in , , ,

HAYA NDIYO MATATIZO YA CHELSEA

 

 

Mambo si mazuri Stamford Bridge. Karibu kila mshabiki wa soka anajua kipindi kigumu walicho nacho Chelsea kwa sasa. Ni kigumu zaidi kwa Jose Mourinho kuliko mtu mwingine yeyote mwenye uhusiano wowote na klabu ya Chelsea.

Wakiwa wameshacheza michezo 11 kwenye EPL mabingwa hao watetezi wameshinda michezo mitatu pekee. Wamepokea vipigo sita kutoka kwa Manchester City, Crystal Palace, Everton, Southampton, West Ham na Liverpool. Matokeo hayo mabovu yamewafanya kuwepo kwenye nafasi ya 15 kwenye msimamo wakiwa na alama 11.

Msimu uliopita baada ya michezo 11 ya kwanza Chelsea walikuwa hawashikiki. Walikuwa kileleni mwa msimamo wa EPL wakiwa na alama 7 zaidi ya Manchester City waliokuwa kwenye nafasi ya pili. Walikuwa wameshinda michezo 9 kati ya hiyo 11 ya kwanza na kutoa sare miwili pekee dhidi ya Manchester City na Manchester United.

Walikuwa wameshafunga jumla ya magoli 28 na kuruhusu 11 pekee. Msimu huu hali ni tofauti kabisa. Kwenye michezo 11 ambayo Chelsea wameshacheza mbaka sasa wamefunga mabao 16 na kuruhusu 22 ambayo ni mara mbili zaidi ya waliyokuwa wameruhusu kwenye msimu uliopita baada ya michezo 11 ya kwanza.

Hali hii imefanya mashaka ya kuwa Mourinho anaweza kutimuliwa kuongezeka hasa baada ya kupokea kipigo cha 3-1 kutoka kwa Liverpool wiki iliyopita. Hali ni mbaya na imemuharibu mno kisaikolojia Jose Mourinho na wachezaji wa Chelsea.

Hata wanapocheza dhidi ya timu zisizo tishio mara nyingi wanakuwa kwenye hali ya kutojiamini. Hili huwa linawapelekea kupata matokeo mabaya mara kwa mara. Najaribu kujiuliza ni kipi kilichowafanya Chelsea kufika hapa walipofika?

Wapo wanaosema kuwa kushuka kiwango kwa wachezaji muhimu wa Chelsea ambao walikuwa tishio kwenye msimu uliopita ndiko kunakowafanya Chelsea kuonyesha udhaifu endelevu. Mara nyingi Eden Hazard ndiye anayetajwa kama mfano kwenye madai ya namna hii.

 

Advertisement
Advertisement

Hazard si tishio tena kwa sasa. Silaha yake kubwa ya uwezo wa kukokota mpira na kuwatambuka walinzi imekuwa butu na haifanyi kazi msimu huu. Hata anapokabiliwa na mlinzi mmoja pekee huwa anadhibitiwa mara moja na kunyang’anywa mpira.

Si Hazard yule aliyekuwa akikusanya walinzi watatu mbaka wanne na kuwaondoka kisha akafunga ama kutengeneza bao ama akasababisha kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari na kuzawadiwa mkwaju wa penati ambao angeuweka wavuni yeye mwenyewe.

Ukiacha hilo la kushuka kwa kiwango cha Eden Hazard nafikiri tatizo la ulinzi ndiyo tatizo kubwa zaidi lililowafanya kuwa kwenye nafasi mbaya ya msimamo wa EPL kwa sasa. Kwenye hili watatajwa Branislav Ivanovic, John Terry, Nemanja Matic na wengine walioifanya Chelsea kuwa imara kwenye swala la ulinzi msimu uliopita.

Msimu huu Chelsea wamerushusu mabao 22 kwenye michezo 11 wakati msimu uliopita walikuwa wameruhusu mabao 11 kwenye idadi kama hiyo ya michezo ya mwanzo. Hii ni ishara kubwa ya kuyumba kupita kiasi kwa safu ya ulinzi ya Chelsea.

Ulinzi imara ndio uliowafanya Chelsea kutwaa taji la EPL msimu uliopita. Waliruhusu mabao 32 ambayo yalikuwa machache kuliko timu yoyote kwenye michezo yote 38 ya EPL. Hawakuwa vizuri kwenye ushambuliaji ambapo walifunga mabao 73 pekee wakati Manchester City walifunga 83.

Haya ndiyo matatizo ya Chelsea msimu huu. Yanatokana zaidi na kuyumba kwa safu yao ya ulinzi. Huenda Mourinho ndiye meneja sahihi wa kuirudisha timu hii kwenye ubora wake kama anavyojinadi yeye mwenyewe. Tususbiri tuone itakavyokuwa mbeleni.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal hali mbaya

Tanzania Sports

ARSENAL v. TOTTENHAM