in

Dakika 90 ‘Kwa Mkapa’ zilizowamaliza Simba 

Jwaneng Galaxy

Mabingwa wa soka nchini Tanzania klabu ya Simba imetupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa klabu ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. kutoka makosa ya wachezaji mmoja mmoja, benchi la ufundi na timu kw aujumla wake ni miongoni mwa sababu zilizowatupa nje ya mashindano Simba. 

TANZANIASPORTS inakuleta uchambuzi kuhusiana na mchezo mzima kutoka nchini Botswana hadi jijini Dar es salaam. Ni mambo gani yaliwamaliza Simba katika mchezo huo, pamoja na namna Simba wanavyoonekana kurudia makosa mara kwa mara tangu fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 hadi mpambano dhidi ya Jwaneng Galaxy ambao wametinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yao.

KURUDIA MAKOSA

Kwa mujibu wa kocha maarufu nchini Tanzania, Meja Mingange amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa Simba ni kama timu isiyojifunza kutokana na makosa ya miaka ya nyuma kuania fainali ya Kombe la CAF hadi Ligi ya Mabingwa miaka ya karibuni. 

“Wapenzi wa Simba pamoja na Watanzania wapenda soka na uzalendo wan chi mechi hii ya Simba imewaumiza watu wengi kwa sababu Simba ilikuwa na mtaji wa goli mbili na bahati wakaja kupata moja hapa nyumbani. Kuna jambo naona Simba hawajajifunza. Tukio hili la kufungwa na Jwaneng Galaxy ni la mara ya tatu. Mwaka 1993 Simba ilifika fainali ya Kombe la CAF, mechi ya kwanza kule Ivory Coast iliisha kwa sare 0-0. Kazi ilibaki kushinda goli moja tu wabebe ubingwa. Simba walifungwa magoli 2-0 uwanja wa Uhuru. Mara ya pili ni dhidi ya UD Songo ya Msumbiji nah ii mara ya tatu sasa. 

MAKOSA YA MAKOCHA

Mtaalamu wa soka Kocha Meja Mingange anaendelea kuchambua, “Mchezo wa Simba dhidi ya Galaxy wapenzi wa mpira wanapenda matokeo hasa ya kushinda tu. Simba haikucheza vibaya ila imepata matokeo mabaya. Nini kilichotokea uwanjani? Kwanza naamini wachezaji na wapenzi wa mpira waliamini shughuli imeisha, hilo ni kosa kubwa sana kwa sababu dakika 90 hazikuwa zimekwisha. Mchezo wa mpira hautabiriki hata siku moja. 

Anaongeza, “Wachezaji wa Simba waliamini mechi imeisha baada ya kupata goli moja, hilo ni kosa la pili. Kosa la tatu ni walimu wa Simba walifanya mabadiliko kwa sababu walikuwa na wachezaji nje si kwa sababu za kiufundi au mbinu. Bernard Morrison alikuwa mchezaji tishio kwa Galaxy hivyo hakuwa mchezaji wa kubadilishwa. Baada ya kuwa sare Meddie Kagere angeingia kuwa na washambuliaji wawili. Nne Simba wangeendelea na mbinu zaomza kucheza mpira kwa pasi fupi fupi kupitia pembeni. Labda angeingia Duncan Nyoni kwa nafasi ya Hassan Dilunga. Tano, kulikuwa na haja gani Simba kukimbizana kwa muda uliobaki wakati yule alikuwa anataka magoli mawili? Muda mwingi wangekaa na mpira tu. Yote kwa yote tukubali mpira una siku na bahati.”

KUSHINDWA KULINDA USHINDI NA MABEKI

Lipo suala jingine ambalo walimu wameshindwa kutekeleza, kwamba Simba walihitaji viungo wa ulinzi angalau watatu. Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin walipaswa kucheza pamoja kwa nia ya kubloku na kuwarudisha nyuma Galaxy. 

Badala yake kati ya Lwanga na Kanoutre kukawa na mapengo yaliyowabadili mbinu wapinzani wao. Galaxy waliingia kipindi cha pili na kupiga mipira mirefu ili kuwakumbiza mabeki wa Simba. Inafahamika mabeki wa Simba na viungo hawana kasi hivyo kilichofanyika ni kuwazungusha mbele na pembeni. 

Kwamba pasi ndefu za Baruti zilikwenda katikati ya eneo la hatari la Simba na pembeni kwa Shomari Kapombe na Mohammed Hussein. Benchi la ufundi lilipaswa kuamgalia njia ya kulinda ushindi wao sio kupambana kutanua uwanja na kutafuta mabao. Kwa mechi ya Galaxy Lwanga na Kanoute hawakucheza vibaya lakini walihitaji msaada katika eneo hilo ambapo walimu walipaswa kuliona mapema mwanzoni mw akipindi cha pili. 

KUJIAMINI KUPINDUKIA

Mchezo wa soka una dakika 90 za nyumbani na zingine ugenini. Katika dakika 90 a kwanza Simba walishinda ugenini, hivyo wakawa wamebakiza dakika 90 zingine nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa. Simba waliingia katika mchezo wa marudiano wakiwa na faida ya bao mawili waliyopata ugenini wiki moja iliyopita. 

Ushindi wa mabao 2-0 uliwapa matumaini Simba kuwa wasingeshindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi hiyo. Ndio maana baada ya kufungwa bao la tatu Shomari kapombe alishika kichwa kwa mshangao na kuonesha kama haamini kile kilichotokea. Ile ni ishara kwamba wachezaji waliajimini kupita kiasi hivyo kuwadharau Jwaneng ambao walitambua kuwa wanacheza dhidi ya kigogo wa soka Afrika na hivyo lazima wapambane ili kupenya kuingia makiundi.  

KUKOSA MABAO YA WAZI

Simba walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hawakupata magoli. John Bocco, Larry Bwalya,Morrison,Dilunga,Peter Banda ni wachezaji waliopata nafasi za kufunga lakini hawakukwamisha mpira wavuni. Simba wangeweza kuibuka mabao matatu hadi manne katika kipindi cha kwanza. 

Kushindwa kutumia nafasi zao vizuri ndio adhabu pekee waliyopata ndani ya dakika 90 kwani wapinzani wao walitumia nafasi zao kupachika mabao. Kwa mfano bao la pili lilitokana na makosa ya walinzi kuzubaa na kumpa nafasi Wendell aunganishe mpira uliorushwa na mlinzi wake. Kwa bao lile wapenzi watajiuliza nini kilichotokea kwa Pascal Wawa na wenzake kubaki kukodolea macho wakati mshambuliaji Wendell wa Galaxy alipokwamisha mpira wa pili wavuni? Makosa madogo madogo yamewaadhibu Simba hivyo kutupwa nje ya michuano.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Michael Edward

Siku Michael Edward aking’oka Liverpool

Yanga Vs Simba

Yanga kumaliza ufalme wa Simba?