in

Carlinhos ni kama mwalimu wa zamu

Carlinhos

MTANANGE wa Ligi kuu Tanzania Bara kati ya vigogo Yanga na Mtibwa Sugar limerejesha mjadala wa namna ya uchezaji wa Carlos Carmo maarufu kwa jina la Calinhos raia wa Angola. Uchezaji wake umesisimua wengi kutokana na matukio yake kusaidia klabu hiyo ya jangwani kuibuka na pointi kwenye michezo anayocheza.

Kiungo huyo hakuonekana uwanjani kwa muda mrefu, kwa sababu kubwa moja rasmi iliyotolewa kwa wadau w a soka; alikuwa majeruhi. Kwamba majeraha ndiyo yalisababisha akae nje kujiuguza kabla ya kurejea uwanjani.

Tanzaniasports pia inafahamu kuwa Calinhos alipewa mpango maalumu wa kujijenga kimwili na kurudisha utimamu pamoja na kuongeza misuli yake. Tangu ujio wa kocha Cedric Kaze alitoa tathmini kuwa nyota huyo ajiimarishe zaidi kwa kuongeza misuli. Hivyo basi pamoja na kuwa majeruhi bado Calinhos alikuwa kwenye mpango maalumu wa kujenga afya yake.

Lakini sasa  taratibu ameanza kurejea katika hali ya kawaida. Mwonekano wake wa sasa ameongezeka misuli, yuko tofauti kimwili kulinganisha na kipindi alipokuwa anatua Yanga kutoka kutoka kwao Angola.

Tukitazama mchezo wa Yanga na Mtibwa Sugar uliojaa kila aina ya presha kwa vijana wa mitaa ya Jangwani na Twiga, ilililazimu benchi la ufundi kuhakikisha wanatumia kila njia kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo. Ndipo Calinhos alipoingizwa uwanjani kuongeza maarifa ya ubunifu katika eneo lakiungo mshambuliaji.

Tanzania Sports
Yanga vs Azam FC

Kimsingi Calinhos ni kiungo wa pembeni kulia au kushoto, katikati na mshambuliaji wa pili. Wakati anaingia kipindi cha pili matokeo yalikuwa 0-0. Hapakuwa na dalili za kupachika mabao, Yanga walikosa nafasi nyingi kama ilivyo kwa Mtibwa. Washambuliaji wa Yanga Michael Sarpong na Deus Kaseke walishindwa kufurukuta mbele ya mabeki wa Mtibwa Sugar walioongozwa na mkongwe Dickson Daudi.

Calinhos anatumia akili sana uwanjani. Hatumii nguvu kubwa ila akili kubwa. Soka la kisasa linahitaji sana uchezaji wake. Hakai na mpira bila sababu. Akipata mpira mara moja anatoa pasi. Anabadili mwelekeo wa mashambulizi, mikato yake inaweza kwenda kulia au kushoto. Anapiga pasi ndefu na fupi za haraka zaidi. Anapishana na nguvu za mabeki au wapinzani wake uwanjani. Anaweka mpira kwenye njia na kuhakikisha unamfikia mlengwa hata kama yeye atakuwa amezuiwa.

Ushahidi wa chachu ya uchezaji wa kipekee wa Calinhos tunaupata kwenye bao  alilofunga. Unaweza kutazama  mara 3 au zaidi kuona namna alivyonyoosha mkono kuomba pasi kutoka kwa Tuisila Kisinda. Utaona namna makosa ya safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar kutegemea kukaba kwa ‘zonal marking’ na hivyo kujikuta wakielekeza nguvu na akili ulikokuwa mpira na kusababisha eneo lao la hatari kuwa wazi.  Wakati Calinhos anaingia eneo la hatari hakukuwa na kiungo wala beki wa Mtibwa Sugar ambaye angeweza kuona hatari ile na kujaribu kuzuia.

Calinhson alitumia akili kubwa mno na utulivu wake unamsaidia. Kipa alielekea kulia kwake, lakini Calinhos hakutumia nguvu sana akapiga kule alipotoka. Hapo ilikuwa ni kushindanisha nguvu na akili.

