in , , ,

Manchester Derby: Pambano lisilotabirika

Manchester Derby: Pambano lisilotabirika

Mechi ya watani wa jadi wa Manchester – au Manchster Derby (dabi) imekaribia na kwa jinsi mambo yapo wakati huu, haitabiriki kwamba ni nani ataibuka kidedea kati ya Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United na Pep Guardiola wa Manchester City.

Ni mechi kubwa si tu kwa jiji la Manchester bali England, Uingereza na hata dunia, kwa sababu washabiki maelfu kwa maelfu wanafuatilia kwenye mitandao ya jamii na wakati wenyewe ukiwadia watakuwa mbele ya skrini za televisheni zao kutazama.

Siku hizi ni vigumu kujifikirisha na kuona kipi cha kutarajia kutoka kwenye dabi za jamaa hawa siku hizi, huku Manchester United wanaochechemea kiasi kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) wakishitukiza mara moja moja na kupiga wasiotarajiwa kama Chelsea, huku Man City nao wakitisha.

Wakati Man United zamani walikuwa ndiyo timu kubwa kwa miaka kadhaa, wakiwa na ngome ya Old Trafford ambayo haikuwa ikiguswa hovyo hovyo hasa zama za Sir Alex Ferguson, sasa wamekuwa wakipoteza mechi chini ya mchezaji wake huyu wa zamani wa eneo la kiungo – Solskjaer.

Man City walitia fedha nyingi kwenye usajili na uendeshaji wa klabu baada ya kununuliwa na Waarabu wa visima vya mafuta na madini, na wameweza kutwaa ubingwa na kufanya vyema chini ya Guardiola hadi kutwaa ubingwa, lakini hufikia kuduwazwa na wale wasiotarajiwa, hata kama majuzi waliwapiga Real Madrid kwao Madrid.

Man United wangependa kurejesha nguvu yao ile ya zamani, lakini kama alivyosema Solskjaer, si siku moja mbili wala mwaka – ni mchakato. Mapambano ya jamaa hawa yamekuwa na kawaida ya kutoa matokeo yasiyotarajiwa, dabi ikimalizika kinyume na kile watabiri walichokuwa wamesema.

Mechi hii inachezwa Jumapili kama ilivyo ile ya Simba na Yanga nyumbani Dar es Salaam, wenyeji wakiwa ni Man United. Wageni wameshinda mechi sita kati ya saba zilizopita a dabi hii ya Manchester, na kwa kawaida wamekuwa wakivunjilia mbali utabiri unaokuwa umefanywa kabla ya mechi, tena kitaalamu.

Ukitazama mambo yalivyokuwa katika dakika za mwanzo za mechi ile ya Desemba, kulikuwapo wachezaji waliokuwa na kasi kubwa katika Marcus Rashford, Anthony Martial na Daniel James walionesha kuwazidi nguvu na maarifa . United wana makosa mengi chini ya ukocha wa Solskjaer, lakini hufika mahali wakafanya ‘mauaji’, ndiyo kusema hawatabiriki.

City nao wana washambuliaji wakali kwenye upande wa ushambuliaji, na kwa ujumla Guardiola ana uwezo mkubwa wa kubadilisha mwenendo wao uwanjani katika nafasi zote, isipokuwa siku ambayo maji yanaonekana kabisa kwamba yamezidi unga.

Kuna mpangilio wa asili wa mambo na ni wazi kwamba kwa sasa City wanaonekana kuwa juu na wenye nguvu zaidi. Hata kwenye ligi kuu wanawazidi mahasimu wao hawa kwa alama 15, japokuwa ujio wao wa mwisho hapo Old Trafford haukuendana na nguvu yao, tofauti kabisa na 2011 ambapo waliwadunga City 6-1.

Ingekuwa ngumi, si ajabu watu wangekuwa wanampa nafasi Solskjaer zaidi ya Guardiola lakini kubwa ni kusubiri wakati wenyewe ufike na kuiona mechi. Alhamisi wiki hii Man United waliwashinda Derby kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA, ushindi ambao kocha ameuchukulia vyema lakini alionekana kuchukua hadhari kuliko inavyokuwa kawaida, akijua kinachomsubiri siku chache tu baada ya hapo.

“Unapokuwa nyumbani unatakiwa kufungua mchezo kwa timu kama Man City, lakini ukiwa huna uhakika kwa asilimia 100 juu ya unachokifanya, basi watatumia udhaifu wowote utakaotokea kwa ajili ya kukuteketeza. Wakati mwingine ukiwa unacheza nyumbani na washabiki wako wanakutazameni, unataka kuwaonesha ule udambwidambwi ambao wangependa kuona na kumshinda mpinzani wako,” anasema.

Anaongeza kwamba kinachotakiwa kwa wachezaji wake ni kuweka uwiano katika kuamua kufunguka na kwenda kushambulia vilivyo, lakini pia wakihakikisha wanajilinda vyema. Guardiola anajulikana kwa kutoa kikosi cha kushangaza na aina ya mifumo ya kucheza huku Solskjaer naye akiwa hatabiriki.

United walijaribu ‘diamond’ walipocheza Goodison Park kwa Everton wiki jana ili kuhakikisha wanapata kwa kiasi kikubwa kile walichokuwa wakikitaka kutoka kwa mchezaji wao mpya matata, Bruno Fernandes, na kweli aling’ara sana.

Kwenye dabi iliyopita, Solskjaer aliweka ulinzi wa watu watatu huku Anthony Martial na Mason Greenwood wakitakiwa kujenga upili katika ushambuliaji. Kwneye ushindi kule EtihadDesemba, inaonekana ulitokana na uamuzi wa Solskjaer kujaribu na kutumia mfumo wa 4-2-3-1.

“Nina uhakika tuna tunu moja nzuri, nayo ni kushitukiza na kushangaza wapinzani wetu,” anasema raia huyu wa Norway. Ni aina hiyo ya mabadiliko ya mara kwa mara yaliwawezesha United kwenda mechi tisa bila kupoteza hadi walipokuja kutandikwa nyumbani na Burnley.

Wamekubali kufungwa mabao mawili tu wakati wenyewe wakifunga 22, lakini nyingi ya timu walizokabiliana nazo ni ndogo ndogo kwa hiyo hawatakiwi kujisifu sana wala kubweteka. Ni ngumu pia kujidai kwa hakika kwamba watawalaza City. Tangu kung’atuka kwa Fergie kwa ujumla City wamewazidi watani zao hao kwa alama 91 za mechi uwanjani. Fergie alikuwa akiwiata majirani wapiga kelele, kwa jinsi walivyoanza vitimbi na kushangilia kutokana na kufanya vyema baadaye.

Wakati Man U wakipewa nafasi kutokana na dabi kuwa na tabia za kupindua matarajio ya watabiri, City wanapewa nafasi pia kwani timu za ugenini zimetokea siku hizi kuibuka na ushindi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Yanga inawahitaji MHILU na MAKAMBO kuifunga SIMBA

Tanzania Sports

Feisal Salum “Fei Toto” atawasumbua Simba leo