in

TFF wamekosea uzani wa ‘Play-off’ ya kupanda na kushuka Ligi

Ligi Kuu Tanzania

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania umemalizika huku Simba wakitetea ubingwa wao. Msimu huo ulikuwa na mambo mengi yaliyojitokeza kwenye mchezo wa soka ndani na nje.

Malalamiko kuanzia utatanishi wa uamuzi ya waamuzi,ubovu wa viwanja vingi vya soka,ubora wa timu,viongozi kutokuwa na welediwa kutosha, ushirikina kudhaniwa ni chachu ya mafanikio ya soka nchini Tanzania na mengineyo mengi.

Timu za kushuka daraja tayari zilishajulikana na zile za kucheza mtoano nazo zilipatikana hadi siku ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu. Baadhi ya mambo mazuri katika Ligi yetu tumeyaona na kufurahia.

Lakini yapo mengine ambayo bado yanatatiza na namna gani kanuni za Shirikisho la Soka TFF zilivyokosa uzani, jambo ambalo linaweza kusaidia kuondokana na mzigo wa kero zilizopo kwenye Ligi yetu.

Katika makala haya tuangalie namna mfumo unaotumika wa kucheza michezo ya mtoano ya timu za kupanda Ligi kuu na kushuka maarufu kwa lugha ya kimombo kama ‘Play-off’.

Timu mbili za Ligi kuu ambazo zimecheza mechi za mtoano ni Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro dhidi ya  Transit Camp Dar es salaam na Coastal Union ya jiini Tanga dhidi ya Pamba ya jijini Mwanza.

Mtibwa Sugar na Coastal Union zote zimefanikiwa kubaki Ligi Kuu baada ya kushinda michezo yao ya marudiano. Michezo ya kwanza Mtibwa waliifunga Transit Camp mabao 4-1, wakati Coastal Union walitoa sare 2-2.  Pamba ilishuka Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2000 na tangu hapo haijafua dafu kurejesha hadhi yake ya soka na kuamsha hamasa katika ukanda wa ziwa hususani jijini Mwanza ambako kwa muda mrefu wamekosa burudani ya timu yao kwa sababu Toto Africans nayo tangu ilipoporomoka haiawahi kurejea tena Ligi kuu.  

Madaraja ya timu hizo nne zilizocheza mechi za mtoano hayalingani. Mtibwa Sugar na Coastal Union zipo daraja la juu uzani,uwezo na uzoefu kuliko Pamba na Transit Camp.

Kimsingi madaraja hayo yanathibitisha kuwa TFF ingeweza na ilipaswa kutengeneza utaratibu tofauti ambao timu zingecheza zenyewe kwa zenyewe kwenye mechi za mtoano ili kupanda,kushuka au kubaki Ligi Kuu.

Kwa mfano, Pamba haina uzoefu wala uwezo wowote wa kuitupa nje Coastal Union ambayo imecheza Ligi Kuu na vilabu vikali na hivyo kiuwezo na viwango  haviwezi kulinganishwa na Pamba.

Hii ina maana kwa maoni yangu Pamba walipaswa kucheza na timu ya Ligi darajala kwanza ambayo inapigania nafasi ya kupanda Ligi Kuu kuliko kucheza dhidi ya tiu inayotoka ligi kuu na kupigania kutoshuka daraja.

Kwa mfano Pamba walitakiwa kumenyana na Transit Camp ili kupata timu moja itakayopanda Ligi Kuu. Vilevile kwa Mtibwa Sugar na Coastal Union zilipaswa kucheza zenyewe kwa zenyewe za Ligi Kuu kwa sababu ya hadhi zao.

Mtibwa na Coastal zilitakiwa kuchuana kuamua nani kati yao anabaki Ligi Kuu ili mmoja ashuke daraja. Zote ni timu za Ligi kuu na ambazo zinalingana kwa hadhi na viwango vya mahali zilipo.

Lakini kuzipambanisha Mtibwa na Transit Camp kisha Coastal na Pamba ni kutowatendea haki wachezaji na timu nzima za Ligi daraja la kwanza.

Kwa sababu timu hizo hazilingani kwa hadhi zao, ilibidi Pamba sasa wakamuane na Transit huko huko daraja la kwanza kuamua wa kupanda na kushuka.

Unapozipambanisha timu za daraja moja maana yake uwiano wao na hadhi zao zinalingana. Lakini kuzipambanisha na timu za Ligi Kuu Mtibwa na Coastal ni sawa na serikali kuwaamuru wanafunzi wa kidato cha kwanza kufanya mitihani ya kidato cha sita au wanafunzi wa kidato cha nne kwenda kufanya mitihani ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya mwaka wa mwisho.

Uzani wao haulingani na daima inaonekana si mantiki kabisa na inaonesha sisi sio watu kanuni. Kimsingi maoni yangu yanajikita katika mfano wa Ligi Kuu England, ambako timu za daraja la kwanza zenyewe kwa zenyewe hucheza mechi za mtoano ili kupata mshindi ambaye anapanda Ligi Kuu EPL.

Na sio kumchukua Newcastle United au Cryastal Palace aende kuoambana na Derby Country au Reading. Madaraja au hadhi za timu hizi ni tofauti, ni sawa na kanuni za mchezo wa ndondi lazima uzito  na uzani wa wanandoni uzingatiwe.

Kuzipamabanisha timu za Ligi Kuu Bara na Ligi daraja la kwanza ni kudidimisha ari,nguvu, uwezo na maendeleo ya timu za daraja la kwanza. Kama timu zilizopo kwenye mstari wa kushuka Ligi Kuu kwenda la daraja la kwanza, inatakiwa zilizopo kwenye mstari hatari zipambanishwe kwenye uwanja huru au mechi za nyumbani na ugenini kuamua mshindi kati yao.

Vilevile kwa timu za daraja la kwanza ambazo zipo kwenye mstari wa kushuka daraja kwenda la daraja la pili zinatakiwa kupambanishwa zenyewe kwa zenyewe kwa mechi kucheza kwenye uwanja huru au ugenini na nyumbani ili kuamua mshindi.

Wale wa daraja la kwanza wapambane wenyewe kwa wenyewe kuamua nani anabakia na nani anashuka kwenda la pili. Wale wa daraja la pili nao wapambane wenyewe kwa wenyewe ili kuamua nani anabakia na nani anashuka daraja la pilikwenda la tatu huko.

Hivi ndivyo tunaweza kuzingatia uzani wa kupambanisha timu za kupanda,kushuka na kubaki katika Ligi zetu. Narudia uzani wa timu za Ligu kuu za Mtibwa, Coastal dhidi ya timu za daraja la kwanza za Pamba na Transir Camp haulingani na wala haukupaswa kupambanishwa.

Pamba angemenyana na Transit Camp ili kuamua mshindi. Mshindi kati yao ndio angelipanda daraja. Vivyo hivyo kwa Mtibwa na Coastal Union zilipaswa kupambana zenyewe kwa zenyewe zenye uzani sawa kuamua nani kati yao anabaki Ligi Kuu Tanzania Bara. Nimeona namna hiyo kwa leo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Using trained Gymnasts to entertain politicians won’t win Tanzania Olympic Glory

Mbappe

Kama si pesa basi Mbappe atatafuta mataji