in

Kifua cha kocha wa Samatta kina maumivu makali

Dean Smith wa Aston Villa

WAKATI mwingine unaweza kuitazama orodha ya majina ya timu ukajua imekamilika. Majina ya wachezaji wenye kila sifa. Kuna wenye mashuti makali. Wenye ufundi wa mipira ya juu. Wenye maarifa ya hali ya juu. Wenye utundu wa kugundua mbinu za adui. Wenye kutumika kama wasoma mbinu za timu pinzani. Wabunifu na wanaotoa ufundi wa ziada.  

Kocha yeyote anafahamu mchezaji gani amtumie kwenye kusaka ushindi. Anaweza kumpanga mchezaji fulani kwa vile ana ujuzi wa kusoma mchezo. Anaweza kumnunua mchezaji fulani akijua kule aliko hatumiki vema au ana uwezo mzuri unaoweza kumsaidia katika kikosi chake. Mchezaji mwingine anakuwa mbunifu wa kiwango cha juu.

Wapo makocha ambao wamefanikiwa kununua wachezaji wa ngazi za chini ya kuwapaisha matawi ya juu. Eneo hilo, pengine na kwa maoni yangu Arsene Wenger na Alex Ferguson walikuwa wataalamu katika eneo hili kati ya makocha wengine wa Ligi Kuu England. Kwa sababu kama walikuwa na wasaka vipaji hodari maana yake wao walikuwa wameona utaalamu wa wasakaji wao.

Hali hiyo ndiyo aliyokuwa nayo Dean Smith wa Aston Villa. Jicho lake na benchi zima la ufundi liliamini kuwa kuwanunua washambuliaji walionao kikosini wangeweza kuyafanya mambo kuwa mepesi zaidi.

Walitamani magoli matamu. Walitamani shangwe pomoni. Walitamani sifa za maarifa yao zitambe katika Ligi Kuu England. Walitamani kuona Aston Villa inarudisha makali yake ya miaka iliyopita. Walitaka iwe Aston Villa inayoogopewa na wapinzani wao katika uwanja wowote ule.

Uwe uwanja wa ugenini au nyumbani. Walitaka kuona Liverpool, Manchester United, Arsenal, Chelsea Man City zinakuwa timu zinazotafakari mara mbili mbili linapofika suala la kupambana na Villa. Tena Villa ya kisasa. Dean Smith alicheza kamari yake kwenda kwa Mbwana Samatta ambaye alikuwa nyota wa Ligi Kuu ya Ubelgiji akitamba katika klabu ya KRC Genk.

Tanzania Sports
Theo Walcott, aliwafungia Everton goli la jioni kabisa

Lakini kabla ya kuelekeza akili zake huko, mwaka mmoja kabla Aston Villa ilikuwa inamtegemea kinda wa Chelsea, Tammy Abraham ambaye alikwenda kucheza klabuni hapo kwa mkopo. Tammy akafunga mabao 26.

Mchango wa Tammy ndio uliwezesha Aston Villa kupanda hadi Ligi Kuu England kutoka daraja la kwanza. Lakini jambo la kusikitisha zaidi kwamba mara baada ya mchezo wao wa kuamua nani afuzu kutinga Ligi Kuu ndio ilikuwa siku ya mwisho ambayo Tammy kuichezea Villa, naye akaamua kula bata la kuagana na Villa huo Los Angeles.

Kusherekea mafanikio katika umri wake mdogo kuiwezesha Villa kupanda daraja. Hii ilikuwa na maana Villa wangekosa huduma ya mshambuliaji huyo, kwani alitakiwa kurudi Chelsea.  

Nyota huyo aliombwa kubaki Villa kwa msimu wa 2019/2020, lakini moyo wake ulishaondoka klabu hapo na akili ikishatangulia kwenye viwanja vya Chelsea akitarajia kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza.

Hilo ni jambo moja. Lakini jambo lingine lililowakwamisha Villa kumbakiza Tammy lilikuwa ni pesa. Villa hawakuwa na uwezo wa kulipa ada ya pauni milioni 50 kwa Chelsea. Ilibidi Villa wacheze kamari kuwa ni heri kiasi hicho kutumia kuwanunua washambualiji wengine wenye uzoefu nje au ndani ya England.

Hapo ndipo ‘maarifa ya kamari’ ya Dean Smith na mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Jesus Garcia Pitarch walianza kusaka suluhisho. Walijua bila kupata mshambuliaji wa kuziba pengo la Tammy ni balaa.

Tena lingekuwa balaa ambalo liliwahakikishia kukosa mabao 20 kwa msimu au 26 kama alivyofanya Tammy. Ilibidi wafikiri zaidi nani anaweza kuingia kikosini mwao na kuwaletea mabao 20, tena Ligi Kuu sio daraja la kwanza. Hapo ndipo mzizi wa Aston Villa kuwa na hali waliyonayo leo ulipoanzia.

