WENYEJI wa pambano la mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Yanga walitoshana nguvu dhidi ya wataniwao wa jadi Simba katika mchezo uliofanyika jumamosi Nobvemba 7 mwaka huu. Wikiendi hii imekuwa ya aina yake na mchezo huo umetuletea mambo kadhaa muhimu ambayo tunayaangazia katika makala haya.
1. Mashabiki roho mkononi
Nilikuwa ukumbi mmoja wa soka mjini Morogoro nikitazama mechi kati ya watani wa jadi Yanga na Simba. Siti ya nyuma yangu alikaa kijana mmoja aliyevalia jezi ya Simba. Zilipofika dakika ya 83 ya mchezo kijana huyo aliinamisha kichwa kukata tamaa. mashabiki wa Yanga waliokuwepo ukumbini walimvisha skafu na jezi ya Yanga.
Lakini kibao kikageuka mara baada ya Simba kusawazisha bao kupitia kwa beki wake Joash Onyango Ochieng. Shabiki huyo alianguka kutoka kwenye kiti alichokaa hadi chini pwaa! Akapoteza fahamu. Ndipo mashabiki wa Yanga wakwa wanampa huduma ya kwanza ya kumlaza vizuri, kumpepea na kumwagia maji waliyokuwa nayo kwenye vyupa.
Kisha wakambeba kumwingiza kwenye chumba cha huduma ya kwanza. Sijui nini kiliendelea, lakini naamini aliondoka salama. Mechi ya Yanga na Simba zinakuwa na presha kubwa miongoni mwa mashabiki,wadau,viongozi wa timu, serikalini na kila kona ya nchi. Ni mechi ambayo mashabiki wanakuwa na roho mkononi.
2. Simba wanacheza kama mabingwa haswa
Mabingwa watetezi simba wanacheza soka la uhakika. Ilikuwa burudani kuwatamani namna wanavopasiana. Ni burudani sana kuwatazama, ingawa wana ‘vijitabia’ vya ulalamishi kama ilivyokuwa Barcelona ya Pep Guardiola kila ilipokutana na Real Madrid ya Jose Mourinho ama kwenye mashindano ya Ulaya mara nyingi walikuwa walalamishi mno kwa mwamuzi.
Simba walipia pasi fupi fupi na walipanga viungo wawili wakabaji Mzamiru Yassin na Jonas Mkude. Eneo hili liliwafanya watawale mchezo zaidi, licha ya makosa ya mmoja mmoja katika kipindi chote cha mchezo. Ukiacha makosa, uzembe na kukosa maarifa ya kuipenya ngome ya ngumu ya Yanga, kwa hakika Simba wanacheza mpira mzuri sana.
3. Ukuta mgumu wa Yanga na spidi
Kuna umwamba wa Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto kama mabeki wa kati, halafu kuna spidi ya Tuisila Kisinda na Farid Mussa. Licha ya Moro kutolewa mapema lakini ilionesha namna alivyo mchezaji muhimu kikosini. Ni kiongozi thabiti.
Wachezaji hawa waimeifanya Yanga iwe timu inayocheza kwa kasi zaidi na kuwafanya mabeki wa Simba kuwekwa kwenye shinikizo kila wakati. Tazama kasi ya Farid Mussa ambaye alikuwa kwenye ‘free role’, akicheza pembeni kushoto, katikati na kurudi nyuma kuchukua mipira kwenda mbele.
Spidi ya Tuisila Kisinda ndiyo iliwamaliza Simba katika kipindi cha kwanza, ambapo walishindwa kumdhibiti hivyo kumfanyia madhambi eneo la hatari na kuzaa bao la kuongoza. Hii inanikumbusha pale kocha wa Real Maadrid Zinedine Zidane alipokuwa akimpanga Gareth Bale, sababu ilikuwa ni hii; Speed, pace and power. Kasi, nguvu na nafasi vilihitajika kuipa uhai timu. Hivyo Real Madrid ilitumia nafasi chache kwa kasi na nguvu. Ndiyo kazi ya Tuisila Kisinda, nadhano Onyango kalala na viatu.
4. Vita ya kifundi ilikuwa tamu pembeni
Cedric Kaze kwa vile aliwasoma mabeki wa pembeni wa Simba,naye akachora mstari kuhakikisha mabeki wake wa pembeni hawafanyi kama wanavyofanya wa Simba. Yassin Mustafa upande wa kushoto mara nyingi alipandisha mashambulizi ya Yanga na kuishia mstari wa katikati yaani nusu yao.
Hali kadhalika Kibwana Shomari naye alikuwa akiishia eneo hilo na kufanya kazi ya ulinzi zaidi badala ya kucheza kama beki mshambuliaji wa pembeni. Vita hii ilisababisha Mohammed Hussein na Shomari Kapombe wawe wanapanda kwa tahadhari. Shomari Kapombe alikuwa hatari zaidi kuliko Mohammed Hussein ambaye naye alifanya kama Yaasin Mustafa kuishia kwenye nusu yake. Kisinda alinyukana na Mohammed Hussein, huku Mosquiness akichuana na Yassin au Kibwana Shomari.
