*Wawapisha Ghana na Mali kwa nusu fainali
*Newcastle wawafunga Chelsea, Arsenal safi
*Man United watanua uongozi kwa pointi 10
Vilio vimewatawala wenyeji Afrika Kusini, baada ya Bafana Bafana kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Wenyeji hao walionesha udhaifu kwenye upigaji mikwaju ya penati dhidi ya Mali, baada ya dakika 120 kumalizika kwa bao 1-1.
Mbele ya Rais Jacob Zuma, Afrika Kusini walishindwa kulinda bao la dakika ya 31 la Tokelo Rantie aliyepokea majalo ya Thuso Phala.
Mali waliofuzu nusu fainali kwa mara ya pili mfululizo, walisawazisha bao kupitia kwa nahodha Seydou Keita dakika ya 58.
Bafana Bafana walikosa penati tatu, huku golikipa wao, Itumeleng Khune akishindwa kuzuia hata moja ya wapinzani wao.
Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali, Ghana waliwafunga Cape Verde 2-0 na kutinga nusu fainali kilaini ndani ya dakika 90 za mchezo.
Black Star walipata mabao yote kupitia kwa Mubarak Wakaso aliyeanza kwa kufunga penati tata baada ya nahodha Asamoah Gyan kuangushwa eneo la hatari.
Kocha wa Cape Verde, Luis Antunes hakuridhishwa na uamuzi wa mchezo huo, akisema kwamba timu bora imetolewa na watu watakosa kuuona mng’ao wake.
Katika Ligi Kuu ya England (EPL), jahazi la matajiri wa London, Chelsea lilizamia St. James’ Park, baada ya Newcastle kuwalaza mabao 3-2 na kuacha maswali kwa kocha Rafa Benitez.
Moussa Sissoko aliyesajiliwa Januari hii alifunga mabao mawili baada ya mwenzake Jonas Gutierrez kutangulia kufunga moja.
Chelsea walipata mabao yao kupitia kwa Frank Lampard na Juan Mata. Ilikuwa siku mbaya kwa Demba Ba aliyehamia Chelsea kutoka Newcastle, ambapo hakufurukuta uwanjani. Chelsea wapo nafasi ya tatu kwa pointi 46.
Katika mechi nyingine, Arsenal waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stoke City katika uwanja wa Emirates, baada ya Stoke kucheza kwa kujihami muda mrefu wa mchezo.
Lukas Podolski aliyeingia badala ya Alex Oxlade-Chamberlain alifunga bao hilo dakika ya 78, huku Gunners wakiutawala mchezo kwa asilimia 70.
Mlinzi mpya wa kushoto, Nacho Monreal alianza vyema kazi Emirates, kuchukua nafasi ya Kieran Gibbs aliyeumia na atakayekuwa nje ya dimba kwa wiki sita. Arsenal wanabaki nafasi ya sita kwa pointi 41 na Stoke ni wa 10 kwa pointi 30.
Manchester United wameongeza pengo kileleni kwa pointi 10 mbele ya majirani zao, Manchester City.
Bao pekee la Wayne Rooney katika dakika ya 79 lilitosha kumpa usiku mzuri Alex Ferguson, kwa kufikisha pointi 62.
Kwa muda United walishika uongozi kwa tofauti ya pointi saba, kabla ya kupunguzwa, ikazirejea tena na sasa imefikisha 10, lakini uendelevu wake utategemea mechi ya Manchester City dhidi ya Liverpool kesho.
Everton waliepuka kichapo nyumbani kwa Aston Villa, baada ya mchezaji wake, Marouane Fellaini kufunga mabao mawili, moja dakika ya mwisho ya mchezo na kuiokoa timu iliyokuwa nyuma kwa mabao 3-1.
Villa walishaanza kushangilia ushindi wa kwanza wa ligi kwa mwaka huu, hivyo kubaki nafasi ya 19 kwa pointi 21 wakati Everton wakiwa ya tano na pointi 42.
Reading wameendelea kufanya vyema kwenye ligi, wakishika nafasi ya 17 kwa pointi 23 baada ya kuwafunga Sunderland mabao 2-1. Sunderland ni wa 13 wakiwa na pointi 29.
Mchezaji wake wa Mali, Jimmy Kebe alifunga mabao yote huku lile la Sunderland likiwa la penati iliyopigwa na Craig Gardner.
West Ham United waliokuwa nyumbani Upton Park waliibuka na kupata ushindi kwa bao pekee la Andy Carroll dhidi ya Swansea City. West Ham wamefikisha pointi 30 wakiwa nafasi ya 11 huku Swansea wakibaki ya nane kwa pointi 34.
Queen Park Rangers (QPR) walikosa bahati ya ushindi baada ya Adel Taarabt aliyeng’ara kwa ushambuliaji kukosa penati dhidi ya Norwich na mchezo kuisha kwa suluhu.
Golikipa wa Norwich, Mark Bunn alimwangusha Jamie Mackie, lakini akasahihisha makosa kwa kuuokoa mkwaju wake kiustadi. QPR wamebaki mkiani kwa pointi 17 wakati Norwich ni wa 14 baada ya kujikusanyia pointi 28.
Wanyonge wengine, Wigan waligawana pointi na Southampton baada ya kuchomoa bao dakika ya mwisho na kwenda sare ya mabao 2-2. Kwa sare hiyo, Wigan ni wa tatu kutoka mkiani wakiwa na pointi 21 wakati Southampton ni wa 16 kwa pointi 24.
Kivumbi kingine ni Jumapili hii pale Manchester City wasiokuwa na Mario Balotelli watakapowakaribisha Liverpool wakati Tottenham Hotspurs wanawaalika West Bromwich Albion waliomwengua kwenye msafara mpachika mabao mtata, Peter Odemwingie.
Comments
Loading…