Leo hii hakuna anayemkumbuka Ramadhani Singano “Messi” kwa uharaka.
Kuna miguu mbalimbali ya kushoto ambayo najivunia kuitazama mpaka sasa hivi kwenye ligi yetu kuu ya Tanzania bara. Simba SC iliwahi kuwa na Ramadhani Singano ambaye mahaba yalituzidi tukaamua kumwiita “Messi”.
Mahaba ambayo mwanzoni yalituonesha uchawi wa Lionel Messi kwenye miguu ya Ramadhani Singano. Kipindi ambacho alichokuwa anavyokokota mpira kitu pekee kilichokuwa kwenye akili yetu ni Lionel Messi.
Kipaji cha Ramadhani Singano “Messi” kilikuwa kikubwa sana na wengi tulitamani sana kukiona kikifika mbali lakini kuna kitu kimoja kilipungua katikati ya kipaji na mafanikio. Cristiano Ronaldo aliwahi kusema kipaji bila jitihada ni kazi bure.
Jitihada ilipungua katikati ya kipaji na mafanikio ya Ramadhani Singano “Messi” mpaka akashindwa kufika ile sehemu ambayo tuliona anastahili kufika. Leo hii hakuna anayemkumbuka Ramadhani Singano “Messi” kwa uharaka.
Ni nadra sana mtu kukumbuka kuwa Simba SC na Azam FC iliwahi kuwa na Ramadhani Singano “Messi” kwa sababu hakuna alama ambayo amewahi kuiacha akiwa Simba SC au Azam FC kutokana na kipaji chake.
Zile alama za Emmanuel Okwi akiwa Simba SC au Kipre Tchetche akiwa Azam FC ni vyepesi kukumbukwa kuliko mguu wa kushoto wa Ramadhani Singano “Messi” mguu ambayo ulitakiwa kuweka alama uwanjani kutokana na umaridadi wa mguu wake wa kushoto lakini kilichokosekana na jitihada katikati ya kipaji.
Jitihada katikati ya kipaji ndiyo iliyosababisha leo hii Shiza Ramadhani Kichuya awepo Namungo FC timu ambayo siyo ya daraja la kipaji ambacho alikuwa nacho. Shiza Ramadhani Kichuya alitakiwa kuwepo nje au sehemu ambayo ni kubwa kwa hapa Tanzania.
Shiza Ramadhani Kichuya ndiye mtu pekee ambaye angesababisha leo hii Simba SC wasiende Zimbambwe kumchukua Perfect Chikwende. Shibe ya mafanikio ya Shiza Ramadhani Kichuya ndiyo sababu kubwa ambayo imewafanya Simba kumsajili Perfect Chikwende.
Simba SC wapo katika michuano ya kimataifa. Michuano ambayo inahitaji wachezaji ambao wanaweza wakafanya maamuzi bora ndani ya uwanja kwa faida ya timu husika. Perfect Chwikende ana uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi sahihi katika eneo la mwisho la Simba SC
Perfect Chikwende ana uwezo wa kufunga magoli au kutengeneza nafasi za magoli katika eneo la mwisho la Simba SC. Mashindano ya ligi ya mabingwa barani Afrika yanahitaji wachezaji wa kufanya maamuzi sahihi katika kila eneo la uwanja.
Kufanya maamuzi sahihi ndani ya uwanja hakuhitaji kipaji kikubwa sana ndani ya uwanja ila jitihada ndiyo kitu cha msingi kinachohitajika kwa mchezaji ndani ya uwanja. Unaweza ukawa na kipaji kikubwa lakini jitihada isipokuwepo hakuna faida yoyote itakayoonekana kutokana na kipaji chako.
Siyo kwamba Perfect Chwikende ana kipaji kikubwa sana kuzidi Shiza Ramadhani Kichuya. Kitu pekee ambacho kilikosekana kwa Shiza Ramadhani Kichuya ni jitihada katikati ya kipaji chake na mafanikio yake.
Siyo kwamba anachokifanya Perfect Chwikende hawezi kukifanya Shiza Ramadhani Kichuya pengine Shiza Ramadhani Kichuya anaweza kukifanya kwa ukubwa kuzidi Perfect Chwikende lakini kinachowatofautisha ni jitihada katikati ya kipaji na mafanikio ndiyo maana Simba SC wakamsajili Perfect Chwikende na Shiza Ramadhani Kichuya yuko Namungo FC.
Comments
Loading…