in , , ,

Yanga inawahitaji MHILU na MAKAMBO kuifunga SIMBA

makambo

Inawezekana tarehe 8 mwezi wa tatu mwaka huu yaani jumapili ijayo nchi nzima ikawa imesimama, shughuli nyingi za uchumi zikawa zimepumzika kwa ajili ya kuitazama Kariakoo Darby.

Darby ambayo hubeba hisia za watu wengi kwa sababu tu ndiyo Darby ambayo inabeba maisha ya watu. Kuna watu wamewekeza maisha yao kwenye hizi timu za Simba na Yanga.

Hapo ndipo mwanzo wa mchezo huu kuwa wa hisia unapoanzia. Kila shabiki hupenda timu yake ishinde, hakuna anayetamani timu yake ifungwe kwenye mechi hii, mioyo yao huwa juu kwa ajili ya matokeo ya hii mechi.

Matokeo pekee ambayo hujaza furaha upande mmoja wa timu ni ushindi na matokeo pekee ambayo hujaza huzuni upande mwingine wa timu nyingine ni kufungwa. Kwa hiyo ushindi ndicho kitu pekee kinachohitajika kwenye timu zote.

Ushindi ambao kwa siku zote huamuliwa na safu ya ushambuliaji. Safu ya ushambuliaji ikiwa nzuri inakupa asilimia kubwa ya ushindi kwa sababu ya matumizi sahihi ya nafasi ambazo huzipata.

Yanga kwa mechi za hivi karibuni inatumia muda mwingi sana kumiliki mpira tofauti na zamani ambapo walikuwa wanatumia mipira mirefu sana kwa sababu ya aina ya wachezaji ambao walikuwa nao.

Yanga ilizoea kuwa na wachezaji wa pembeni ambao wana kasi pamoja na uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga wakitokea pembeni mwa uwanja ndipo hapa unapowakumbuka kina Simon Msuva, Edibilly Lunyamila na Said Maulid “SMG”.

Kwa sasa ni tofauti kabisa, Yanga imejaza wachezaji wengi wenye asili ya kiungo cha Kati. Hawana tena aina ya wachezaji ambao walizoea kuwa nao kipindi cha nyuma. Wanategemea sana viungo wa kati kwa ajili ya kufunga magoli na kutengeneza nafasi.

Kitu ambacho ni kigumu sana kwa Yanga kwa sababu aina ya viungo wa Yanga ni viungo ambao hawatengenezi nafasi nyingi za magoli na hawafungi sana wakitokea katikati.

Hiki kitu hufanya Yanga kuonekana, wanacheza sana kwenye robo tatu ya uwanja Lakini kwenye robo ya mwisho yani “final third” mipira huwa ni michache kwa sababu ya aina ya viungo ambao wanao.

Viungo ambao hawatengenezi sana nafasi za kufunga magoli na ndiyo viungo ambao hawafungi sana magoli. Kwa hiyo mtu pekee ambaye Yanga wanamtegemea ni mshambuliaji wa Kati kwa ajili ya kufunga.

Tofauti na zamani ambapo wachezaji ambao walikuwa wanatokea pembeni mwa uwanja walikuwa wanafunga kwa kusaidiana na washambuliaji wa kati wa Yanga. Kuna wakati Donald Ngoma, Obrey Chirwa walikuwa wanafukuzana kwa wingi wa magoli na Simon Msuva ambaye alikuwa anatokea pembeni.

Kwa hiyo uzalishaji wa magoli ulikuwa mkubwa na ulikuwa hautegemei kwa mchezaji mmoja tu tofauti na sasa hivi, Yanga wachezaji wao wa pembeni hawafungi sana, wachezaji wa katikati ya uwanja hawafungi sana na kibaya zaidi hata washambuliaji wao hawafungi sana.

Hapa ndipo mwanzo wa wazo langu la makala hii linapoanzia. Yanga msimu uliopita waliwahi kuwa na Herieth Makambo ambaye alifunga magoli zaidi ya 15. Msimu jana walikuwa na mchezaji ambaye alikuwa anatokea pembeni Yusuph Mhilu.

Chini ya George Lwandamina, Yusuph Mhilu alikuwa anatengenezwa kama mchezaji ambaye alikuwa anafunga sana akitokea pembeni Lakini kwa bahati mbaya hakuaminiwa sana kwenye kikosi cha Yanga akapelekwa Kagera Sugar.

Sehemu ambayo kwa sasa ana magoli 11 ndiye mchezaji wa pili kwenye ufungaji wa magoli baada ya Meddle Kagere mwenye magoli 16. Kwa sasa Yanga hawana Makambo (mshambuliaji anayefunga sana) na Mhilu (winga anayefunga sana).

Kwa sababu wachezaji wa sasa wa Yanga katika eneo la kiungo cha Kati hawafungi sana na wachezaji wa kushambulia hawafungi sana basi Yanga walikuwa wanahitaji mshambuliaji anayefunga sana na winga anayefunga sana.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ni ‘vita’ Uefa na Fifa

Tanzania Sports

Manchester Derby: Pambano lisilotabirika