in , , ,

KWANINI ANDRE ONANA ANAWINDWA NA MAN UNITED

ROME, ITALY - MAY 06: André Onana of FC Internazionale looks on during the Serie A match between AS Roma and FC Internazionale at Stadio Olimpico on May 6, 2023 in Rome, Italy. (Photo by Giuseppe Bellini/Getty Images)

Andre Onana anatarajiwa kuwa mchezaji wa kuimarisha kikosi na mfumo wa uchezaji wa Manchester United….

WAKATI mashabiki wa soka Afrika wakishuhudia golikipa mahiri toka Senegal, Eduardo Mendy akiondoka EPL baada ya kuachana na Chelsea sasa wanatarajia kuona kipaji kingine kutoka bara hilo kikitua klabu ya Manchester United. Si mwingine ni Andre Onana raia wa Cameroon. Nyota huyo amekuwa lulu barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichokionesha msimu ulioisha. Kiwango ambacho kimedhihirisha kipaji chake na kusababisha mabosi wa Manchester United kumtumia virago golikipa wao David De Gea. 

TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu ambayo yamechangia Nyota huyo wa Cameroon kuwa lulu. Takwimu zake zinasisimua na kumfanya kuwa golikipa wa kuigwa Kati ya wale wa kisasa waliopo kwenye vikosi vya timu mbalimbali. Akiwa na umri wa miaka 27 tu, nyota huyo ametengeneza jina lake kwa wino wa dhahabu. 

Man United wameandaa kitita cha pauni Milioni 43 kumsajili Andre Onana kutoka klabu ya Inter Milan. Usajili wa kipa huyo ni tumaini pekee la kocha Erik ten Hag kuimarisha ubora wa kikosi chake, na anafahamu uwezo mkubwa na kipaji cha nyanda huyo kwani wamewahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

Andre Onana anatarajiwa kuwa mchezaji wa kuimarisha kikosi na mfumo wa uchezaji wa Manchester United.

Onana anafahamika vizuri kwa Ten Hag kwakuwa walidumj kwa miaka minne na nusu katika klabu ya Ajax, lakini hatuwezi kusema uhusiano wao wa kikazi bora au sahihi kwa asilimia 100 Kati yao.

Hata hivyo Eric Ten Hag anataka huduma nzuri ya Onana kuwa mrithi wa David De Gea kama golikipa namba moja wa Manchester United.

Tanzania Sports

Kwa namna nyingi Onana ana staili yake ya kucheza inayovutia makocha kuliko David De Gea. Manchester United watanufaika na kipa huyo ambaye katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alionesha uwezo mkubwa na kwanini anastahili kuwa namba moja Inter Milan. Kwenye mchezo huo kuna wakati alikuwa karibu na mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland akamlamba chenga na kutoa pasi kwa mabeki wake. Mara nyingi alikuwa akituliza Mpira vizuri sana mguuni mwake bila.hofu huku akitoa pasi za uhakika kwa mabeki wake.

Tatizo lililomwondoa David De Gea aliyedumu miaka 12 ni uwezo mdogo wa kucheza kwa miguu. Ingawa De Gea ni kipa anayepangua michomo mingi inayolengwa golini mwake. Ni kweli kwamba ameiokoa Man United mara kadhaa kwa uhodari wake, lakini Andre Onana ana kitu ambacho David De Gea hana kabisa; kukokota mpira,kupiga pasi,kutokuwa mwoga, kucheza katika nafasi ya beki wa mwisho, kutumikia mfumo kama beki wa mwisho, na pia kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi ndefu kwenda kwa washambuliaji. Hayo ndiyo hufanywa Andre Onana lakini kwa David De Gea hakuweza kuyafanya hata robo tu. 

De Gea alifanya makosa makubwa katika mechi dhidi ya Brentford, West Ham na Sevilla, kabla ya kuhusika tena katika bao la ushindi la Ilkay Gundogan wa Manchester City katika mchezo wa Fainali ya FA. 

Jambo lingine liliomwangusha David De Gea ni utoaji wa uhakika wa pasi kwenda kwa walengwa. Hapa alikosa maarifa ambayo yangemwezesha kuifanya Man United iwe inaanzisha pasi nzuri toka langoni mwao. Mara kadhaa alitoa pasi vyongo kwenda kwa mabeki wake wakati timu ikiwa kwenye umiliki wa mpira.

Tukio la kukumbukwa ni kumpigia pasi mbovu beki wake Lisandro Martinez wakati Muargentina huyo alipokuwa anacheza.

Kwa Onana alionesha mbele ya Milioni ya watu kwenye fainali ya UEFA dhidi ya  Manchester City mwezi uliopita licha ya kufungwa 1-0, lakini ule uchezaji wake ulikuwa kivutio kwa wengi. Onana alituliza mipira kwa ustadi kila alipopigiwa pasi,alikotroo vizuri,akagawa pasi,akawapiga chenga washambuliaji wa Man City na kama hewani aliruka vizuri na kutawala eneo lale kwa kujiamini. Akapangua michomo ambayo ilionesha wazi kuwa inaingia wavuni, hasa mingine ya mita sita tu na Erling Haaland lakini akalinda lango lake vizuri.

