in , ,

Simba walishinda nje ya uwanja , Yanga wakashinda ndani ya uwanja

Sherehe ya mpira Tanzania ilimalizika jana kwa kuwakutanisha Yanga Sc na Simba SC katika uwanja mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga Sc walifanikiwa kushinda goli moja kwa bila, goli ambalo lilifungwa na Bernard Morrison kwa mpira wa adhabu.

Huu ulikuwa mchezo wa pili ndani ya mwaka huu 2020 baada ya mwezi wa kwanza mwaka huu tukishuhudia timu hizi zikitoka sare ya magoli 2-2 kwenye uwanja huu huu wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa jana ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakubwa kama Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa CAF Ahmad Ahmad pamoja na Rais TFF Wallance Karia.

Kwenye mchezo huu Simba SC ambaye aliingia uwanjani akiwa anaongoza ligi kwa alama 68 yeye alionekana vyema kufanikiwa kushinda nje ya uwanja tofauti na Yanga ambao walionekana kushindwa nje ya uwanja ila wakaja kushinda ndani ya uwanja.

KWANINI SIMBA SC WALISHINDA NDANI YA UWANJA ?

Kabla ya mchezo huu Simba SC mashabiki wake walikuwa wanajiamini sana kuzidi mashabiki wa Yanga. Hali ambayo ilifanya wajitokeze kwa wingi katika uwanja wa Taifa kwa kuwazidi wapinzani wao Yanga.

Wakati nafika kwenye uwanja wa Taifa mashabiki wengi waliokuwepo nje ya uwanja walikuwa mashabiki wa Simba SC . Nilipofanikiwa kuingia ndani ya uwanja mashabiki waliokuwa wengi ni mashabiki wa Simba SC.

Mashabiki wa Simba SC walifanikiwa kujaza majukwaa yao ambayo wamezoeleka siku zote kukaa na walifanikiwa kukaa mpaka kwenye eneo ambalo mashabiki wa Yanga huwa wanakaa .

Kwa kiasi kikubwa eneo lao walilijaza na eneo dogo la Yanga walifanikiwa kulikalia . Hii inaonesha mashabiki wa Simba walikuwa wamehamasika sana na ndiyo maana nikasema Simba SC walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kushinda nje ya uwanja.

YANGA WALIFANIKIWA KUSHINDA NDANI YA UWANJA

Yanga kupitia mwalimu wake Luc Eymael alijua ndani ya kikosi cha Simba SC mchezaji muhimu ni Cloatus Chota Chama na mchezaji bora ni Luiz Miquissone alichokifanya ni kuwaanzisha kwa pamoja Papy Kabamba Tshishimbi na Feisal Salum “Fei toto” kwa pamoja.

Papy Kabamba Tshishimbi na Feisal Salum “Fei toto” walikuwa na kazi mbili ambazo wote walizitimiza vizuri kwa pamoja. Walihakikisha Cloatus Chota Chama na Luiz Miquissone hawapati uhuru wa kucheza, kila walipokuwa wanashika mpira walikuwa wanakabwa.

Hawa watu ndiyo huwa wanaamua mashambulizi ya Simba SC yaanzie wapi na yapitie wapi ndiyo maana jana walinyimwa uhuru wa wao kuamua mashambulizi ya Simba SC kuyaanzisha na kuyapitisha katika njia sahihi.

Kazi ya pili ambayo Papy Kabamba “Tshishimbi” na Feisal Salum “Fei Toto” waliyopewa ni wao kuhakikisha wanapofanikiwa kuupoka mpira wanakuwa na uwezo wa kukaa nao mguuni bila kupoteza na kuusambaza kwenye timu, hapa ndipo ukawa mwanzo wa Yanga kushinda ndani ya uwanja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Feisal Salum “Fei Toto” atawasumbua Simba leo

Tanzania Sports

Man U wawashangaza City