in

Yanga kumaliza ufalme wa Simba?

Yanga Vs Simba

Kwa miaka minne mfululizo Simba wamekuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania. Simba wametwaa kila kitu katika miaka hiyo, kuanzia Ligi Kuu,Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii kadiri walivyojisikia. Ni miaka minne ambayo Yanga walikuwa wakiugulia maumivu ya kukosa ubingwa na angalau sasa wameanza kuchukua taji la Ngao ya Hisani na Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar.

Maumivu ya Yanga ni sawa na makocha wazawa ambao kwa miaka 20 sasa wameshindwa kufurukuta kutwaa taji hilo hivyo kuwaachi makocha wa kigeni kunyakia kadiri walivyotaka. Pia makocha wazawa wameshindwa kufikia rekodi ya John Simkoko aliyetwaa taji la Ligi Kuu mksimu miwili mfululizo ya mwaka 1999 na 2000.

Katika mchezo wikiendi iliyopita kati ya Yanga na Azam FC uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kulikuwa na masuala kadhaa ambayo yanaonesha dalili za mabingwa wa zamani kutaka kukata ngebe za Simba. Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam yaliyofungwa na Fiston Mayele na Jesus Moloko. Je ni mambo gani yanayoonesha Yanga wanaweza kunyakua taji hilo?

UNENE WA BENCHI LA UFUNDI

Benchi la ufundi la Yanga lina watu wa nguvu. Kocha mkuu ni Nasredine Nabi anasaidiwa Cedric Kaze. Kaze amewahi kuwa kocha mkuu wa Yanga kabla ya kufutwa kazi, lakini amerejea msimu huu kuwa chini ya Nabi. Kimsingi hawa wote ni makocha wa kigeni, Kaze ni raia wa Burundi na Nabi ni raia wa Tunisia.

Benchi hilo linaonesha kuwa limejipanga na kunyakua ubingwa. Unene wa benchi una maana kwamba ndilo lenye makocha wenye wasifu mkubwa zaidi kuliko wengine katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wapinzani wao Simba wametoka kuachana na makocha wao akiwemo mkuu Didier Gomes baada ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Jwaneng Galaxy kwenye Ligi ya Mabingwa.

Kwa sasa wapo chini ya Hitimana Thiery raia wa Burundi, huku wakiwa kwenye msako wa kocha mpya. Kwahiyo unene wa benchi za ufundi la Yanganunaipa matumaini makubwa ya kukomesha ufalme wa Simba tangu 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020, 200-2021. Kwa kipindi chote hicho mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiishi kinyonge mbele ya wale wa Simba.

VITA  KUBWA YA NAMBA YANGA

Nafasi ya kiungo ya Yanga imeingia katika vita kubwa. Makocha wana kibarua kigumu cha kuamua nani aanze kikosi cha kwanza kati ya Yannick Bangala,Khalid Aucho,Mukoko Tonombe,Zawadi Mauya na Feisala Salum. Wote hawa wanawania kucheza namba 6 na 8.

Nani awe kiungo mkabaji na nani apande mbele kucheza kiungo mshambuliaji. Kwa kawaida nafasi ya kiungo mshambuliaji inachukuliwa Feisal Salum, huku kibarua kigumu kikiwa katika nafasi ya kiungo mkabaji kati ya Tinombe,Mauya na Bangala.

Katika vita hiyo kila mchezaji atajitahidi kuonesha uwezo mkiubwa utakaomshawishi kocha Nabi ampange katika mechi nyingi zaidi. ushindani huo ndio utawapa nafasi Yanga kuwa viungo imara na wenye uwezo wa kumtawala mpinzani wao yeyote.

Nafasi ya ushambuliaji nayo imekuwa na ushindani mkubwa. Yacouba Sogne,Herieter Makambo, Fiston Mayele,Yusuf Athuman na Ditram Nchimbi wanapigania namba katika eneo ya ushambuliaji.

Makocha wanayo kazi kubwa ya kuamua nani apangwe kikosi cha kwanza na nani abakie benchi. Hadi sasa Fiston Mayele anaonekana kuongoza jahazi la safu ya ushambuliaji, huku Yusuf Athuman akiwa mshambuliaji chaguo la pili. Nchimbi na Makambo wanaonekana kuwa chaguo la tatu ambalo ni la mwisho.