Calinhos ana maarifa makubwa kuliko nguvu kubwa. Calinhos anajua soka la kisasa. Anapokea na kutoa haraka sana. Kabla hajapata mpira anaonekana kimatendo anajua ataupeleka  wapi ukimfikia mlengwa. Anacheza kwa faida na malengo, tofauti na wachezaji wetu wazawa wanakaa na mpira, anapocheza hata kama hakukuwa na sababu.

Makosa mawili ya mabeki wa Mtibwa Sugar ni mawili, kuanzia kwa beki wa pembeni Hassan Kessy aliyetaka kumparamia Calinhos mara kwa mara, lakini wakaruhusu aingie kwenye eneo la hatari.

Tanzania Sports
VPL

Calinhos ukimfuata kwa nguvu kubwa anakupisha, anapitisha mpira katikati ya miguu ya beki na kumruka. Wanapania kumchezea faulo lakini anapitisha mpira kwenye njia, ukimzuia yeye, ujue mpira unaenda kwa mlengwa.

Niseme tu, Calinhos anatupatia elimu kubwa sana. Unaweza kudhani anacheza kwa dharau lakini anajua tuna wachezaji wengi wenye‘minguvu’ mingi mno dimbani kuliko maarifa.

Kuna muda nilijawa na hisia jinsi alivyodhalilisha nguvu za wenzake. Unamfuata kwa kasi na nguvu lakini yeye anachukua mpira tu, anakupisha na ‘minguvu’ yako. Hakika huyu ni mchezaji ambaye analeta darasa kubwa kwa viungo wetu oamoja na sokala Tanzania kwa ujumla wake.

Kiungo wa Mtibwa Sugar, Baraka Majogoro ana mwili unaofanana na Calinhos. Wote wembamba ambao wanatakiwa kujenga misuli miilini mwao. Angalau Calinhos ameanza na hilo anaelekea kufanikiwa. Naamini Majogoro naye anaweza kupata mtaalamu na akaongeza misuli kidogo.

Majogoro kwenye mashindano ya CHAN alikuwa anapenda kupimana ubavu na wapinzani wake na mara nyingi alijikuta akiangushwa. Hata hivyo Majogoro  anatakiwa kucheza kijanja kama Calinhos, kupishana na adui hivyo anapaswa kutumia maarifa makubwa ili kupunguza matumizi ya nguvu nyingi wakati mwili wake unafafana na Calinhos.

Vilevile Calinhos anatuletea hoja, ni namna gani viungo wetu Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Feisal Salum, je kanzu,tobo na  vyenga zinasaidia nini ikiwa timu haishindi? Zinasaidiaje timu kuondoka na pointi tatu? Kwanini kuwe na pasi za nyuma nyingi kuliko mbele?

Je, Feisal Salum na viungo wenzake tunaamini wana vipaji vikubwa na tegemeo la taifa hili, je wametengeneza mabao mangapi kwa msimu huu au misimu mitatu iliyopita? Kama hakuna basi ni changamoto yao, wanatakiwa kubadilika. Kama yapo basi iwe heri zaidi.

Calinhos ana wastani wa mzuri, mechi alizocheza ni 3, amefunga bao 3, mechi nyingine 3 ametokea benchi na katoa pasi za mwisho. Uchezaji wake umetawaliwa na maarifa kuliko kuchosha mwili.

Je, viungo wetu wshambuliaji wanajifunza nini kwa Calinhos? Je, wanayaona malengo yake kila mechi anayopewa kucheza? Simaanishi kila kiungo mshambuliaji awe anacheza kama Calinhos bali kuchota maarifa kucheza kwa malengo zaidi. Vipaji vyao vitumike kutengeneza nafasi za mabao,kufunga na kujiwekea takwimu muhimu zenye faida kwa timu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Lionel Messi

Barca wanatakiwa kusukwa upya

Mpambano wa nguvu

Al Ahly ni kibonde wa Simba