Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ni mtu mwenye akili, mwelewa na anayejua kuyapanga maneno yake kwa wakati.
Majuzi baada ya mechi baina ya timu yake na West Ham United alitoa maneno ya ajabu kidogo baada ya kukasirishwa na Hammers, akadai wamecheza mfumo wa soka ya karne ya 19.
Wakati Chelsea wanafukuzia nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, West Ham wanaofundishwa na Sam Allardyce ‘The Big Sam’ wanajiepusha na kushuka daraja na si ajabu wakati wowote wakawa mkiani huku Chelsea wakiwa kileleni.
Lakini katika mechi hiyo, kwenye dakika zote 90, sheria 17 za soka zikifuatwa, Chelsea na West Ham walitoka suluhu, yaano 0-0 na kuna wakati nusura Chelsea wapachikwe bao.
Mechi hiyo ilichezwa Jumatano nyumbani kwa Chelsea Stamford Bridge na alitoa kauli ya soka ya karne ya 19 kutokana na jinsi Hammers walivyolinda lango lao.
Hata hivyo, Mourinho inaelekea maneno hayo yalimtoka tu, akidhani kwamba kila mtu angemsikiliza na kumkubalia (isipokuwa West Ham bila shaka), lakini ukweli ni kwamba soka ya karne ya 19 haikuwa ya ‘kuweka basi golini’ kama Mourinho alivyopata kuita mtindo wa kujihami.
Tangu kuanzishwa kwa Chama cha Soka hapa Uingereza 1863, timu zilikuwa na wachezaji wazuri waliokuwa na kasi ya ajabu uwanjani, wala hawakuwa na mpango wa kukaa golini kuzuia bao lisiingie.
Wengi wao walijifunza soka katika shule za umma na kwenye vyuo vikuu, hakika inaelezwa kwamba soka ya wakati huo ungeipenda zaidi kwa kucheza wala si kuketi jukwaani au kusimama nje ya uwanja kuitazama.
Wachezaji walikimbia na mpira mpaka walipoupoteza au kunyang’anywa huku wachezaji wenzao wakiwafuata nyuma ili kumsaidia kutumbukiza wavuni iwapo angekuwa na kasi kuliko mpira akauacha nyuma.
Kazi kubwa enzi zile ilikuwa kukimbizia mpira kwenye lango la adui, naye adui akiushika mbio zinaanza tena wala hapakuwa sana na hizi pasi za siku hizi, hivyo Mourinho alichokisema ni kitu kisichokuwapo enzi hizo na amefurahisha tu baraza.
Kuna nukuu ya mchezaji katika mechi baina ya England na Scotland mwaka 1877 ambapo
Alfred Lyttleton alilalamikiwa sana kwa kukokota mno mpira badala ya kutoa pasi kwa wenzake, naye akajibu hivi; “nacheza kwa raha zangu mwenyewe Mkuu!” Na waliokuwa wakicheza walikuwa watu wakubwa, ndipo baadaye soka ikaenea kwa watu wa kati, wafanyakazi ndipo mambo ya pasi na kadhalika yakaja.
Kwa msingi huu, Mourinho anachoweza kufanya ni kuwafundisha vijana wake mbinu zaidi za kuwavuta maadui uwanjani, kuwazunguka, kuwapiga chenga na hata kutafuta kwa njia sahihi penati wanapopita kwenye ‘msitu’ wao.
Kumbukumbu nyingine zinaonesha pia kwamba katika fainali ya Kombe la FA mwaka 1883,
Blackburn Olympic waliwashangaza Old Etonians kwa mtindo wao wa ‘kurusha ndege’ kama za Athumani Iddi Chuji, yaani mipira mirefu mirefu tu kutoka wingi moja hadi nyingine. Hapakuwa na kupaki basi. Olympic walishinda 2-1 kwa mara ya kwanza na kubadili mchezo huo kabisa.
Uchezaji wa kulipwa ulihalalishwa hapa England 1885, nayo ni karne ya 19 anayodai kuizungumzia Mourinho na klabu bora zaidi zikaufanya mchezo huo kuanza kuwa biashara kuanzia 1888 zikishindana kwenye Ligi ya Soka.
Miaka mitatu baadaye ligi ilianzisha, je, timu hizi zilikuwaje katika ulinzi dimbani? Tangu miaka ya 1870 haikuwa jambo la ajabu kwa timu kuweka mafowadi wanaofikia sita hadi saba.
Kipaumbele kwa timu zote ilikuwa ni ushambuliaji tu wala si kiungo au ulinzi, maana huku nyuma waliona inatosha kuacha mabeki wawili tu
Ni baadaye kabisa ndipo timu zilianza kufikiria kupunguza washambuliaji na kuwarudisha kwenye kiungo na ikawa wanacheza mfumo wa 2-3-5 wakiuita mfumo huo piramidi na ikawa kabisa standard hadi mwishoni mwa miaka ya 1880.
Sasa utasemaje kwamba mfumo wa West Ham ulikuwa wa karne ya 19? Je, walicheza 2-3-5 kama enzi za Victoria? Hapana, Mourinho kakosea kabisa, labda tuseme yu gizani maana si mwanahistoria.
Kuna timu enzi zile zilikuwa na washambuliaji hadi tisa zikisema hata kuacha hao mabeki wawili wakae na kipa ni kupoteza rasilimali yao maana lengo lilikuwa kufunga, hawakuwa wamefikiria sana mambo ya kisayansi ya siku hizi ya viungo wakabaji, wa kati wachezeshaji. Haikutokea akawepo mshambuliaji mmoja tu mbele, hiyo si soka ya karne ya 19 anayoidai Mourinho. Adios.
Comments
Loading…