Kwa vile walijua Tammy hawezi kubaki Villa, hapo ndipo walipata nafasi ya kumsajili Neal Maupay ambaye alijiunga Brighton & Hove Albion kutoka Brentford kwa pauni milioni 20.

Habari ikageukia kwa Wesley Moraes ambaye alinunuliwa kwa pauni miliini 22 na Kelechi Iheanacho. Baada ya kumnasa Moraes, kocha Dean Smith alitetea bei yake na kudai si mchezaji wa kubeza kwani anayo hazina ya mabao 12,13 au 14 Ligi Kuu.

Ndoto za wachezaji hukatishwa na majeraha. Mipango ya makocha huyumbishwa na mchezaji muhimu ambaye hulazimika kukaa benchi kutokana na kuumia. Hapo ndipo mambo yalipoanza kumchachia Dean Smith.

Villa wakalazimika kuingia sokoni kutafuta suluhisho la muda mfupi. Majina mawili yakawasili Aston Villa; Mbwana Samatta na Keinan Davis ambapo hadi sasa wamefunga bao katika mechi za Ligi Kuu. Washambuliaji hao wangekuwa wamepachika mabao ya kutosha bila shaka wangeokoa hali ya Villa katika hatari ya kushuka daraja.

Kushindwa kumbakiza Tammy klabu hapo, ni kama vile kulitengeneza jinamizi linalowasumbua sasa. Villa walikumbwa na  mkanganyiko mkubwa kwenye dirisha kubwa na dogo la usajili.

Maumivu ya Aston Villa

Hadi sasa hawana uhakika wa mabao kutoka kwa Maupay wala Benrahma, na hata Iheanacho hajapata nafasi ya kutosha kucheza kama alivyoahidiwa. Kwenye dirisha dogo la usajili waliwakosa washambuliaji Olivier Giroud, Michy Batshuayi na Islam Slimani kwa lengo la kuwa washindani wa Samatta na Davis. Villa walimnunua Samatta kwa pauni milioni 8.5 tu.

Dean Smith anaweza kujutia uamuzi wa kuwatosa Callum Robinson na Jay Rodriguez. Robinson ni mchezaji wa Villa aliyetoka akademi yao sambamba na kapteni wao Jack Grealish. Kimahesabu Robinson hakuwa kwenye mipango ya kocha wa Villa hivyo akaenda zake West Bromwich Albion.

Kwa upande wa Jay Rodriguez, Villa walihitaji mchezaji mwenye uzoefu na Ligi Kuu England. Lakini sasa Jay Rodriguez ni mshambuliaji wa Burnley ambaye katika mechi tano za awali alifunga mabao matatu. Tangu hapo amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Sean Dyche. Amepachika mabao 11 msimu huu na kushiriki mengine 10.

Samatta alisajiliwa kuwa mbadala wa mshambulaji wao Davis ambaye alikuwa ameumua. Hapo hapo Villa walimpoteza mchezaji wao muhimu Jonathan Kodjia aliyejiunga na Al-Gharafa ya Qatar. Ujio wa Borja Baston kutoka Swansea City uliongeza idadi bila mafanikio. Haikujulikana Villa walitaka kwenda wapi kwani nyota huyo alicheza dakika 14 tu, kisha Juni 30 mwaka huu wakaamua kumtema kikosini mwao.

Katika maizngira hayo unaona Villa walijiweka katika nafasi ngumu. Maarifa ya kamari ya Dean Smith hayajafanya kazi. Walihitaji mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumbukiza mabao wavuni, lakini mabao yamekataa. Ukame umewanasa na kushikilia miguu ya washambuliaji wao.

Kocha wao naye amekuwa kwenye maumivu makali ya kifua. Kama kichwa kimeuma mno, na kifuani sasa ni kama presha imemshika. Magoli hayafungwi. Washambuliaji wake hawana maarifa zaidi. Timu ipo kwenye janga la kushuka daraja. Aston Villa wanahitaji ushindi wa pointi 6 katika mechi mbili ili kubaki Ligi Kuu England.

Kamera za TV zinapomwonesha Deam Smith akiongoza timu yake ni wazi ana maumivu makali mno. Timu haifanyi vizuri. Washambuliaji hawafumanii nyavu. Mbaya zaidi Samatta ni mchezaji mpya aliyeingia katika timu mpya. Mbinu mpya. Wachezaji wapya wenye ujuzi tofauti na alikotoka KRC Genk.

Uzalishaji wa eneo la kiungo ni hafifu. Nahodha wake Jack Grealish amekuwa mwingi wa kuharibu muvu za mchezo. Nafasi za mabao 357 zimetengenezwa lakini mabao hayaingia wavuni. Kwahiyo Villa wanalo tatizo kubwa la kutatua katika timu yao. Mahali pa kuanzia ni benchi la ufundi kisha kikosi chao.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Zinedine Zidane

Real Madrid Mabingwa

Giroud

Mechi hizi za ‘kuwachinja’ Lampard na Solskjaer