Mashabiki wa Serie A wamezoea kufaidi ubora wa Andre Onana kila mechi ambako alikuwa anaacha gumzo kubwa. Katika mechi za Ligi Kuu msimu uliopita, Onana alipiga pasi fupi (za kawaida) 224 na asilimia 98 ya pasi za ndefu. 

Linapofika suala la kupiga mipira mirefu kwenda kwa washambuliaji wa Inter Milan, asilimia  54.7 iliwafikia walengwa.

Kwa ujumla Onana alihitimisha asilimia 81.3 ya pasi zake 1030 kwenda kwa wachezaji wenzake.  Kwa mtindo huo ikawa sababu ya kocha Simone Inzaghi kumweka benchi golikipa mkongwe wa Inter Milan, Samir Handanovic msimu uliopita. Onana alichukua jukumu la kulinda lango la Inter Milan kwa ustadi na alitumia vema mwanya wa kuwekwa benchi kwa Samir Handanovic.

Tukirudi kwa David De Gea msimu uliopita katika mechi 38 za EPL amefikisha asilimia 71.1 za utoaji wa pasi kwa usahihi. Asilimia 43.6 ni mipira mirefu kwenda kwa washambuliaji wa Man United. Kwahiyo utaona Onana amemwacha mbali sana David De Gea katika suala la ufanisi.

Hii Ina maana ikiwa Man United watampata kipa huyo wataongeza ufanisi katika utoaji wa pasi, kuanzisha mashambulizi na namna ya kutuliza presha toka kwa washambuliaji wa timu pinzani. Ten Hag anataka kipa wake awe na uwezo wa kuifanya timu yake kutawala mchezo ikianzia kwa golikipa.

Lakini United wanaweza kupata faida nyingine kwani Onana anao uwezo mkubwa wa kucheza eneo la mabeki wa kati akitokea golini bila hofu, na kuwa sehemu ya mfumo wa kuanzisha mashambulizi. Hili ndilo lilikosekana Man United.

Onana anao uwezo mkubwa wa kwenda mbele kwa yadi 10 hadi 20 toka golini kwake, na haogopi kuchukua uamuzi kama huo kwa sababu ana uwezo mkubwa wa matumizi ya miguu katika uchezaji wake kitu ambacho David De Gea hakuwa nacho.

Hivyo upo uwezekano Onana akaonesha hilo kwa kwenda mbele hadi eneo la kiungo huku akipigiana pasi na mabeki wake Lisandro Martinez na Raphael Varane, au kupigiana pasi na mabeki wa pembeni Luke Shaw au Aaron Wan-Bissaka ambao atawasaidia kushambulia zaidi.

Ikiwa mabeki hao watakuwa wamebanwa na wachezaji wa timu pinzani,  Onana anao uwezo wa kupiga mipira mirefu kwenda kwa washambuliaji  Marcus Rashford, Antony, Jadon Sancho au yeyote atakayepangwa.

Katika msimu wa  2022-23, Onana amecheza mechi  24 za Ligi Kuu Italia huku Samir Handanovic akicheza mechi 14. Onana ni kipa ambaye hana papara awapo langoni mwake.

Wakati wa Fainali za Kombe la Dunia, 

Onana alimtia hofu kocha wake kutokana na uchezaji wake wa kuondoka eneo lake yadi 10 hadi 20 kwenda eneo la kiungo.

Kuona hivyo Rigobert Songo akaamua kumwelekeza kupunguza au kuachana na mtindo wake wa uchezaji kuwa na mpira miguuni badala yake abakie golini. Hilo Onana hakukubaliana nalo, likawa Sababu ya kulumbana na Song ambaye aliamua kumtimua kambini. 

“Onana anafanya hayo mara nyingi mazoezini, lakini ana mambo yanayihatarisha timu wakati wa mechi. Nilimwambia apunguze kuhatarisha lango letu mara kwa mara, nilitaka asipige pasi kwenda eneo la katikati, badala yake apige kwenda pembeni kwa beki wa kushoto au kulia. Hakutekeleza agizo hata moja,” aliwahi kukaririwa  Rigobert Song na vyombo vya Habari.

Kutokana na malumbano na kocha wake akawekwa benchi  baada ya Mechi ya kwanza Kati ya Cameroon na Uswisi. Baada ya kuondolewa Cameroon alitangaza kustaafu soka la Kimataifa. Ameichezea Cameroon mechi 34.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Yanga watanaka kumfanya nini Zawadi Mauya?

MAMBO MATANO YANAYOMKABILI KOCHA MPYA AZAM