in , ,

Nyuma ya pazi Jonas Mkude na Yannick Bangala

KLABU inapofanya usajili wowote, kitu cha kwanza kinachoangaliwa ni kipaji cha mchezaji husika, pamoja na vitu vingine vya ziada ambavyo anaweza kuvileta kwenye kikosi chao. Kila mchezaji anacho kitu cha ziada anachoongeza kwenye timu. Inawezekana kitu hicho kikawa kwenye eneo analosajiliwa ili kuimarisha, lakini wengine wanakuwa wanaongeza vitu vya ziada kikosini ikiwemo hamasa. 

TANZANIASPORTS katika tathmini ya usajili imeambiwa na wataalamu kuwa wapo wachezaji wanaokataliwa kwa sababu wanaua ari ya timu (Mood killers). Wachezaji wa aina hii wanaogopwa kwa kile wanachodai wanapenda kuchochea au kuhamasisha wengine kukata tamaa au kukosa ari ya kupigania namba katika kikosi. Pia wanachangia kuharibika kwa ari ya mazoezi. 

Imeambiwa kwa mfano sakata la mkongwe Cristiano Ronaldo na Erik Ten Hag, moja ya matatizo makubwa yaliyovunja uhusiano ya wawili hao ni kuua ari ya wachezaji wengine katika timu. Kwamba Ronaldo alikuwa anachangia kiasi fulani kutokana na ushawishi aliua ari ya baadhi ya wachezaji. Katika hilo, si Ronaldo pekee yake bali kote duniani kuna wachezaji wanaochangia kuharibu utulivu wa timu. Kwahiyo usajili wowote lazima uangaliwe kwa makini juu ya mwenendo au tabia ya mchezaji. 

Unaweza kukuta mchezaji ana matatizo binafsi na uongozi, anataka wachezaji wengine nao wagombane na viongozi wao. Ugomvi wake unakuwa kama vile wa timu nzima, kila mahali anakuwa mwenye chokochoko. Lakini hilo linaonesha namna usajili wake ulivyokosa umakini kujua nyendo zake ndani na nje ya uwanja. 

Klabu ya Yanga imemsajili Jonas Mkude kama mchezaji huru. Nyota huyo alikuwa amedumu kwa miaka 13 katika kikosi cha Simba kabla ya kutupiwa virago. Wakati Jonas Mkude akisajiliwa Yanga mjadala ulikuwa mkubwa juu ya nafasi ya kiungo. Eneo la kiungo mkabaji lilikuwa na Zawadi Mauya, Khalid Aucho, Salum Abubakar, Mudathir Yahya na Yannick Bangala. Hata hivyo sasa imejulikana kuwa Yannick Bangala hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwa msimu 2023/2024. Je kuna tofauti ipi kati ya wachezaji hawa wawili wa kiungo?

YANNICK BANGALA

Zipo tetesi kuwa Yannick Bangala alikuwa miongoni mwa wachezaji wanaoua ari ya timu (Mood Killers) lakini uongozi wa Yanga hawakuwahi kuzungumzia jambo hilo hadharani. Huenda zinabaki kuwa tetesi lakini hatua ya kuuzwa Yannick Bangala kwenda kwa Mabwanyenye wa Azam Fc, ni dhahiri tathmini ya uongozi kwa mchezaji (overall) imefika mahali ikaona ni jambo la heri kuachana na nyota huyo. Matatizo ya Yannick Bangala hayakujulikana kabisa, lakini pengine viongozi wanaweza kupewa kura ya imani kuwa waliamua kumuuza nyota wao. 

Pili, Yannick Bangala ni mchezaji mwenye sifa nyingi katika kikosi. Kama unataka kumsajili kwa kuangalia sifa za uwanjani unaweza kuweka fedha nyingi ili umvute kwenye kikosi chako. Bangala anao uwezo mkubwa wa kutawala eneo la kiungo. Anaweza kuzuia mipango ya adui,kukokota mpira, kukaba kwenda kulia na kushoto. Tatizo pekee kwa mtindo huu Bangala hakuwa kiungo wa kupanda kupitia katikati kwa maana ya kupasua eneo la adui. Kazi hiyo aliifanya zaidi Khalid Aucho. 

