ni Alhamisi tu Liver wamerejea kutoka safari ndefu nchini Urusi walikowafunga Rubin Kazan 1-0.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ARSENAL v. TOTTENHAM

Tanzania Sports

Arsenal, Man City doro