5. Onyango ni mwamba mwenye bahati
Refa amekupatia kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Tuisila Kisinda. Kisha mwamuzi alikuwa amemuonya mara mbili ikiwa tayari alikuwa hatarini huenda angepewa kadi ya pili ya njano hivyo kuambulia nyekundu.
Nilitegemea kocha wa Simba, Sven Vandebroeck asingemrudisha uwanjani kuendelea na kipindi cha pili, badala yake alimtoa Larry Bwalya. Vyanzo vya taarifa vilieleza mapema wiki hii kuwa Bwalya alipangwa kucheza mchezo huo huku akiwa anachomwa sindano la kuondoa maumivu aliyonayo.
Hata hivyo kasi ya Kisinda ilikuwa mwiba kwa Onyango, licha ya bahati ya kusahihisha makosa yake kwa kusawazisha bao. Onyango ni beki mtulivu, anayo maarifa na amefanikiwa kuwa beki anayokokota mpira kwa ufasaha na kwa umbali mrefu. Anao utulivu kichwani, licha ya kufanya makosa hakutoka mchezoni yaani akili zake zilikuwa zimetulia mno.
6. Tonombe anawakilisha maarifa ya wachezaji wa kigeni
Wachezaji wa kigeni wanawakilishwa vema na Tonombe Mukoko, Mosquines,Tusila Kisinda, Joash Onyango, Pascal Wawa Lamine Moro ni baadhi ya wachezaji ambao wanawakilisha maarifa ya wageni waliopo VPL. Wachezaji hawa wameongeza ufundi,ushindani,msisimko wa Ligi na kuwavutia washabiki wengi.
Unapomtazama Tuisila, kisha ukamgeukia Wawa na halafu Moussine unaona wazi kabisa ni wachezaji ambao wamekucha chafu ya ushindi katika timu zao. Wanawakilisha maarifa makubwa ya kandanda na kuwaachia wachezaji wazawa. Yanga wanao mawinga watatu mahiri kwa sasa, Deus Kaseke, Farid Mussa na Tuisila Kisinda.
Bila shaka Kisinda atakuwa anawaachia maarifa zaidi kutokana na kasi yake. Toinombo Mukono ametuonesha nini kazi ya kiungo mkabaji. Amezuia pasi vipenyo nyingi za Simba kwenye 18 za Yanga.
Amepanda mbele kusaidia mashambulizi, apiga mashuti lango la Simba, amatumia nguvu zake na ikibidi amecheza mechi kama kiungo mkabaji halisi. Ni furaha kumwona akiwakilisha Yanga. Mmakonde Mosquines naye ni fundi mzuri anayeleta ladha soka la Bongo, akiwa na mpira haeleweki atauficha upande upande upi na kusababisha madhara lango la adui.
7. Yacouba si Sarpong, wana vitu tofauti.
Ukimpanga Yacouba kwenye 4-3-3 maana yake anakuongezea spidi na uwezo wa kukaa na mpra. Yacouba ana mikimbio ya aina yake, na muda aliokuwa uwanjani alikuwa hatari zaidi kuliko Sarpong.
Katika mfumo huo huo ukimpanga Michael Sarpong maana yake anatakiwa kuzungukwa na wachezaji wawili ambao watakuwa na kazi ya kutengeneza pasi ili afunge. Yacouba anaweza kukusadia kwenye ulinzi, na akacheza kama mshambuliaji mmoja peke yake mbele katika mfumo wa 4-5-1, lakini Sarpong atahitaji zaidi mfumo 4-4-2 ambao ni ‘diamond’ zaidi.
Sarpong anaweza kuwa machachari dhidi ya mabeki, ni kama alivyokuwa Joseph Kaniki ambaye alitegemea ‘pace and power’ nafasi na nguvu ili kuwashinda mabeki. Kwa Yacouba anakuja na kitu tofauti kwani anaweza kumiliki mpira kwa muda mrefu mbele ya beki kuliko Sarpong. Je wanaweza kuchea pamoja? Jibu ni ndio na hapana. Ni hapana kwa sababu watakonsa balansi kati ya kiungo na ushambuliaji.
8. ‘Plan B’ ya Kaze?
Simba wanapiga mpira mwingi sana. Wamejaza wabunifu kwenye kikosi chao. Wanaweza kutawala mchezo na kukufunga wakati wowote. lakini Yanga ya Cedric Kaze ‘plan B’ yake ilikuwa ipi?
Kwa haraka mimi ninaweza kusema kulihitajika nguvu na akili ya Calinhos kipindi cha pili kutokana na uwezo, mipira yake yenye malengo na mirefu ingewafanya Simba warudi nyuma zaidi na kusababisha shinikizo kwao. Calinhos ni mmoja tu ambaye anajua kutumia nafasi za mipira ya adhabu,pasi ndefu na maarifa ya ziada kulainisha kazi za timu. Kipindi cha pili Yanga ilikuwa inalinda zaidi bao lao, na akamuingiza Mauya kwa kulinda, hali ambayo ilisababisha Shomari Kapombe aongeze kasi ya kupanda zaidi na kuwasumbua Yanga.
Uzuri ni kwamba Yanga hawajafungwa mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Kutoka sare na Simba wamedhihirisha kuwa wamedhamiria kulitwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Comments
Loading…