Mwanzoni mwa miaka ya 2000 kulitokea kundi moja ambalo lilipata mashabiki wengi wa mziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Kundi hilo sio linguine bali ni kundi la Wagosi wa kaya. Kundi hilo lilikuja na mtindo wake wa kipekee ambao ulikuwa unatumia lafudhi ya kuimba kama wanavyozungumza watu wa Tanga. Wimbo wao ambao uliowatoa na ukawafanya wakawa maarufu sana ulikuwa unaitwa “TANGA KUNANI PALE”. Wimbo ule ulikuwa unagusia masuala mbalimbali ya kijamii ambayo yalikuwa yanaikumba jamii ya wakazi wa Tanga. Kuanzia masuala ya kijamii mpaka masuala ya kisiasa. Wimbo ule uliwika na ukawa kama ni wimbo wa taifa. Prodyuza Master Jay amewahi kutamka hadharani kwamba moja ya albamu ambayo ilimfungulia milango ya kuanza kutengeneza pesa katika masuala ya mziki ilikuwa ni albamu ya Wagosi wa kaya.
Katika nyakati hizo hizo jijini Tanga bwana Joseph Rushahu aliamua kijikita kwenye mziki na akajipa jina la “Bwana Misosi” na aliingia studio jijini Dar es salaam na kurekodi wimbo na msani mwenzake Hard Mad wimbo walioupa jina la “NITOKE VIPI?”. Wimbo aliamua kuelezea namna ya mitindo ambayo wasanii wengi maarufu wa nyakati hizo walivyoamua kutoka katika Sanaa ya mziki kwa kila mmoja kwa namna yake. Wimbo huo nao ulivuma nchi nzima na ukamfanya bwana misosi akawa staa mkubwa katika ukanda wa Afrika mashariki. Bwana misosi alijaribu kuwauliza mashabiki wa mziki wampe majibu ya juu namna gani atumie ili aweze kupata mafanikio katika Sanaa ya muziki. Baada ya hapo akatoa wimbo wa mabinti wa kitanga ambao ndani ya wimbo huo alisifia wanawake ambao wanaotoka ndani ya mkoa huo.
Miaka 20 baadaye historia imeandikwa katika jiji la Tanga kwa klabu yao pendwa ya Coastal Union kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa kwa kufuzu kushiriki mashindano ya kombe la shirikisho la soka barani Afrika. Wamefuzu wakati ambapo misimu 2 iliyopita klabu ya Yanga ilifika hatua ya fainali ya kombe hilo kwa jitihada za hali ya juu. Klabu ya Coastal Union wanajiita jina la Wagosi wa kaya kama jina lao la utani na mashabiki wamelikubali sana jina hilo kwani huwaita wagosi wa kaya. Mafanikio hayo yanakuja katika msimu wake wa kwanza baada ya kusaini mkataba na kampuni ya ELSEWEDY ELECTRIC ndipo wanapata mafanikio ya kufuzu kushiriki mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Wagosi wa kaya wa Coastal Union ambayo inakadiriwa kuwa na umri wa miaka Zaidi ya 60 na hakika mashabiki wana kiu ya kuwaona wakifanya mambo makubwa katika soka la nchi yetu kwa ukongwe wao. Klabu ya Simba imezindua kauli mbiu yao ya Ubaya Ubwela na hakika kwa kauli mbiu hiyo imewagusa washabiki wengi wa soka nchini Tanzania. Yanga wamejitambulisha kwenda ziara nchini Afrika Kusini ambapo walishiriki mashindano ya TOYOTA CUP ambapo walipata nafasi kucheza na vilabu kama Kaizer Chiefs. Swali linakuja mbona Coastal Union wako kimya kunani pale? Mbona hawatuonyeshi wachezaji ambao wamewasajili kwa ajili ya msimu huu?
Kuna muda klabu hiyo ilitoa taarifa kwamba ilikuwa ina mpango wa kuutumia uwanja wa Mkwakwani kama uwanja wa nyumbani kwa ajiliya mechi za kimataifa. Na katika kulifanikisha hilo wakawa wameanza ukarabati wa uwanja huo. Kama watafanikiwa kuukarabati na ukapitishwa kutumika kwa uwanja huo kwa ajili ya mechi za nyumbani basi watakuwa wana fursa ya kucheza mechi zao huki wakiwa wana mtaji wa mashabiki wao wa nyumbani ambao itawasaidia kuwaongezea morali ya kucheza ili wapate matokeo ya ushindi mnono katika mechi za nyumbani.
Kiujumla sehemu kubwa ya mashabiki wa klabu hiyo wa ndani ya mkoa wa Tanga na nje ya mkoa wa Tanga bado wanajiuliza Coastal Union kunani pale na wengine wakiwa wanajiuliza Coastal Union itatoka vipi? Katika mashindano ya kimataifa kwani mpaka sasa klabu hiyo haijafanya usajili wa kushitua nchi licha ya kwamba kuna mda ilitangaza inamtaka mchezaji wa kimataifa wa Burundi Saido Ntibazonkiza lakini haikkufanikisha usajili huo.
Comments
Loading…