*Setif na Vita Club zatinga fainali
Klabu yenye washabiki wengi ya TP Mazembe wametupwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Mazembe wamezidiwa nguvu na Waalgeria wa Entente Setif kwa bao la ugenini.
Katika mechi ya wikiendi hii, Setif walishinda 3-2 katika mechi iliyopigwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika mechi ya kwanza nchini Algeria, Mazembe walifungwa 2-1, hivyo mizania inaonesha kwamba wamekwenda 4-4 na Waalgeria wakavuka kwa wingi wa mabao ya ugenini.
Mabao yote ya Setif yalitokana na majalo, yakimwacha hoi kipa mwenye mbwembwe, Robert Kidiaba. Abdelmalek Ziaya alifunga bao zuri katika dakika ya nane tu, wakati Sofiane Younes akitoka benchi alifunga bao kipindi cha pili.
Mazembe walicharuka na kupata mabao kupitia kwa Daniel Adjei, Salif Coulibaly na Joel Merikani
Setif waliwaumiza Mazembe dakika 11 tu kabla ya mechi kumalizika walipofunga bao na kufanya wawe nguvu sawa na kuingia fainali kwa mara ya kwanza tangu 1988 walipofika fainali.
Sasa Setif watakabiliana na Wakongomani wengine, AS Vita Club kwenye fainali, ambapo kama Mazembe wangevuka ingekuwa fainali ya kihistoria kukutanisha timu za taifa hilo.
Vita wameingia fainali baada ya kuwatoa CS Sfaxien wa Tunisia kwa jumla ya mabao 4-2.
AS Vita Club wataanza kuwa wenyeji wa Entente Setif Oktoba 26 kwenye fainali ya kwanza kabla ya kusafiri hadi Algeria Novemba mosi.
Comments
Loading…