in ,

Arsène Wenger – KOCHA WA KUDUMU ARSENAL

Arsene Wenger amepewa mkataba wa miaka miwili utakaombakisha Arsenal mbaka 2019. Mfaransa huyo hakuwa na msimu mzuri mwaka huu kufuatia kushindwa kuiwezesha Arsenal kuwemo kwenye nafasi nne za juu za EPL na hivyo kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Hata hivyo Mmiliki wa Arsenal Stan Kroenke ameendelea kumuamini Wenger na kumpatia nafasi ya kuendelea kusalia Arsenal.

Inaripotiwa kuwa ingawa baadhi ya vigogo wa bodi ya Arsenal hawakubaliani na swala la Wenger kuendelea kuwa meneja wa klabu yao lakini uamuzi wa mwisho upo kwa Kroenke anayemiliki sehemu kubwa zaidi ya hisa ndani ya Arsenal. Mfanyabiashara huyo mkubwa kutoka Marekani amekutana na Wenger na kutumia muda mwingi kujadili hatma ya kocha huyo tangu Jumamosi baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea.

Hivi karibuni Wenger amekuwa katika mgogoro na baadhi ya vigogo wa Arsenal kuhusu mpango wa bodi kufanya mabadiliko ya mfumo wa kiufundi. Ivan Gazidis ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa klabu hiyo ameshikilia mpango wa kuongeza nafasi mpya ya ‘Mkurugenzi wa Ufundi’ kwenye benchi la ufundi la timu hiyo. Wenger anaupinga mpango huu na aliwahi kuweka wazi kuwa hataendelea kuwa kocha endapo kutakuwa na mtu kwenye nafasi hiyo anayoiona haina maana na inaingilia mamlaka ya kocha nje ya uwanja.

Gazidis aliwahi kuweka wazi kuwa cheo hicho kipya hakiwezi kuathiri mamlaka ya kocha. Alidai kuwa kazi za ‘Mkurugenzi wa Ufundi’ zitahusu kuratibu maswala ya kutafuta vipaji vipya, mambo ya kitabibu ya wachezaji na mambo ya timu za vijana. Alieleza kuwa mamlaka ya kocha kwenye kufundisha kikosi, kuchagua wachezaji kwa ajili ya michezo na mikakati ya uhamisho hayataingiliwa. Lakini Wenger bado alibaki na msimamo wa kupinga mpango wa kuanzishwa nafasi hiyo mpya.

Taarifa rasmi kuhusu mkataba mpya wa kocha huyo inatarajiwa kutolewa Jumatano. Klabu hiyo ya jijini London inaendelea kubaki na Arsene Wenger tangu alipojiunga nayo miaka 21 iliyopita. Ikiwa atasalia mbaka mwishoni wa msimu wa 2018-19 kama unavyohitaji mkataba wake huo mpya atamzidi Sir Alex kwenye rekodi ya kuongoza timu kwenye michezo mingi zaidi ya EPL.

Lakini kwanini anaendelea kusalia ndani ya Arsenal? Misimu 13 imeondoka tangu ubingwa wa mwisho wa EPL aliowapatia Washika Bunduki hao wa London kwenye msimu wa 2003-04. Inashangaza kuona akisalia kuinoa klabu hiyo yenye mataji mengi zaidi ya EPL ukiwatoa Manchester United na Chelsea tangu mwaka 1992 mashindano hayo yalipoanzishwa rasmi.

Chelsea wanayo mataji matano ya EPL tangu Arsenal walipotwaa ubingwa wa mashidano hayo kwa mara ya mwisho. Wanalo pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya walilotwa msimu wa 2011/12. Lakini tayari wameshabadilisha makocha zaidi ya mara 10 tangu mwaka 2004 Arsenal walipopata taji lao la mwisho la EPL huku majina makubwa kama Luiz Felipe Scolari, Carlo Ancelotti, Jose Mourinho na mengine yakipita na kuondoka Darajani. Wenger bado yumo.

Manchester City si miongoni mwa klabu zenye historia kubwa sana kwenye soka la England lakini wameshatwaa mataji mawili ya EPL tangu ubingwa wa mwisho wa Arsenal. Pamoja na mafanikio hayo wameshabadili makocha mara 7 tangu Arsenal waliponyanyua taji lao la mwisho la EPL mwaka 2004. Ivan Kroenke bado anaendelea kubaki na Arsene Wenger.

Pengine klabu hiyo bado inastahili kuwa na imani na kocha wao huyo aliyedumu tangu mwaka 1996 kufuatia ushindi wa taji la FA Jumamosi baada ya kuwafunga mabingwa wa EPL (Chelsea) kwa 2-1 kwenye mchezo wa fainali. Hilo ni taji la tatu la Kombe la FA kwa Arsenal ndani ya miaka minne wakiwa wamelitwaa pia kwenye misimu ya 2013/14 na 2014/15. Inaweza kusemwa kuwa Wenger ni kocha wa kudumu Arsenal.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

AZAM WAMEMCHOMA KISU JICHONI BOCCO, HUKU WAKIWA WAMEMTUMBULIA JICHO.

Tanzania Sports

INASHANGAZA KUSHANGAA VALVERDE KUWA KOCHA WA BARCELONA