in , , ,

Ndemla ana kipaji, kwanini makocha humweka benchi ?

Kuna kizazi ambacho kwenye akili yangu hakiwezi kufutika. Kizazi cha dhahabu katika klabu ya Simba SC, kizazi ambacho kilianza kusukwa kuanzia Simba B mpaka kikafanikiwa kupandishwa Simba A.

Ndicho kizazi ambacho ukimuuliza kocha msaidizi wa Simba SC, Selemain Matola lazima akiongelee kwa kujivunia. Mikono yake ilifanya kazi kubwa sana katika kufinyanga kizazi hiki bora cha Simba SC kwa wakati huo.

Ndicho kizazi ambacho macho yangu yalibarikiwa kumshuhudia mchezaji mzuri sana ambaye alikuwa anatokea pembeni huku akiwa na uwezo wa kufunga, Edward Christopher. Huyu ni aina ya wachezaji wa kisasa na kwenye soko la sasa wanahitajika sana.

Huyu alikuwa ana uwezo wa kufunga akitokea pembeni, kama ambavyo ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa au kama ilivyo kwa Simon Msuva wa sasa, Jardo Sancho au Raheem Sterling wa Pep Guardiola.

Edward Christopher alikuwa wa aina hii lakini kwa bahati mbaya hakutengenezewa mazingira ya yeye kukuza na kukiendeleza kipaji chake, leo hii sifahamu hata sehemu ambayo yupo, ila kama angekuwa na watu nyuma yake naamini Edward Christopher angekuwa mbali sana kwa sasa.

Tuachan e na huyu, kikosi hiki kiliwahi kumtoa Ramadhani Singano, huyu ambaye tulipagawa na kipaji chake na tukaamua kumwita Messi.Guu lake la kushoto lilikuwa tamu sana, kila aina ya mchoro mzuri ulikuwa unapatikana kwenye guu lake la kushoto.

Wakati unamtazama Ramadhani Singano “Messi” lazima jicho lako liwe linapita katikati ya uwanja kumtazama Jonas Mkude, huyu ndiye alikuwa kiranja mkuu wa hiki kikosi cha Simba B, hata walipopanda mpaka kikosi cha Simba kubwa alibaki kuwa nahodha wao.

Ni mtaalamu wa dimba, anajua kulimiliki dimba haswaa, Zao kubwa jingine la Suleman Matola kwenye Simba B, Ibrahim Ajib naye ni moja ya mazao ya Simba B. Kipaji kingine ambacho inasemekana kina miguu ya dhahabu.

Tuachane na hiyo miguu ya dhahabu, tuitazame kwa pamoja hii miguu ambayo wengi wetu tunaipenda, miguu ya Said Ndemla. Tunaipenda miguu ya Said Ndemla kwa sasa tunaiamini kuwa ina kipaji kikubwa sana.

Tunaimani nayo sana, wengi wetu huwa tunaiombea sana na kila uchwao huwa tunaamini kuna siku miguu hii itafika sehemu ambayo tunayotamani, tunayo imani kwa sababu bado ni mapema mno, giza halijafika sehemu ambayo yupo.

Bado yuko kwenye mwanga, anaweza akafanya chochote kile ambacho tunatakitamani sisi. Ndiyo maana tulifurahia sana tuliposikia habari ya yeye kwenda kufanya majaribio ulaya, lakini tuliumia tuliposhuhudia karudi nyumbani bila taarifa inayoeleweka ya kwanini amerudi.

Tulihuzunika, lakini tuliendelea kuwa na imani naye. Kuna swali kubwa sana ambalo mimi huwa najiuliza na huwa nakosa jibu sahihi, kwanini wengi wetu tunamwamini sana Said Ndemla lakini makocha wanaomfundisha hawajawahi kumwamini kama ambavyo tunavyomwamini sisi?

Jiulize ni kocha yupi wa Simba Sc ambaye alimwamini kwa asilimia kubwa Said Ndemla na kumpa nafasi ya mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza? Bila shaka jibu la swali hili ni hakuna kocha ambaye amewahi kumwamini Said Ndemla kwa kiwango hicho.

Hapa ndipo tunaweza kuanza kujiuliza kwanini hakuna kocha ambaye amewahi kumwamini Said Ndemla? Tatizo liko wapi, kwa kocha au Said Ndemla mwenyewe? Kama ni kwa kocha, ina maana kila kocha ana tatizo na Said Ndemla ?

Bila shaka jibu ni hapana, Said Ndemla kuna sehemu anakwama. Inawezekana miguu yake haishughulishi kwa kiasi kikubwa kama ambavyo sisi tunavyotamani aishughulishe. Kuna sehemu miguu ya Said Ndemla ni mizito, hapa ndipo mwanzo wake yeye kuanza kuweka wepesi kwenye akili na miguu yake.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Klabu EPL zinadeka

Tanzania Sports

Jamal Malinzi, Usiniulize alipo Yohana Nkomola