in , , ,

Man U wawashangaza City


*Imani kwa Lampard yalipa Chelsea

ILIIKUWA siku ya aina yake Old Trafford, baada ya Manchester United kuwachakaza watani wao wa Jiji la Manchester, Manchester City.

Ole Gunnar Solskjaer ambaye alisema wana kawaida ya kuwashangaza wapinzani wao mara kwa mara, alithibitisha tena kwa kumzidi maarifa mpinzani wake, Pep Guardiola.

Ilikuwa mechi ya 50 kwa Ole kama kocha wa United aliyochezea enzi za Sir Alex Ferguson na aliingia uwanjani kwenye Dabi ya Manchester akiwa na mchanganyiko wa mawazo, wengi wakiwapa nafasi ya ushindi City ambao ni kana kwamba wameshapoteza ubingwa wanaoutetea.

Sasa United wamekwenda mechi 10 wakiwa hawajapoteza hata moja, wakifunga mabao 2-0 dhidi ya City, wakipanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 45, tatu pungufu ya wanaoshika nafasi ya nne – Chelsea.

Ole alipata kuwaongoza United kwenda mechi 11 bila kufungwa tangu kuteuliwa kwake kuchukua nafasi hiyo kama kaimu Desemba 2018 kisha kuipewa kabisa kama kocha mkuu. Hii ni mara ya kwanza tangu kuondoka kwa Fergie United wanashinda mechi zote mbili dhidi ya mahasimu wao hao.

Mara ya mwisho Fergie alishinda mechi zote mbili kwenye msimu wa 2009.2010 lakini pia Dave Sexton alifanya hivyo msimu wa 1978/79. Anaungana pia na Jurgen Klopp wa Liverpool ambaye ni kocha pekee kufanikiwa kutoka na ushindi mara tatu dhidi ya Guardiola aliyewafundisha Barcelona na Bayern Munich, katika msimu mmoja.

Ama kwa kutazama kwenye kupoteza mechi, huu umetokea kuwa wakati mbaya msimu huu kwa matokeo yasiyokuwa mazuri kwa Guardiola. Ukilinganisha na Jose Mourinho alipokuwa Old Trafford, bado Ole hajamfikia, kwa sababu ana alama 10 pungufu yake katika mechi 50, akifunga bao moja pungufu na kukubali kuchapwa mabao 20 zaidi ya mtangulizi wake huyo.

‘Ufufuko’ wa United unakuja baada ya kusajiliwa kwa kiungo mahiri wa Ureno, Bruno Fernandes. Ni huyu aliyetoa usaidizi kwenye bao la kwanza la Anthony Martial na tangu aanze kuchezea United Februari mosi amehusishwa moja kwa moja na mabao mengi zaidi katika ligi kuu hii.

Kwingineko Chelsea walikuwa na kicheko, baada ya kocha Frank Lampard kuwaongoza kwenye ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Everton waliokuwa wameanza kuimarika chini ya kocha wao mpya na mzoefu Carlo Ancelotti.

Mchezaji wa timu ya Chelsea
Mchezaji wa timu ya Chelsea

Imani waliyoweka wakuu wa Stamford Bridge kwa mchezaji huyo wa zamani, licha ya kuanza kwa kusuasua sana inaonekana inalipa.

Chelsea wamekuwa wakizungukwa na maswali mengi msimu huu, lakini kwa kuwasambaratisha Everton kwa kiasi kikubwa hivyo cha mabao, majibu yanaonekana kwamba yanakuja.

Chipukizi mpya kutoka kwenye akademia yao kuonesha vitu vyake safari hii alikuwa Billy Gilmour, aliyecheza vyema pia kwenye ushindi dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya Kombe la FA majuzi.

Mskochi huyo mwenye umri wa miaka 18 tu alionesha uwapo wake na ukawa na mguso mkubwa kwa watu, akicheza vyema kwenye kiungo. Lampard amekuwa na kawaida sasa ya kutumia zaidi wachezaji chipukizi kwenye mechi nyingi.

Msimamo wa Epl mpaka sasa
Msimamo wa Epl mpaka sasa

Washabiki sasa watakuwa wanazidi kuwa na imani na mchezaji huyu wao wa zamani baada ya kuwa na ushindi mmoja tu katika mechi sita za ligi kuu. Wanapambana kuona kwamba waweze kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mbele yao wapo Liverpool ambao wanachukuliwa kama mabingwa tayari, Manchester City na Leicester. Tofauti ya alama zao na Leicester ni mbili lakini huku nyuma wanakabwa na Man United, Wolves, Sheffield United Tottenham Hotspur na Arsenal.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
mtanange wa YANGA NA SIMBA

Simba walishinda nje ya uwanja , Yanga wakashinda ndani ya uwanja

Tanzania Sports

Samatta: Haikuwa sahihi kusaini Villa Januari