in , , ,

Pauni milioni 120 zatumika usajili

Pauni milioni 120 zatumika usajili

*Samba, Balotelli na Monreal ndio ghali zaidi

*QPR, Newcastle na Liverpool wachangamka

Klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zimetumia pauni milioni 120 kununua wachezaji katika usajili wa dirisha dogo.

Siku ya mwisho ya usajili, Januari 31, ilikuwa na pilika nyingi, ambapo licha ya kwamba hakuwa akicheza EPL, David Beckham alifunika habari kwa usajili wa bure Paris St-Germain.

Mtoto mtukutu wa Kitaliano, Mario Balotelli hatimaye ameiacha Manchester City, na tayari kocha Roberto Mancini analalamika kumkosa, baada ya kumuuza kwa pauni milioni 19 kwa AC Milan ya kwao Italia.

Tajiri wa Queen Park Rangers (QPR), Mmalaysia Tony Fernandes ameshitua wengi kwa kumkubalia kocha Harry Redknapp kumnunua beki Christopher Samba wa Anzhi Makhachkala ya Urusi kwa pauni milioni 12.5.

Arsene Wenger, baada ya kutoonesha kutaka kununua mchezaji, alimnunua beki na kiungo wa kushoto Nacho Monreal wa Malaga kwa pauni milioni 10, baada ya kuumia kwa tegemeo la Arsenal, Kieran Gibbs.

Wachambuzi wa masuala ya michezo wanadhani Wenger alitakiwa kusajili zaidi, hasa kutokana na udhaifu wa timu yake inayoshindwa kuingia kwenye eneo ililozoea la nne bora katika msimamo wa ligi, hivyo kujihatarisha kukosa ligi ya mabingwa Ulaya msimu ujao.

Uhamisho mwingine mkubwa EPL ni wa Danny Graham aliyekuwa mfungaji bora wa Swansea msimu uliopita, ambaye safari hii alipigwa kumbo na Michu. Amehamia Sunderland kwa ada ya pauni milioni tano.

Zile tetesi za fulani anahamia klabu hii au wengine wanauzwa sasa zitatulia kidogo hadi mwisho wa ligi, japokuwa tayari taarifa zinasambaa za Manchester City kutenga pauni milioni 40 kumchukua Luis Suarez Liverpool.

Suarez amepunguziwa mzigo wa utegemezi wa kufunga, baada ya kocha Brendan Rodgers kufanikisha usajili wa Daniel Sturridge kutoka Chelsea kwa pauni milioni 12 na Mbrazili Philippe Coutinho kutoka Inter Milan kwa pauni milioni 8.5.

Newcastle United ndiyo klabu iliyolitawala zaidi dirisha la usajili, kwa kuchukua wachezaji watano wa Kifaransa ili kujinusuru na hatari ya kushuka daraja baada ya kuondokewa na mfungaji wao, Demba Ba aliyehamia Chelsea.

Kocha Alan Pardew aliyekuwa kwenye msukosuko kwa kupoteza mechi mfululizo, ikiwa ni pamoja na kufungwa mabao 7-3 na Arsenal, aliomba fedha na kupewa, hivyo akakimbilia kwa Wafaransa.

Wachezaji aliosajili ni mabeki Mathieu Debuchy, Mapou Yanga-Mbiwa. Mshambuliaji Yoan Gouffran na kiungo Moussa Sissoko. Yupo pia Massadio Haïdara, wote wakiungana na Wafaransa wengine sita waliotangulia, hivyo Kifaransa kinapigwa sana pale St. James’ Park.

Redknapp mbali na kumchukua Samba, amekamilisha usajili wa Loic Remy, Jermaine Jenas, Andros Townsend na Tal Ben Haim.

Kama ilivyotarajiwa, Tottenham Hotspurs wamefanya vyema kwenye usajili huu, chini ya mwenyekiti wao, Daniel Levy.

Amefanikiwa kumpatia kocha Andre Villas-Boas mchezaji muhimu kama Ezekiel Fryers akimpiga kumbo kocha Alex Ferguson wa Manchester United aliyelia kuingizwa mjini.

Levy pia alicheza pele kwa kufanikiwa kumnasa mchezaji muhimu na chipukizi anayefaa kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lewis Holtby, tena kwa bei rahisi, huku akimchukua mapema Januari badala ya mwisho wa msimu ilivyokubaliwa awali. Fryers na Holtby wamemgharimu pauni milioni mbili tu.

Mambo haya huwa hayakosi vituko, ambapo usiku wa Januari 31, Peter Odemwingie wa West Bromwich Albion alikwenda QPR kusaini na kuchukua vipimo vya afya, kumbe hapakuwa na makubaliano yoyote, akarudishiwa getini.

Odemwingie amerudi West Brom ambako alifanya kikao na wakubwa wake, akatakiwa akapumzike nyumbani hadi Jumatatu, na anatakiwa kuomba radhi au kukabiliana na faini.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa Nigeria mwenye umri wa miaka 31, anasema lazima ataondoka West Brom, ni suala la muda tu, japokuwa mkataba wake unaonesha kwamba bado ana miezi 18 hapo Hawthorns.

Manchester United walishasema hawakuwa wanahitaji mchezaji kutokana na kusheheni vipaji na kuongoza ligi vizuri, lakini wamemsajili Wilfred Zaha wa Crystal Palace na kumwacha huko kwa mkopo hadi majira ya kiangazi.

Hilo ni pigo kwa mchezaji wao wa Kireno, Luis Carlos Nani, anayechezea nafasi hiyo hiyo na ambaye Ferguson anaelekea kutompa nafasi sana msimu huu, lakini pia hataki kumuuza.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Bafana Bafana nje AFCON

KUNA UMUHIMU WA KUWA NA SHINETA BADALA YA CHANETA