in , ,

MTOANO KOMBE LA LIGI:

Chelsea, Arsenal nje

*Mourinho kufukuzwa? Majeruhi wazidi Arsenal

 

Mabingwa watetezi wa Kombe la Ligi – Chelsea na wenzao wa London – Arsenal wametupwa nje ya michuano hiyo, huku wakipata hasara kubwa kutokana na wachezaji wao kujeruhiwa.

Wakati Arsenal iliwapoteza wachezaji wake wawili muhimu, Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya tano tu, aliyechukua nafasi yake – Theo Walcott aliumia pia dakika 13 tu baadaye. Chelsea walitolewa kwa penati na Stoke baada ya kwenda sare ya 1-1 kwenye muda wa dakika 120 huku mshambuliaji wao, Diego Costa akipelekwa hospitali baada ya kuumia mbavu, alizoumia na kutolewa uwanjani dakika ya 33.

Wakati kocha wa Chelsea, Jose Mourinho atakuwa na wakati mgumu kutokana na timu yake kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu na sasa kupokonywa Kombe la Ligi, Arsene Wenger wa Arsenal atakabiliwa na kazi ngumu ya kujipanga kwa mechi muhimu zijazo ugenini dhidi ya Swansea na Bayern Munich katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kisha Tottenham Hotspur.

Kuumia kwa wachezaji hao kunaongeza orodha ya majeruhi, kwani tayari nahodha Mikel Arteta, Jack Wilshere, Danny Welbeck, Aaron Ramsey, Tomas Rosicky na kipa namba mbili David Ospina, ikimaanisha kwamba Petr Cech atakuwa uwanjani kwa karibu kila mechi.

Arsenal waliadhibiwa vibaya na timu ndogo ya Sheffield Wednesday kwa kunyukwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Hillsborough ambako Wenger hajapata kushinda huko kwa miaka 19. Kwa ushindi huo Wednesday wametinga robo fainali.

Jose Mourinho
Jose Mourinho

Arsenal walianza kuadhibiwa mapema dakika ya 27 pale Ross Wallace alipofunga kilaini akiwa umbali wa yadi 18 kutoka golini na Cech hakuwa na la kufanya. Wallace alimtengenezea nafasi murua Lucas Joao aliyefunga kwa kichwa dakika ya 40 kabla ya Sam Hutchinson kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Arsenal akiwa umbali wa yadi nne tu kunako dakika ya 51.

Wenger alishindwa kubadili mambo kutokana na kwamba alishafanya mabadiliko ya wachezaji mapema kabisa kipindi cha kwanza kutokana na kuumia wachezaji wale wawili, na wala haikuonekana kwamba waliokuwa uwanjani wangeweza kubadili matokeo.

Wednesday waliofika hatua hii baada ya kuwafunga Newcastle, wamefika robo fainali ya mashindano haya kwa mara ya kwanza katika miaka 13. Hawajapata kufungwa katika mechi tisa sasa lakini kocha wao, Carlos Carvalhal alisema kabla ya mechi kwamba uwezekano wao kushinda ulikuwa asilimia 10 tu. Arsenal walifungwa licha ya kutawala mchezo kwa asilimia 71.

Arsenal walionesha nguvu ya ushambuliaji na kutaka bao mara moja tu, pale kaimu nahodha, Per Mertesacker alipokaribia kufunga, lakini kipa Joseph Wildsmith akatumia vidole kurushia juu ya goli mpira. Mmiliki wa Wednesday, Dejphon Chansiri anataka klabu hiyo iingie EPL ifikapo 2017.

Makinda wa Arsenal walipelekeshwa kiaina na Sheffield "Jumatano"
Makinda wa Arsenal walipelekeshwa kiaina na Sheffield “Jumatano”

Ama kwa upande wa Mourinho, atakuwa katika tafakari nzito juu ya hatima yake klabuni hapo, licha ya ukweli kwamba amekuwa bado akiungwa mkono na mmiliki wa klabu, Roman Abramovich.

Tetesi ni kwamba mechi ya wikiendi ijayo dhidi ya Liverpool inaweza kuamua hatima yake, lakini vyanzo vingine vinadai kwamba anaweza kufungashiwa virago au mwenyewe kuondoka wakati wowote.

Stoke walishaelekea kushinda mechi hiyo kwa bao la Jon Walters lakini Loic Remy aliwasawazishia Chelsea katika dakika ya 90, hivyo mechi ikaingia dakika 30 za ziada kisha changamoto ya mikwaju ya penati ikaanza.

Kipa wa Stoke, Jack Butland alikuwa shujaa wa mechi hiyo, kwani aliokoa penati moja – na kwa bahati mbaya kwa mpigaji, ilikuwa ya Eden Hazard ambaye msimu huu amekuwa na kiwango kibaya na kocha Mourinho alishaeleza kushangazwa na hali hiyo.

Washabiki wa Stoke walionekana kumdhihaki Mourinho, hasa baada ya bao la Walters na kisha pale kipa wao alipookoa penati ya Hazard, wakimwashiria kwamba Jumatano hii asubuhi angekuwa amefukuzwa kazi, hivyo atafute ajira sehemu nyingine.

Katika mechi nyingine, Everton waliokwenda sare ya 1-1 na Norwich walifanikiwa kusonga mbele baada ya kuwafunga kwa penati 4-3. Hull na Leicester nao walienda sare kama hiyo, kisha Hull wakavuka kwa penati 5-4.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

USAJILI UPI UMEKUWA WA MAFANIKIO ZAIDI?

Tanzania Sports

Man United nao wakatwa