Mawinga wa Yanga nao wameingia vitani. Deus Kaseke, Jesus Moloko, Farid Mussa wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwashawishi makocha wa Yanga ili wapangwe.

Jesus Moloko anaonekana kuwapiga kumbo wenzake, na katika mchezo dhidi ya Azam alipachika bao la pili. Kasi,chenga na uwezo wa kuwapangua mabeki wa timu pinzani ni kigezo kinachompa nafasi winga huyo mbele ya wenzake. Lakini bado eneo hilo linanekana kutokuwa na mwenyewe.

Beki wa kushoto wa Yanga nako kuna shughuli sio kidogo. Adeyum Saleh na Mustapha Yassin ni mabeki asilia wa kushoto. Yassin amekuwa majeruhi wa muda mrefu, lakini sasa amepona na huenda siku zijazo akapangwa, lakini kabla ya uamuzi huo kufanyika inabidi ahakikishe anamzidi uwezo na maarifa beki anayetumikia nafasi hiyo sasa, Kibwana Shmari.

Adeyum Saleh licha ya kuchezeshwa mara kadhaa eneo hilo inaonekana hajamridhisha kocha wake. Hivyo basi Kibwana Shomari ambaye kiasili ni beki wa kulia amekuwa akipangwa kucheza beki wa kushoto na ameitendea haki kiasi kwmaba kumng’oa itakuwa kazi ngumu. Ushindani huo unasaidia Yanga kuwa imara katika mbio za kuwania ubingwa. Lakini wataweza kumaliza ufalme wa Simba?

Mabeki wa kati Dickson Job na Bakari Mwamnyeto ni kama wanaelekea kumiliki nafasi zao namba nne na tano. Pale benchi wapo nyota wengine kama Abdallah Shaibu mwenye uwezo wa kucheza nafasi hiyo,lakini hadi sasa ameshindwa kuwatoa vinara hao wawili. Eneo hilo linawapa nafasi Yanga kupigania ubingwa kwa sababu safu hiyo hairuhusu mabao ya kufungwa.

KUHIMILI PRESHA YA MCHEZO

Ushindi wa kwanza wa Yanga upo eneo hili, kuhimili presha za mechi na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka. kwamba Yanga wanatazamwa kama timu ambayo itaweza kupambana vilivyo na Simba, lakini ili ifanikiwe hilo lazima wawe na uwezo mwa kuhimili presha za michezo yao.

Katika ulimwengu wa soka wapo wachezaji wanaweza kutamba katika timu ndogo lakini wakashindwa kung’ara ndani ya jezi za Simba na Yanga. Ipo hivyo kwa baadhi ya makocha ambao wamekuwa wakitamba kwenye timu mbalimbali lakini wanapopewa kazi ya kuzinoa Simba au Yanga wanafeli.

Presha ya timu hizo mara nyingi zimesababisha makocha hao kutupiwa virago na namna ambayo mashabiki wengi wanashindwa kuelewa kinachomtokea licha ya sifa kuwa alikuwa mahiri mahali kwingine.

Kwa vile Yanga na Simba zimeweka viwango vya ushindani kwahiyo kila mmoja anatakiwa kumshinda mwenzake kudhihirisha utemi wake kwenye kandanda. Benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuhimili presha wanayokabiliana nayo ili kuipatia ushindi Yanga.

NYOTA WAZAWA WATATOBOA?

Kuna mastaa wazawa wanaamini hawajazidiwa uwezo na wachezaji wa kigeni. Deus Kaseke,Farid Mussa,Ditram Nchimbi,Yusuf Athuman,Zawadi Mauya,Shomari Kibwana,Feisal Salum,Dickson Job,Bakari Nondo Mwamnyeto na wengineo wana kibarua cha kuonesha umahiri wao mbele ya wachezaji wa kigeni. Ni nani ataibuka kuwa kinara mbele ya wachezaji hao wa kigeni mwishoni mwa msimu? Hilo nalo swali linalosubiri majibu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Jwaneng Galaxy

Dakika 90 ‘Kwa Mkapa’ zilizowamaliza Simba 

West Ham

Nani huyu anataka kuinunua West Ham United?