Kusema hivi si kumsifia pekee bali uwajibikaji wake uwanjani ndicho kitu cha kuzingatia. Mashabiki wa Yanga watakuwa mashahidi wa hili….
KWANZA ni kijana mtanashati. Mpira anaujua. Ni kiungo halisi wa ukabaji, mbabe dimbani, anapiga pasi za kwenda mbele, anafanya ‘tackling’ za kutosha. Haijalishi anacheza na nani, iwe Khalid Aucho, Salum Abubakr au Yannick Bangala. Lakini Zawadi mauya anabaki kuwa kiungo mkabaji ambaye anaweza kucheza katika timu yoyote hapa Afrika mashariki. ni mchezaji ambaye hsukiii akilalamika kuwekwa benchi, kwa vile anajua waliopangwa ni wachezaji mahiri.
Kila anapokuwa na mpira ni kiungo ambaye anajua thamani kutoa pasi haraka. Ni kiungo ambaye anaweza kukabiliana na washambuliaji wowote wale. Anajua kucheza kibabe,kistaarabu na zaidi anaisukuma timu kwenda mbele. Mara nyingi uchezaji wake utamwona anavuka eneo la katikati ya uwanja akitafuta namna ya kupika pasi za mabao na kutafuta ubunifu wa namna timu inaweza kupenya ngome ya adui. Amefanya hivi mara nyingi na mashabiki wameona.
Makocha wake Nasredine Nabi, Cedric Kaze wamekuwa wakimtumia kama mpango wa pili kuimarisha safu ya kiungo katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu au mashindano yaliyopita. Kiujumla msimu ulioishia hivi karibuni unaonesha kabisa Zawadi Mauya ni dhahabu iliyopo Yanga na inaweza kupata nafasi hata kwenye kikosi cha USM Alger au Waydad Casablanca na pale Al Hilal.
Kusema hivi si kumsifia pekee bali uwajibikaji wake uwanjani ndicho kitu cha kuzingatia. Mashabiki wa Yanga watakuwa mashahidi wa hili. Zawadi Mauya anaweza kucheza kama kiungo mkabaji peke yake. Anaweza kucheza kwa kombinenga ya ‘Double pivot’ akiwa na Khalid Aucho na Bangala hawa wote wanaweza kutumika pale kocha anapotaka kujilinda zaidi na kuwanyima wapinzani wao nafasi ya kugusa nyavu za Yanga. Sijui kocha mpya Miguel Gamondi anafikiria nini kuhusu kipaji hiki, lakini uwepo wake Yanga ni mchango mkubwa sana.
Hata hivyo lipo jambo ambalo linatatiza kwa namna fulani. Yanga wanahusishwa na suajili wa kiungo mkabaji Jonas Mkude aliyetemwa Simba. Mkude ameichezea Simba kwa kipindi cha miaka 10, lakini sasa amefika tamati na ameondolewa kikosini. Lakini Yanga wanadaiwa kuzungumza na nyota huyo. Lengo hapa si kubeza uwezo wa Jonas Mkude au uamuzi wowote mzuri wa viongozi wa Yanga wanaotaka kumsajili kiungo huyo.
TANZANIASPORTS imeambiwa kuwa usajili wa Jonas Mkude kwa Yanga utakamilika kwa neno la mwisho la kocha wao mpya Miguel Gamondi. Lakini swali linalokuja hapa, Yanga wanataka kumtumia Jonas Mkude katika mfupi upo? Na je nafasi ya kiungo ni sehemu iliyokuwa na matatizo msimu uliopita?
Tuangalie eneo lenyewe, kuna Khalid Aucho, Yannick Bangala, Mudathir Yahya na Zawadi Mauya. Aliyekuwa kocha wa Yanga Nabi alikuwa anampanga Ucho na Bangala katika eneo la kiungo mkabaji na ufanisi ulikuwa mkubwa na mzuri. Mabadiliko kadhaa yalikuwa yamweka benchi Bangala au Aucho kadiri benchi la ufundi lilivyoona na kumpanga Salum Abubakar.
Lakini mbele ya Bangala na Aucho alikuwa akipangwa Mudathir Yahya. Hii ina maana alikuwa analindwa na viungo watu katika mfumo wa 3-2-4-1 (hata -3-4-3), kwamba mabeki watatu, viungo wawili wakabaji, na viungo washambuliaji wawili (Mudathir na Kennedy Musonda) kisha mshambuliaji alikuwa Mayele na mawinga winga mmoja upande wa kulia.
Kwe mchezo wa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho, kocha Nabi alifanya mabadiliko kwa kumweka benchi Yannick Bangala na kumpa nafasi Salum Abubakar kucheza na Mudathir Yahya katika eneo la kiungo. Ingawa unaweza kusema Zawadi Mauya hata mbele ya Salum Abubakar hakutoboa lakini ukweli unabaki ndiye kiungo mbadala anayeingia kuimarisha na uchangmsha eneo la kiungo mkabaji na ushambuliaji.
Kwa kimombo husemwa ‘fresh legs’ ama tusemavyo uswhaili miguu mipya ambayo ni kama nguvu mpya inayoingizwa kwenye timu. Sasa iwapo Yanga wanaelekea kumsajili Jonas Mkude, swali moja linaibuka wanataka kumfanya nini Zawadi Mauya? Ni namna gani kipaji hiki kinaweza kupiga hatua baada ya uzoefu mkubwa mbele ya wachezaji wa kigeni?
Ifahamike sipendelei uzawa wake bali ushindani wake. Vilevile haionekani kama Yanga walihitaji mchezaji wa eneo la kiungo mkabaji au mshambuliaji. Ningeulizwa na viongozi wa Yanga, ningewaambia waimarishe eneo la mawinga na kuingiza mmoja au wawili kwa sababu Dickson Ambundo na Tuisila Kisinda wanaondoka klabuni, kwahiyo kuna nafasi katika eneo hili.
Ili kujiimarisha Yanga walipaswa kuongeza mchezaji eneo hilo na kuifanya safu ya kiungo iendelee kubaki kama ilivyo kwakuwa ndiyo msingi uliowafikisha kwenye mafanikio licha ya kukosa kombe. Yanga hii haikuhitaji mchezaji wa kuchukua nafasi ya Khalid Aucho kwa sababu yumo ndani ya kikosi chao. Ni Zawadi Mauya.
Hili ni jambo rahisi na linaonekana wazi wazi kiufundi, na hata kocha mpya huenda akapata mtihani wa kuamua juu ya hatima ya Jonas Mkude kumsajili au kumkata, na namna ya kumtumia Zawadi Mauya ambaye amepata uzoefu kwa kuingia kwenye mpango wa Yanga na kuwa sehemu ya kombinesheni ya kiungo. Sijui Yanga wanatakaje hawa watani wetu.!
Comments
Loading…