Tanzania Sports

Sifa nyingine ya Yannick Bangala akiwa kwenye kikosi chako ni kucheza kwa umakini dakika 90 zote. Ni mara chache hufanya makosa kiwanjani. Vilevile sifa kubwa ambayo inamtofautisha na Jonas Mkude ni uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati. Bangala kwa hili anamzidi kwa mbali sana Mkude. Uwezo wa kucheza nafasi nyingi ndiyo sifa ambayo inawavutia makocha wengi kufanya kazi na Yannick Bangala. 

Ni mchezaji ambaye kwa namna fulani hata akipangwa beki wa kulia anaweza kucheza kwa ufanisi. Ni aina ya mchezaji ambaye kila mwalimu anatamani kuwa naye. Ni kama vile Dickson Job anavyomudu kucheza nafasi zote za beki, kati, kulia na kushoto pamoja na kiungo mkabaji. Sifa hii Jonas Mkude hana kabisa.

JONAS MKUDE

Nyota huyu na Yannick Bangala wanakutana katika eneo moja tu; kwenye kuua ari ya timu (Mood Killers). Mara kadhaa akiwa Simba, uongozi ulilazimika kumwondoa kikosini kwa madai ya utovu wa nidhamu. Jambo hili limekuwa likiathiri kipaji cha Jonas Mkude. haijulikani ikiwa anao washauri wa mpira na saikolojia kwa ajili ya kuboresha kazi yake. 

Hata hivyo anabaki kuwa mchezaji mwenye kipaji kizuri katika soka. Ni aina ya wachezaji wanaocheza kwa nguvu moja dakika zote 90 za mchezo. Huwezi kumlalamikia kuwa amechoka au anazembea, labda ikiwa Kocha anatakiwa kufanya mabadiliko ya kimbinu. Udhaifu pekee ambao alikuwa nao siku za nyuma ni kupiga pasi nyingi zaidi eneo la nyuma badala ya kwenda mbele. 

Kwa misimu miwili hivi Jonas Mkude katika mechi chache alizocheza ameonesha kubadilika, anasogea mbele, hata faulo zake nyingi huzifanya akiwa kwenye nusu ya eneo la adui. Si Mkude Yule aliyekuwa anaishia kwenye mstari wa katikati ya kiwanja na kurudi nyuma. Marekebisho yake ya uchezaji bado hayajampatia nafasi ya kurudi Taifa Stars, ambako Mzamiru Yassin anakimbia kwenda mbele zaidi yake, na pasi zake huelekea eneo la adui zaidi. Hiki ndicho wanapenda makocha.

Mkude ni mchezaji wa kiungo mkabaji pekee. Hawezi kutumika katika eneo la kiungo mshambuliaji kama ilivyo kwa Salum Abubakar au Mudathir Yahya ambao wanatumikia nafasi zote mbili; kiungo mshambuliaji na kiungo mkabaji. Sifa hii Bangala anamzidi kwa mbali sana Jonas Mkude. angalau pia Jonas Mkude anamzidi Bangala pasi ndefu kuelekea langoni mwa adui. Mkude anazo pasi ndefu kama zile za Salum Abubakar kuelekea lango la adui. 

MMOJA ZAIDI KATIKA WAWILI

Hitimisho ni kwamba wachezaji hawa wawili wana tofautiana kwa kiasi kikubwa na wanazidiana maeneo fulani. Eneo la utimamu wa mwili Yannick Bangala ni kama chuma, ingawa pia Jona Mkude si mbaya kwenye hili lakini hajawa fiti kama Bangala. Uzuri wote wawili wanaweza kutumika katika kikosi kimoja bila bila kupishana ikiwa mwalimu atachagua mbinu sahihi kama ya kucheza na wakabaji wawili kwa sababu Bangala ni msahihishaji mkubwa wa makosa ya beki wa kati. Pia Bangala ana kasi zaidi kuliko kipaji cha Jonas Mkude.  

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
David raya

Mapengo mawili Arsenal

Tanzania Sports

Simba wamezindua, je watanguruma msimu huu?