in

Nini chanzo wachezaji wetu kurudi kutoka Ulaya?

Wachezaji wetu

YANGA wamemsajili mwanasoka Farid Mussa aliyekuwa akikipiga katika klabu ya Tenerife ya Hispania. Winga huyo ni miongoni mwa wachezaji wapya waliojiunga na wakali hao wa mitaa ya jwangwani na twiga jijini Dar es salaam.

Mussa anakuwa miongoni mwa mastaa wa Tanzania ambao hawajafurukuta katika soka huko barani Ulaya. Haijawekwa bayana sababu za kukacha kuendelea kucheza Tenerife ingawaje kuhama timu linaweza kuwa suala la kawaida.

Baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kutimka Ulaya na kurejea nchini ni kama Haruna Moshi na  Shomari Kapombe. Mwaka 2011 Shomari Kapombe alikwenda kufanya majaribio nchini Ufaransa akiwa na Benjamin Mendy ambaye kwa sasa ni beki wa kushoto wa Manchester City.

Wakati unapomtazama Mendy uwanjani kisha kumgeukia Kapombe kuna swali unajiuliza, nini kinachotokea kwa nyota wetu. Je, ni nini tafsiri ya nyota hao kurejea kisoka? Makala haya yanajaribu kubainisha sababu mbalimbali.

WAKALA

Duru za kimichezo zinasema mawakala wana mchango wa kufeli au kufanikiwa kwa mchezaji. Ukweli mwingine ni kwamba unaweza kukuta wakala anayempeleka mchezaji  huko nje ya nchi naye ni mbabaishaji. Anakuwa anamdanganya mchezaji kuwa anampeleka sehemu nzuri kumbe juu tu, hivyo sio suala la wachezaji kukosa viwango.

NIDHAMU

Katika eneo hilo mchezaji anatakiwa kuonesha jitihada, kujitambua, uvumilivu na kujituma. Wakala hata anaweza kuwa na mapungufu yake lakini kuchukua hatua ya kumvusha mchezaji kutoka yake hadi nchi ya kigeni ni juhudi tosha.

“Nina uhakika kikubwa kilichowaangusha ni nidhamu ya mchezo wa soka. Kwenye soka la kulipwa katika nchi za enye mafanikio zaidi hili ni jambo muhimu sana kwa mchezaji ili awe bora na afanikiwe. Nidhamu nikimaanisha kuanzia mazoezi, mazoezi ya ziada, vyakula,mtindo wa maisha, kufuata ratiba. Kwa ujumla kujikita, kuwa na ndoto na utayari wa kujifunza na kuboresha. Wachezaji wa Afrika magharibi wenzetu wametuzidi kwenye hivi vitu ndio maana wanafanikiwa sana,” anasema shabiki mmoja wa kandanda alipozungumza na mwandishi wa makala haya.

UVUMILIVU

Je, wachezaji wetu si wavumilivu kama Mbwana Samatta? Hii nayo inatajwa kuwa miongoni mwa sababu za wachezaji wetu wanaorejea kutoka Ulaya.

Chukulia mfano wa Haruna Moshi alipata timu iliyoko iko Ligi Kuu Sweden, na iko kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa wamecheza mechi moja na Manchester United katika makundi ingawa walifungwa mabao 3-0 ya Dietmar Berbertov. Siku hiyo ndio Haruna Moshi alitambulishwa, wakamchukulia hadi familia yake aende nayo. Akiwa huko Sweden hakudumu na kurudi nchini. Haruna alishindwa kufuata nyayo za John Obi Mikel ambaye baadaye akaenda zake Chelsea kupitia timu hiyo hiyo. Na kama kipaji Hatua Moshi anacho cha uhakika ndiyo maana alisajiliwa na klabu hiyo.

MAHITAJI YA TIMU

Tatizo lingine ni moja, ukiacha hilo la uvumilivu. Wachezaji hupelekwa bila vilabu husika kuwahitaji. Utasikia tu mchezaji amekwenda kujiunga na klabu kama Tenerife ya Hispania na sio Tenerife wanamtaka mchezaji fulani. Kwa mfano, Mbwana Samatta alipokuwa akichezea klabu ya TP Mazembe alitakiwa na wale timu ya Genk inayoshiriki Jupier League hivyo wakamuamini na hawakuwaangusha. Hivyo basi mchezaji anaweza kuwa na kipaji lakini sio sehemu ya mahitaji ya timu. Unaweza kukuta timu inayo wachezaji wake katika akademi wa kiungo, mashambuliaji,winga au golikipa. Hilo linasababisha klabu kuona hakuna ulazima wa kumchukua mchezaji wa kigeni katika eneo ambalo hawahitaji.

Aidha, inawezekana licha ya wachezaji kuwa na vipaji lakini wanakuwa katika hali ya kawaida, kwamba sio kipaji maalumu ambacho kitaitikisa klabu. Wapo wachezaji ambao wamewahi kuachwa na timu mbalimbali kutokana na sababu hii ya mahitaji ya timu.

NAFASI YA TANZANIA

Kwa mujibu wa takwimu za viwango vya soka vya FIFA, Tanzania inashika nafasi 134. Hii ni nafasi mbaya mno katika maendeleo ya soka letu. Kwa vyovyote inawanyima wachezaji kupata fursa ya kuonekana katika klabu vilabu mbalimbali.

Wachezaji wa Tanzania hawajatamba katika soka la Afrika. Katika Ligi za kubwa barani Afrika kama vile Afrika kusini,Misri,Tunisia, Morocco,Zambia, wachezaji wetu hawajakuwa lulu licha ya wengi kujaribu.

Samatta aling’ara barani Afrika ndipo maana akaonekana mbele ya mabosi wa Genk waliomhitaji. Aston Villa walimwona Samatta akiwa mechezaji kwa kiwango cha juu Jupiter League.

Tofauti na wachezaji wengine ambao wanakwenda barani Ulaya lakini wanakuwa na wasifu mdogo binafsi na wan chi. Nchi za Afrika magharibi zimezoeleka kutoa wachezaji wakali na wengine wanapata fursa kwa sababu ya mtandao uliowekwa miaka mingi huko nyuma. Nafasi hii 134 inachangia kutopewa nafasi ya kutosha licha ya upungufu tulionao kwa wachezaji wetu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Leeds United

Leeds United kubebwa tena na uchawi wa Bielsa?

HERSI

Waliombeba Injinia Hersi watakuja kumshusha!