in , , ,

Tunazijua Vyema Sheria, Au Ni Mijadala Tu

Hatukatai kwamba mpira wa miguu ni mchezo wenye mvuto mkubwa ulimwenguni huku ukiwa na mashabiki wengi wenye shauku na hisia kali kuhusu mchezo huu. Hata hivyo, wengi wa wapenzi wa mchezo huu huingia viwanjani au hutazama kwenye runinga bila uelewa wa kina kuhusu sheria na kanuni za mchezo huu ambao wanaushabikia.

Kutokujua sheria ambazo zimekua zikiuongoza mchezo huu kumesababisha lawama nyingi kwa waamuzi na kupelekea mvutano usio wa lazima baina ya mashabiki,wachezaji na waamuzi. Kwa kawaida, matukio yanapokuwa na mvuto au kubadilisha mwelekeo wa mchezo waamuzi mara nyingi hupokea lawama kali kutoka kwa mashabiki na wadau wengine ambao hawajui vizuri sheria za mchezo wa soka.

Ni muhimu kuelewa kuwa sheria za mpira wa miguu zimewekwa na kudhibitiwa na shirikisho la soka duniani (FIFA) pamoja na bodi inayosimamia sheria za mpira (IFAB). Sheria hizi ni nyeti na hufafanua kila hali inayoweza kutokea uwanjani ambapo hapa tunaamisha kuanzia kutokea kwa faulo hadi goli, kutoka kwa mikono hadi kwa kuotea mpira (Offside).

Hata hivyo, kutokana na jinsi sheria hizi zinavyoweza kuwa ngumu na kubadilika mara kwa mara, mashabiki wengi wamekosa ufahamu wa kina, hali ambayo husababisha kutoelewa maamuzi ya waamuzi wanapokuwa uwanjani. Hili limekuwa chanzo kikubwa cha lawama kwa waamuzi hali ambayo pia huathiri mtazamo wa jumla kuhusu mchezo wa mpira wa miguu.

Ni vizuri kujisomea na kujifunza sheria na kanuni za mchezo husika
Ni vizuri kujisomea na kujifunza sheria na kanuni za mchezo husika

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matumizi ya teknolojia kama vile VAR (Video Assistant Referee) ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha usahihi wa maamuzi ya waamuzi japokua nayo katika baadhi ya lig ambayo wanatumia teknolojia hii imekua pia ikilaumiwa. VAR hutoa nafasi ya kuangalia tena matukio ya mashaka kama vile penalti, faulo na kuotea uwanjani.

Lengo la teknolojia hii ni kuhakikisha kuwa maamuzi ni sahihi na kupunguza lawama zisizo za lazima kwa waamuzi. Hata hivyo, matumizi ya VAR nayo yameibua mijadala mikubwa kutoka kwa mashabiki, baadhi wakidai kuwa inachelewesha mchezo na kuondoa ladha ya mpira ya hapo awali, ambapo maamuzi yalifanyika papo hapo. Hii pia inaashiria jinsi mashabiki wengi wanavyokosa uelewa wa jinsi teknolojia hii inavyofanya kazi na umuhimu wake katika kuhakikisha haki na usawa uwanjani.

Tatizo la kutokujua sheria linazidishwa zaidi na ukweli kuwa baadhi ya mashabiki wanaamini kwamba wanajua sheria zote za mpira wa miguu kwa kuwa wamekuwa wakitazama michezo kwa miaka mingi. Hata hivyo, si wengi wanaofahamu kwa undani sheria nyingi zinazohusiana na mpira wa miguu. Kwa mfano, sheria ya kuotea ni moja ya sheria zinazozua utata mwingi.

Mara nyingi, wakati mchezaji anapofunga goli lililohusisha pasi kutoka kwa mchezaji mwenzake, mashabiki wanaweza kushindwa kuelewa ni kwa nini goli limekataliwa kwa sababu ya kuotea. Kwa kawaida, waamuzi hufuata mwongozo wa sheria wa IFAB, lakini mashabiki wengi hawana uelewa wa kina wa sheria hii na hivyo kuanza kulaumu waamuzi bila kuelewa kiini cha maamuzi yao.

Pia, faulo zinazosababisha kadi nyekundu au ya njano zinaweza kuzua lawama kutoka kwa mashabiki ambao wanaamini kwamba mwamuzi ameonea mchezaji wao. Hii hutokea pale ambapo shabiki haelewi vizuri sheria inayohusu faulo na utoaji wa kadi. Kwa mujibu wa sheria za mpira, kadi hutolewa kulingana na ukali wa faulo na madhara yake kwa mchezaji mwingine. Kwa mfano, faulo inayohatarisha afya au usalama wa mchezaji mwingine inaweza kupelekea kadi nyekundu moja kwa moja. Mashabiki ambao mara nyingi hawana uelewa wa sheria hii, wanaweza kulalamika na kuhisi mwamuzi ameonea timu yao, hali ambayo ingeepukika kama wangejua sheria vizuri.

Kudhibiti hisia za mashabiki kuhusu maamuzi ya waamuzi inahitaji elimu zaidi kuhusu sheria za mpira wa miguu. Moja ya njia za kupunguza lawama zisizo za lazima ni kwa mashabiki kujielimisha kuhusu sheria mbalimbali za mchezo huu. Vyombo vya habari na mashirika ya soka yanaweza kuchukua jukumu la kuwaelimisha mashabiki kwa njia nyepesi na rahisi kueleweka. Hii inaweza kufanyika kupitia vipindi maalum vya televisheni au machapisho ya kila mara yanayohusu sheria za mpira wa miguu. Wachezaji na makocha pia wanaweza kushiriki katika kufafanua sheria hizi kwa mashabiki wao ili kuhakikisha kuwa matukio yanayoibua maswali yanaeleweka kwa usahihi.

Kwenye vijiwe vyetu hivi ambavyo mara nyingi huwa tunakaa na kuzungumza mpira huwa tunaona kuwa kutojua sheria za mpira wa miguu ni tatizo linalochochea lawama zisizo za lazima kwa waamuzi na kuzua migogoro isiyo na msingi viwanjani. Ili kuondoa changamoto hii, elimu kuhusu sheria za mchezo ni muhimu. Mashabiki wanahitaji kujifunza na kufahamu zaidi kuhusu sheria hizi, huku vyombo vya habari na mashirika ya soka yakifanya juhudi za kutoa elimu.

Kwa kufanya hivi watasaidia kuboresha mwelekeo na mtazamo wa jumla kuhusu mpira wa miguu na matokeo yake, mashabiki wataweza kufurahia mchezo kwa uelewa zaidi na kuacha lawama zisizo na msingi kwa waamuzi japokua najua ni kitu ambacho hakitawezekana kwa soka letu la Afrika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Rodri amechukua Tuzo ya Carvajal na Ronaldo

Tanzania Sports

Ligi Kuu Ya Tanzania Ni Bora Au Pendwa?